img

Wanafunzi ndio wanaoambukizwa HIV kwa wingi nchini Kenya

December 1, 2020

Kaunti za eneo la kanda ya Ziwa zinaongoza kwa idadi ya maambukizi. Kwa mwaka huu pekee watu elfu 20 wamefariki kwa ukimwi wengi wao wanaume.

Baa la corona nalo limezua utata mpya kwani dawa za kupambana na makali ya HIV zimekuwa adimu.

Takwimu za baraza la kupambana na Ukimwi nchini Kenya,NACC zinaashiria kuwa kwa mwaka huu pekee, wanafunzi 21,404 wameambukizwa virusi vya HIV kwa mara ya kwanza. Idadi hii ni zaidi ya nusu ya maambukizi mapya yaliyorekodiwa katika kipindi cha mwaka mmoja kote nchini.

Wengi wanaoambukizwa ni wasichana na wanawake.Wasichana 5,254 na wavulana 993 walio na umri wa kati ya miaka 15-19 ndio walioambukizwa Ukimwi kwa mara ya kwanza maishani mwao.

Kundi hili ni la wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Inasadikika kuwa kilichochangia ni watoto kulazimika kusalia nyumbani tangu mwezi wa Machi pale shule zilipofungwa rasmi kuzuwia COVID 19 kusambaa. Nelson Otwoma, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa NEPHAK, shirika la watu wanaoishi na HIV nchini Kenya amesema:

“Tukisema hii miaka 15 hadi 24 wengi wao ni wasichana, sio hata wavulana. Sasa kile kitu wasichana wanaangalia sana ni kuzuia kupata mimba. Sasa hivyo vidonge vya kuzuiwa mimba huwa wanameza. Lakini za HIV zinawalemea hawa kidogo kwasababu wanaangalia mtu, anaangalia mpenzi wake anafikiri huyu yuko sawa.”

Nusu milioni ya watu walioambukizwa HIV hawatumii dawa za ARV

Kenia Schnell-HIV-Test in Nairobi

Vituo vya kupima virusi vya HIV mjini Nairobi

Jumla ya watu 41,728 wameambukizwa HIV katika kipindi hicho na kiasi ya nusu yake ni wanawake.Watoto walio na umri wa miaka 15 na zaidi na wengine ambao hawajatimiza miaka 14 ndio walionaswa na mtego wa Ukimwi. Vijana walio na umri wa miaka kati ya 20 na 29 walioko kwenye vyuo vikuu na vile vya amali nao pia hawakusazwa. Kaunti zinaoongoza kwa maambukizi ni zile za eneo la Kanda la Ziwa za Kisumu, Nairobi, Siaya, Homabay, Migori, Nakuru, Mombasa, Kisii, Kakamega na Kiambu.

Kadhalika,watu 57 wanafariki kwa ukimwi na matatizo yanayosababishwa na hali hiyo kila siku.Maafa mengi zaidi yanaripotiwa kuwa ya walio nguvu kazi ya taifa jambo linalohatarisha janga la kijamii katika siku za usoni.

Kwa upande wa pili,kiasi ya nusu milioni ya watu wazima walioambukizwa virusi vya HIV hawatumii dawa za kupambana na makali ya Ukimwi za ARV. Kilichochangia hali hii ni kuwa janga la corona limesababisha hali ya dharura kwenye vituo vya afya na juhudi zote zinaelekezwa huko. Kiasi ya 30% ya watoto walioambukizwa HIV hawajaanza kutumia dawa za kupunguza makali za ARV. Kulingana na wataalam ,wagonjwa walio na matatizo yanayoathiri mfumo wa kinga mwilini wako katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa COVID 19 kama anavyoeleza Dr Betty Okere wa mjini Nairobi.

“Kama mtu kinga ya mwili wake iko chini, ni rahisi sana apate Covid-19. Na makali ya ugonjwa huo yatakuwa zaidi ambapo atakuwa hata anaangalia kifo tofauti na mtu ambaye kinga yake ni imara.”

Ripoti ya shirika la Afya Ulimwenguni,WHO iliyochapishwa mwezi Julai mwaka huu inaeleza kuwa mataifa 73 yanakabiliana na uhaba wa dawa za kupambana na makali ya HIV kwasababu ya janga la Corona. Jumla ya watu milioni 1.5 wanaishi na virusi vya HIV.

 

 

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *