img

Mama aeleza jinsi baba alivyombaka binti yake

December 1, 2020

Shahidi wa tano wa upande wa mashtaka katika kesi ya ubakaji inayomkabili Hamis Mhina (52), mkazi wa Mbagala Kiburugwa jijini hapa, ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Temeke alimkuta mshtakiwa na mtoto sebuleni wakiwa watupu.

Mhina anadaiwa kumbaka na kumpa ujauzito binti yake aliyekuwa anasoma kidato cha pili Sekondari Mbande mwenye umri wa miaka 15.

Shahidi huyo, Mariamu Ahmed ambaye alikuwa mke wa mshtakiwa ingawa kwa sasa ameolewa na mwanaume mwingine, alisema alimfumania mumewe na binti yao mara tatu.

“Mwanzoni mwa mwaka 2019 mtoto wa mume wangu akiwa kidato cha pili alikuja nyumbani kwangu akitokea kwa mama yake mzazi na tukawa tunaishi naye nyumbani lakini tangu alipowasili maisha ya Mhina yalibadilika sana…nikitaka unyumba alikuwa hataki akidai uume wake haufanyi kazi,” alisema Mariamu.

Mbele ya hakimu mkazi Catherine Madili huku akiongozwa na mwanasheria mwandamizi, Cecilia Mkonongo shahidi huyo alisema yeye na mume wake Mhina walikuwa wanaishi Kiburugwa Mbagala alikomfumania. Baada binti huyo kuhamia nyumbani hapo alisema alikuwa analala sebuleni wakati wao wakilala chumbani na ilipotokea mshtakiwa amesafiri alikuwa analala chumbani na binti huyo.

Tangu alipofika binti huyo, Mariamu alisema hakuwahi kukutana kinyumba na mume wake kwa kipindi cha miezi saba, mshtakiwa huyo mwenye kawaida ya kusafiri, akisema uume wake haufanyi kazi.

Siku moja aliporudi kutoka safarini, Mariamu alisema mshtakiwa alimwambia binti yake aingie chumbani ila alale chini jambo lililomshangaza na alipojaribu kuuliza, alifokewa.

Ilipofika saa sita usiku, Mariamu anasema alijifanya amesinzia fofofo ndipo alimwona mshtakiwa akichota maji na kuyapeleka chooni na baadaye alimfuata mtoto huyo na kumweleza aende akaoge.

Baada ya kuoga mtoto huyo alirudi ndani wakati huo alikuwa amevaa kanga ndipo akamuona Mhina ameingia na chetezo kwa ajili ya kufukiza lakini hakikuwa na moto kama inavyotakiwa.

“Nilikuwa naona kila kinachoendelea mshtakiwa akijua nimelala. Alipoingia ndani alimwambia mtoto avue kanga aliyokuwa amevaa na akaichukua na kuitandika chini na akachukua shuka kitandani wakajifunika pamoja,” alisema.

Wakiwa wamejifunika, Mariamu alisema binti alipiga kelele na kuita ndipo akanyanyuka na kuuliza nini kimetokea wakati alishuhudia kila kilichotokea.

“Niliamka na kumwona binti akiwa uchi huku mshtakiwa akiwa tumbo wazi na chini amevaa kipensi. Niliwafukuza chumbani wakaenda kulala sebuleni lakini asubuhi waliondoka wakarudi jioni,” alisema Mariamu.

Waliporudi, alisema alimweleza mshtakiwa kuwa mdogo wake anaolewa hivyo ataenda na binti huyo shereheni lakini Mhina alikataa akisema atabaki nyumbani.

Baadaye anasema alitafuta mwanya wa kumdadisi binti huyo lakini mshtakiwa alikuwa hampi nafasi ya kuwa naye karibu na akawa anafuata shuleni pia ili arudi naye nyumbani.

Baada ya tukio hilo, siku ya tatu baadaye, saa nane usiku, alisema mshtakiwa alitoka chumbani na kuelekea sebuleni alikolala mtoto huyo. Akiwa usingizini akasikia kelele za mtoto akilia na alipoenda sebuleni alimkuta mtoto pamoja na Mhina wakiwa uchi mshtakiwa huyo alipomwona alivaa taulo haraka huku akishika chetezo na kudai anamfukiza binti yake dawa za kienyeji.

“Huyu mzee alikuwa anamfusha dawa za kienyeji mtoto akidai anaumwa lakini kwa ufahamu wangu alikuwa haumwi. Asubuhi nikampigia mama yake mzazi na kumweleza hayo yote ili aje kumchukua nami nikaomba talaka yangu,” aliieleza mahakama.

Wakili wa utetezi, Julius Kirigiti aliiambia mahakama wanao mashahidi watatu lakini kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 3.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *