img

UN: Libya ina wapiganaji 20,000 wa kigeni na mamluki.

December 3, 2020

Kaimu mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya, Stephanie Williams amesema uwepo wa wapiganaji wa kigeni nchini Libya ni ukiukwaji wa uhuru wa nchi hiyo. Akizungumza kwenye mkutano wa jukwaa linalojadili mustakbali wa kisiasa wa Libya uliofanyika kwa njia ya mtandao, Williams aidha amesema uingizaji wa sialaha nyingi Libya ni ukiukwaji wa kikwazo cha silaha kilichowekwa dhidi ya taifa hilo.

Jukwaa jilo lenye wanachama 75 linajaribu kuzipatanisha pande zinazohasimiana nchini Libya zikubaliane mpango utakaoanzisha utawala wa mpito kuiongoza nchi hiyo kuelekea kufanya uchaguzi wa rais na wa bunge Desemba mwaka ujao.

Mkutano huo ni sehemu ya jitihada za Umoja wa Mataifa kufikisha mwisho machafuko yaliyoigubika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta baada ya kupinduliwa na kuuliwa kiongozi wa zamani wa Libya, Muamar Gadhafi. Nchi hiyo sasa imegawanyika pande mbili, upande wa mashariki na magharibi kati ya tawala mbili hasimu, kila upande ukiungwa mkono na mlolongo wa makundi ya waasi na dola za kigeni. Kamanda wa kijeshi Khalifa Haftar anatawala mashariki na kusini, huku serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa yenye makao yake katika mji mkuu, Tripoli, ikidhibiti eneo la magharibi.

Moammar Gadhafi

Libya imeingia katika mzozo unaoendelea tangu kifo cha kiongozi wa taifa hilo Moammar Ghadhafi na kuzidi kugawanyika.

Umoja wa Mataifa umekata tamaa?

Kauli ya Williams inaashiria hali ya kukata tamaa inayotokana na kukosekana katika suala la wapiganaji wa kigeni na mamluki kuondoka Libya, suala ambalo lilikuwa sehemu ya mkataba wa kusitisha mapigano ulioafikiwa mwezi Oktoba mwaka huu. Mkataba huo uliweka muda wa miezi mitatu wapiganaji wote wa kigeni waondoke Libya. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, maelfu ya wapiganaji, wakiwemo Warusi, Wasyria, Wasudan na Wachad, wamepelekwa Libya na pande hasimu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipanga kuwasilisha mapendekezo kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufikia mwishoni mwa Novemba kuhusu njia zinazoweza kutumika kusimamia usitishwaji mapigano Libya. Hata hivyo kwa mujibu wa barua ya Guterres iliyowasilishwa kwa baraza la usalama, aliahirisha hadi mwisho wa mwezi huu kwa kuwa pande zinazohasimiana bado zinashauriana juu ya vipengee muhimu kuhusu usimamiaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Williams aidha amezikosoa serikali za kigeni ambazo hakuzitaja kwa kuchukua hatua bila kujali wala kuwa na hofu ya kuwajibishwa kisheria na hivyo kuuchochea zaidi mgogoro wa Libya kwa kutumia mamluki na silaha.

Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa pia ameonya juu ya hatari ya kusambaratika kwa gridi ya taifa ya umeme nchini Libya kwa sababu ya rushwa na usimamizi mbovu. Amesema uwekezaji wa thamani ya dola bilioni moja katika miundombinu ya umeme unahitajika mara moja, ikizingatiwa kwamba viwanda 13 kati ya 27 vya kufua umeme vya Libya vinafanya kazi. Amesema inatarajiwa Walibya milioni 1.3 kati ya wakazi jumla milioni 6.8 kuhitaji msaada wa chakula Januari mwakani.

Mashirika: ape.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *