img

Zitambue hatua 7 za maumivu zisizoepukika kabla ya kufanikiwa

December 3, 2020

Mafanikio ni safari ndefu. Katika safari ya mafanikio kuna mengi, milima na mabonde yasiyotabirika. Wengi huanza safari ya mafanikio wakiwa na malengo makubwa, lakini wanasahau kuwa kufanikiwa ni kupambana na changamoto bila kukata tamaa huku ukiyatazama malengo na maono yako. Kama unalenga kufanikiwa katika maisha yako ni vyema ukazifahamu hatua hizi saba za maumivu zisizoepukika katika safari hiyo.

1. Utahisi maumivu
Kila mtu aliyefanikiwa amepitia kwenye safari yenye maumivu; ikumbukwe kuwa kupita njia yenye changamoto ndiko hutuelekeza kwenye mafanikio.

Jifunze kutumia changamoto na maumivu kuwa kama hamasa ya kufanya juhudi zaidi kufikia mafanikio. Hakuna haja ya kulalamika na kukata tamaa bali anzia ulipo kwenda mbele ili kukamilisha malengo yako.

2. Kutamani kukata tamaa mapema
Wengi waanzapo safari ya mafanikio huanza kwa kasi kubwa kwani wao hufikiri tu juu ya mafanikio. Lakini katika ukweli halisi ni kuwa, mwanzoni kuna changamoto lukuki ambazo usipotazama malengo yako ni rahisi kukata tamaa.

Kipindi hiki kimekuwa kigumu sana kwa watu wengi kwani hawaoni ile nuru ya awali tena bali wanaona changamoto kila kukikucha. Kumbuka wahenga walisema “mwanzo ni mgumu”; jitahidi usirudi nyuma nawe utaona matokeo yake.

Mambo ya kufanya kama unataka kukata tamaa:

Uliza waliokutangulia walifanyaje kutatua hizo changamoto unazoziona.

Soma vitabu na makala mbalimbali za kukuhamasisha.

Jikumbushe juu ya malengo yako na matokeo utakayoyapata utakapokuwa umevuka kwenye hizo changamoto.

3. Utapoteza mahusiano na watu
Katika safari ya kuelekea kufanikiwa mambo mengi hutokea, kama vile kupoteza fedha, vitu, watu n.k. Kumbuka kuwa siyo watu wote watakaoweza kwenda pamoja na wewe katika safari hii, kwani kuna wengine hawana hamasa uliyo nayo, hawapendi ufanikiwe, wana mambo au shughuli zao n.k.

Hivyo usishangae hata watu wa karibu uliokuwa unawategemea wakakuacha bila msaada wowote au wakabadilika sana. Jipe moyo, fanya bidii tambua mnufaika wa kwanza wa mafanikio yako ni wewe wala sio wao.

4. Utakatishwa tamaa
Katika njia ya mafanikio kuna watu wachache sana wenye mawazo chanya na wanaopenda mafanikio yako. Hivyo basi, utakutana na watu wengi sana watakao kukatisha tamaa na kukutisha ili urudi nyuma.

Utawasikia wakisema hili hautafanikiwa, hili halikufai, fulani alifanya akashindwa, halinipi faida, n.k. Jambo la kufanya hapa ni kulinda fikra na nafsi yako visipokee mawazo na misimamo ya hawa watu; kwani kwa kufanya hivi utaweza kutazama tu lengo lako na kufanya bidii kulifikia.

5. Utachukiwa bila sababu
Kwa hakika binadamu hapendi mafanikio ya mwingine, moyo wake hujaa chuki, maumivu na husuda pale mwingine anapofanikiwa. Wapo watu wanaotamani ubaki kama ulivyo na usiweze kufanya kitu cha kuwazidi wao au walichoshindwa kukifanya.

Nimeshuhudia marafiki zangu kadhaa wakipunguza uhusiano na mimi pale waliponiona nimepata mafanikio kadhaa hasa kuwazidi wao. Hivyo basi, badala ya kupambana na wenye wivu na chuki pambana na malengo yako, kisha mafanikio yako yatawapa somo.

6. Utajilaumu mwenyewe
Kujilaumu hakuepukiki katika safari ya mafanikio hasa pale unapokuwa umepata tatizo au hasara kwa uamuzi ulioufanya hapo awali. Kwa hakika, huwezi kubadili uamuzi au tendo lililopita; badili uelekeo wa maisha yako ya baadaye kuanzia ulipo. Usijilaumu tena kwani utauwa ile hamasa yako ya dani na hutoweza kufikia mafanikio yako.

Kumbuka haya:

Jana haiwezi kubadilishwa tena

Makosa au kushindwa ni somo zuri la kufanya maamuzi mazuri ya baadaye

Kesho inatengenezwa leo na wala si jana au juzi

7. Utaanguka
Kuanguka ni hatua inayowakabili watu wengi sana katika safari yao ya mafanikio. Tatizo ni namna watu wanavyoshughulikia kuanguka kwao, kumbuka “Usiulize umeangukia wapi bali uliza umejikwaa wapi”.

Kwa mfano inawezekana umekopa mkopo na umepata hasara katika biashara na kupoteza fedha nyingi, badala ya kuendelea kulalamika tafuta namna ya kuziba pengo hilo ili uweze kuendelea mbele. Kujifunza kutafuta tatizo na chanzo chake kutakuwezesha kuliepuka wakati mwingine mbeleni.

Neno la mwisho:

Nakukumbusha tena na tena kuwa safari ya mafanikio inahitaji jitihada nyingi na kutokata tamaa. Kumbuka kuwa wanaojaribu mchezo wa riadha na kuacha njiani hawapewi tuzo bali wanapewa wale walioshinda pekee. Jitahidi kufanya bidii bila kuruhusu kukata tamaa au kurudishwa nyuma na mtu au kitu chochote.,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *