img

Mama wa mfungwa wa ugaidi aiangukia Serikali

December 1, 2020

Fatuma Salim, mama mzazi wa Mtanzania Rashid Charles Mberesero anayedaiwa kujinyonga katika Gereza la Kamiti nchini Kenya, ameiomba
Serikali imsaidie kuurejesha mwili wake ili uzikwe Tanzania.

Akizungumza jana kwa simu kutoka Gonja wilayani Same anakoishi, Fatuma ameiomba ofisi ya Balozi wa Tanzania nchini Kenya na ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi Tanzania (DCI), kumsaidia kufanikisha mchakato huo.

Hata hivyo, baba mzazi wa Rashid, Charles Mberesero alipotafutwa aliomba asizungumze chochote kwa kuwa ana maumivu makali.

Julai 3 mwaka 2019, Rashid na wenzake wawili walitiwa hatiani kwa kushiriki shambulio la kigaidi lililofanywa Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya mwaka 2015 ambako wanafunzi 148 walipoteza maisha.

Kutokana na kosa hilo, Rashid alihukumiwa kifungo cha maisha jela kutokana na kukutwa eneo la tukio wakati washitakiwa wengine Mohamed Ali Abikar na Hassan Edin Hassa walipewa kifungo cha miaka 41 gerezani.

Rashid alikata rufaa na majibu yalikuwa bado hayajatolewa taarifa za kujinyonga kwake zilipopatikana muda mfupi baada kupata mlo wa mwisho.

Vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti kuwa Rashid alikutwa amejinyonga kwa kutumia blanketi katika mahabusu yake iliyopo kitalu H katika Gereza la Kamiti jijini Nairobi lenye ulinzi mkali.

Taarifa zinasema mwili wake ulikutwa ukining’inia katika dirisha la grill kwa kipande cha blanketi. Inadaiwa alijinyonga Ijumaa iliyopita saa tatu usiku.

Mama mzazi alia

“Nilipokea jana hizi taarifa (juzi). Kuna kijana jirani aliniletea liniletea simu. Nikaona ile message aliyokuwa ametumiwa” alisema Fatuma.

Mama huyo alieleza kuwa jana asubuhi akasome kwenye magazeti pia. “Naiomba Serikali na balozi wa Tanzania aliyeko Kenya na Serikali yote ya Kenya na Tanzania wanisaidie kuuleta mwili wake,” alisema.

Alisema anaziomba mamlaka zimsaidie angalau kuurejesha nchini mwili wa mwanaye ili familia imzike kwa heshima nyumbani kwao tena kwa imani ya dini yao kwa sababu kipindi chote alichokuwa Kenya hakuwa na uwezo wa kwenda kumuona.

“Kwa sababu kashafariki basi Serikali inisaidie hata kumrudisha Tanzania nimzike kwa heshima ya dini,” alisema.

Wakati mwanaye anakamatwa, mama huyo alisema alikuwa na mawasiliano na ofisi ya DCI kuhusu suala hilo.

Balozi atoa utaratibu

Alipotafutwa balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk John Simbachawene hakupatikana lakini katibu wake, Annet Mmari, alimpa simu mtu aliyemtambulisha kama kaimu balozi kueleza kinachoweza kufanyika.

Ofisa huyo alimshauri mama wa marehemu kuwasilisha ombi lake kwa maandishi katika ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili lifanyiwe kazi.

“Kuna taratibu za kufuatwa kwa sababu huyo mtu amekufa akiwa anatumikia kifungo kwa hiyo mama wa marehemu tunamshauri awasiliane na wizara,” alisema.

Vilevile, alifafanua kwamba “ombi lake aliwasilishe kwenye wizara kwa maandishi kwa sababu Serikali inafanya kazi kwa karatasi. Kwa hiyo aandike barua mapema kwa wizara aombe mwili wa mtoto wake kurejeshwa Tanzania.”

Kaimu balozi huyo pia alisema ni lazima Serikali ithibitishe ni mama yake mzazi na wizara itawapelekea wao maelekezo au kwa ubalozi wa Kenya nchini Tanzania ikiomba ishughulikie suala hilo.

“Sisi kama ubalozi hatuna shida yoyote ila tunachotakamaombi yafuate utaratibu. Hatuwezi kushughulikia kitu kwa kutumia simu kutoka kwa mtu binafsi, lazima ombi lipelekwe kwenye mamlaka za Serikali,” alisisitiza.

Wakati anakamatwa nchini Kenya mwaka 2015, Rashid alikuwa na umri wa miaka (20) na alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tano katika Sekondari ya Bihawana iliyoko Dodoma inayomilikiwa na Serikali.

Rashid anadaiwa kutoroka shuleni baada ya kukatazwa kuvaa kofia na kwa miezi minne mfululizo hakuwa shuleni. Kwa kipindi chote hicho, taarifa zinasema hakuna aliyefuatilia kujua alipo huku wazazi wakiamini yupo shuleni akisoma.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *