img

Mwakamo aridhishwa na matumizi ya fedha za Magufuli Soga

December 1, 2020

Na Omary Mngindo, Soga

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Michael Mwakamo, amefanya ziara ya kukagua matumizi ya shilingi milioni 68, alizochangisha Rais Dkt. John Magufuli katika Kijiji cha Soga.

Ikiwa ni ziara yake ya kwanza jimboni hapo, alijionea matumizi mazuri ya fedha hizo zilizochangishwa na Rais Magufuli alipopita kijijini hapo miezi michache iliyopita, akitokea kwenye ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR inayopita Soga.

Akiwa shuleni hapo alipokelewa na Mwalimu Mkuu Msaidizi Catherine Mganga, Mwenyekiti wa Kijiji Fadhili Lihamba aliyemwelezea Rais uwepo wa changamo katika shule hiyo, wakiwemo viongozi mbalimbali, Mwakamo alianza kukagua majengo hayo kabla ya kuzungumza na viongozi na walimu hao.

Alisema kuwa akimwakilisha Rais kisiasa na kiserikali, hana budi kufuatilia maagizo anayoyatoa ikiwemo fedha anazozichangisha au kuzipeleka katika miradi mbalimbali, ili kujiridhisha na matumizi yake ndio maana ziara yake ya kwanza akaanzia Soga.

“Mbunge wenu leo nimeamua kufanya ziara yangu ya kwanza toka niapishwe kushika wadhifa huu kuja kukagua matumizi ya fedha zilizochangishwa na Rais wetu Dkt. John Magufuli, niseme kwamba nimeridhishwa na matumizi yake, majengo yamekidhi viwango hongereni sana,” alisema Mwakamo.

Aidha aliwataka mafundi hao kuhakikisha kwamba ukarabati huo wa vyumba hivyo uendane na ukarabati wa sakafu, sanjali na madawati ya zege yaliyopo kwenye baadhi ya vyumba hivyo kuyapaka rangi ili yawe na mwonekano mzuri zaidi, pasipokusahau kuweka jipsam.

“Tunamshukuru Rais wetu wa wanyonge Dkt. John Magufuli kwa kutusaidia,  shule yetu sasa ina muonekano mzuri lakini pongeza za kipekee ziende kwa Mwenyekiti wetu Lihamba, kwa kumwelezea Rais changamoto hii, bado tuna vyumba saba vinahitaji ukarabati tutafute wadau tuvimalizie,” alisema Mwakamo.

Awali taarifa ya upokeaji wa fedha hizo za harambee hiyo pamoja na matumizi yake iliyosomwa na na Mwalimu Catherine, imeeleza kwamba kabla ya kufikia hatua ya kupaka rangi, milango, wavu katika madirisha kurekebisha sakafu na kuweka jipsmu, bado wana salio la shilingi milioni 19 benki.

Kwa upande wake Lihamba alimshukuru Rais Magufuli kwa kugushwa na changamoto ya uchakavu wa vyumba hivyo, ambayo alimwelezea alipokuwa kijijoni hapo na kwamba hivi sasa shule yao inapendeza huku akiwaomba wakazi kuendelea kujitokeza katika shughuli za kimaendeleo.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *