img

Waridi wa BBC: Sikudhani ningetoka hospitalini nikiwa hai

December 2, 2020

Dakika 7 zilizopita

Jahmby Koikai

Maelezo ya picha,

Kila siku zake zilipokaribia, alikuwa anapatwa na uchungu mwingi.

Jahmby Koikai alipoanza kupata hedhi akiwa na miaka 13, badala ya kuanza awamu ya matumaini maishani, alianza kipindi kigumu cha mahangaiko si haba.

Kila siku zake zilipokaribia, alikuwa anapatwa na uchungu mwingi.

Jahmby ni miongoni mwa wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa wa endometriosis. Endometriosis ni ugonjwa ambao huhusisha seli zinazofaa kuwa ndani ya mji wa uzazi kuwa nje ya mji huo.

“Sikuwahi kufikiria kuwa siku yangu ya kwanza kuanza kupata hedhi ningeweza kuanza kupata maumivu makali ambayo yamekuwa ni vita vikali katika maisha yangu,” anasema Jahmby.

Kugundua tatizo

Kuanzia hapo kila mwezi hedhi zake ziliandamana na uchungu usioeleweka.

Lakini licha ya uzito wa tatizo hilo Jahmby alikuwa anavumilia hali, akidhania kuwa kila mwanamke alikuwa anapitia hayo wakati wa hedhi.

Jahmby alilelewa na mama yake pamoja na bibi , na anasema walimfundisha haja ya kuwa mvumilivu na mkakamavu katika kila hali za maisha. Na kwa hivyo, nyakati za hedhi jamii yake ilimtaka atumie dawa za kumsaidia kustahimili uchungu ulioandamana na hedhi. Kwani wakati huo hakuna aliyefahamu tatizo lake.

Wakati huo ilikuwa kama siri ya jamii yake Jahmby lakini pindi alipoendelea kukomaa uchungu na kasi ya damu ya hedhi vilizidi.

Jahmby Koikai

Maelezo ya picha,

pindi alipoendelea kukomaa uchungu na kasi ya damu ya hedhi vilizidi.

Masomo yake hususan ya chuo kikuu yalikumbwa na misukosuko mingi tu , na wakati mwingi alikuwa hawezi kumakinika chuoni wakati wa hedhi yake.

Anakumbuka nyakati ambazo karatasi za mtihani zingekuwa mbele yake lakini kwa uchungu angekosa kuandika chochote. Hali hii ilimfanya arudie masomo na kuchelewa kuhitimu chuo kikuu.

Licha ya hayo Jahmby alitamani sana kuwa mtangazaji maarufu nchini Kenya na kwa hivyo alikamilisha chuo kikuu licha ya taabu.

Alijitosa kwenye utangazaji na akawa amesifika nchini Kenya kwa mtindo wake wa kupeperusha habari na masuala yanayohusu mziki na maisha ya wafuasi wa nyimbo za mtindo wa reggae na miondoko yake.

Kati ya 2015-2007, hali yake ilidhoofisha afya yake mno, kiasi cha kuathiri utendakazi wake .

Jahmby Koikai

Ni nyakati hizo ambapo Jahmby alianza kuwa mkakamavu na kuweka bayana matatizo yake hayo, alijitokeza kwa umma kuzungumzia hilo.

Hii ni hali ambayo kwa wanawake wengi ingelikuwa ni siri ya mtungi.

Hapo ndio mshabiki wake walipoanza kuelewa ni kwanini mwili wake ulionekana kudhoofika mno kwenye runinga .

Upasuaji hatari

Jahmby Koikai , aliendesha kampeni iliyofanikiwa ya kuchangisha fedha kupitia kampeni mbali mbali , shughuli hii ilimwezesha kukidhi gharama za matibabu huko Marekani .

Mwaka wa 2018 yeye na mama yake waliandamana hadi jimbo la Atlanta, mji mkuu wa jimbo la Georgia kutafuta matibabu zaidi .

“Wakati huo nilikuwa nimedhoofika mno kiafya , lakini sikukata tamaa ya kuwa ningepona na kurejelea ndoto zangu,” anasema Jahmby

Jahmby Koikai

Maelezo ya picha,

Alipokuwa anasafiri kwenda Marekani kupata matibabu, alifikiri atakuwa hospitalini kwa siku tatu na atarudi Kenya baada ya mwezi.

Alipokuwa anasafiri kwenda Marekani kupata matibabu, alifikiri atakuwa hospitalini kwa siku tatu na atarudi Kenya baada ya mwezi.

Mambo yakawa mabaya kuliko vile alivyofikiria. Matibabu yake ambayo yalihusisha upasuaji mara kadhaa yalikumbwa na changamoto na mapafu yake yalikuwa yameathiriwa na kuingiliwa na seli za hedhi. Hali hii ilizidisha ugumu wa matibabu.

Haya yakifanyika hospitalini asijue kuwa kuna watu waliokuwa tayari wameanza kuzungumza huku na kule wakisema kuwa hatarudi akiwa hai.

Jahmby anasema alitengwa na baadhi ya marafiki wa karibu mno naye. Baadhi walinukuliwa kwenye baadhi ya mitandao nchini Kenya kwa madai kuwa alikuwa ameaga dunia akiwa hospitalini Marekani.

Ila kile ambacho watu wengi walikuwa hawajui ni kuwa Jahmby alikuwa anapigania uhai wake akiwa chumba cha upasuaji mara kwa mara.

Wasiwasi wakati wa upasuaji

“Wakati wa upasuaji, mapafu yangu yalizua changamoto kubwa kwa madaktari kwani mapafu yangu ya kulia yalikuwa yanaporomoka mara kwa mara. Shida hii na zingine nilizozipata, pamoja na moyo wangu kuwa na matatizo na hata mfumo wa meno yangu, ilihitaji ufuatiliaji wa karibu na madaktari na wauguzi,” anasema.

Anapofikiria alipotoka kwenye mashine zilizokuwa zinausaidia mwili wake hospitalini, anafahamu ni mapenzi ya mwenyezi Mungu kwamba yuko hai leo .

“Siku moja kabla ya upasuaji, mmoja wa madaktari wa upasuaji alinishika mkono na kuniombea. Hii ilisaidia sana kupunguza wasiwasi wangu. Ujuzi na maarifa yaliyoonyeshwa na timu nzima yalikuwa vya kushangaza. Ninawashukuru milele kwa matibabu ya kubadilisha maisha niliyopokea,” anasema Jahmby.

Jahmby Koikai

Maelezo ya picha,

‘Sikudhani ningetoka hospitalini nikiwa hai’

“Lakini pia kuna upasuaji mmoja ambao sitowahi kuusahau huu ulikuwa wa dharura, kabla sijaondoka hospitalini. Iligunduliwa tena kuwa nilikuwa na maji kwenye mapafu yangu. Tayari nilikuwa nimepitia uchungu mwingi wa kuondolewa maji, ila mchakato wa kujaribu tena kutoa maji yale nusura unitoe uhai wangu,” Jahmby anakumbuka.

Mwanadada huyu anasema kuwa dawa alizowekewa kwenye mishipa yake iliusukuma mwili wake kuishiwa na nguvu.

Anasema kuwa pale kwenye chumba cha upasuaji alikuwa nusura akate roho, ila kilio na mayowe ya mama yake mzazi vilimrejeshea fahamu.

Akiwa katika ile hali ya kuzirai alihisi ndani yake kuwa apigane kuwa hai. Polepole uhai ulianza kumrejea.

Alikaa miaka miwili huko Marekani akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa endometriosis.

Alirudi Kenya mnamo Januari mwaka huu na amekuwa katika safari ya kujitafakari mno hasa kwa kuwa anaamini yeye kuwa hai leo ni muujiza mkuu.

Jahmby anasema kuwa tangu alipoanza kuwa na matatizo ya Endometriosis amefanyiwa upasuaji mara 21.

Tangu arudi nyumbani, afya ya Jahmby imeimarika sana, ingawa bado huwa anameza dawa.

Jahmby Koikai

Maelezo ya picha,

Jahmby anasema kuwa tangu alipoanza kuwa na matatizo ya Endometriosis amefanyiwa upasuaji mara 21.

“Ninajisikia vizuri sana. Aghalabu mapafu yangu hayajakuwa na matatizo kwa miezi miwili iliyopita, hedhi yangu haijakuwa na maumivu na hakuna hitaji la dawa za kupunguza maumivu. Ni muujiza na ninamshukuru sana Mungu,” anasema.

Jahmby sasa ameanza kujenga uelewa juu ya endometriosis na ana hamu ya kuona wanawake wengi wanaougua maradhi hayo wanapata utambuzi na matibabu sahihi.

Jahmby, ambaye hapo awali alifanya kazi kama mtangazaji , anasema lengo lake sasa ni kuendesha miradi huru na pia kujenga wakfu wake ili kupaza sauti yake ndoto na azma zake, ambazo bilashaka zimeimarika baada ya pandashuka za ugonjwa wa huo.

Ugonjwa wa kukua kwa tishu za mfuko wa kizazi

Endometriosis ni ugonjwa wa wanawake ambapo tishu zinazotengeneza ukuta wa ndani wa mfuko wa uzazi hukua sehemu ya nje ya mfuko wa uzazi.

Hali hii hutokea wakati ukuta wa ndani wa mfuko wa uzazi unapokua juu ya mfuko wa mayai ya uzazi au ovari, utumbo, na tishu zilizopo kwenye mifupa ya kiuno .

Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na

  • Maumivu ya kuchoma sehemu ya kiuno
  • Makovu maeneo ya uzazi
  • Mwanamke kukosa uwezo wa kushika mimba
  • Maumivu makali kabla au baada ya hedhi
  • Maumivu makali wakati wa tendo la ndoa
  • Maumivu ya tumbo, mgongo na maeneo ya mafupa nyonga (pelvis)
  • Maumivu unapotaka kwenda kujisaidia/kwenda haja ndogo
  • Kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi, damu hiyo inaweza kuwa au kutokuwa na mabonge.
  • Kuwa na hedhi ya muda mrefu isivyo kawaida.
  • Kupata hedhi kabla ya muda wa kawaida

Chanzo cha ugonjwa

Sababu kuu ya kupatwa na hali hii ni ya kiukoo ambapo mwanamke ambaye baadhi ya ndugu zake wa karibu walishapata ugonjwa huu basi na yeye huwa yumo hatarini kuupata.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *