img

Serikali yatolea ufafanuzi mkanganyiko ajira za walimu

November 30, 2020

Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Siku chache baada ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI kutangaza ajira za walimu 13000 na kutokea kwa makosa mbalimbali kwenye mfumo Katibu Mkuu OR TAMISEMI  Eng. Joseph Nyamhanga ametolea ufafanuzi wa baadhi ya mapungufu yaliyoonekana katika orodha ya walimu walioajiriwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Katibu Mkuu OR TAMISEMI, Eng Nyamhanga amesema kuna baadhi ya makosa ya kimfumo yalijitokeza iliwamo jina la mwalimu Abdallah Shonde ambaye jina lake limetokea kwenye kurasa 196 amefafanua kuwa jina hilo lilitokea kimakosa wakati wa kuweka kichwa cha habari ya kurasa husika.

“jina hili lilitokea baada ya wakati ya kuweka kichwa cha habari ndipo hilo jina likatokea kimakosa kwenye mfumo lakini halijaongeza idadi wala kupunguza ajira za walimu wengine bali iliongeza namba ya wingi wa majina tu, lakini tulifanyia marekebisho siku ileile” amesema Eng. Nyamhanga.

Amesema kosa la pili la kimfumo lilikuwa ni mwalimu Benjamini Billal kupangiwa shule binafsi, amebainisha kuwa Serikali huingia makubaliano na shule binafsi na za dini za watu wenye mahitaji maalumu ya kusaidiana kwenye shule hizo zinazopokea wanafunzi wa mahitaji maalumu.

“Lakini kwa mwalimu huyu alipangiwa kimakosa kwenye shule ya Mwalimu Tuntube kigoma na tayari tumembadilisha na sasa tumempangia shule ya Malagalasi huko huko kibongo kigoma tumeona tusimpeleke mbali” amesema.

Aidha ameongeza kuwa mapungufu mengine  yalikuwa ni baadhi ya walimu ambao wanaonekena walimaliza kidato cha nne mwaka 2019, 2018 na 2017 amesema ni makosa ya waombaji wenyewe kwenye kujaza fomu kwa sababu mfumo ulikuwa hauruhusu kufanya marekebisho.

“Tumejaribu kupitia majina ya walimu hao na tumebaini walimu hao walimaliza kidato cha nne kuanzia mwaka 2013 na kidato cha sita walimaliza mwaka 2016 na hakuna mwalimu aliyeajiriwa akiwa amemaliza kidato cha nne mwaka 2019 na 2018” amesema.

Amebainisha kuwa pia hakuna mwalimu aliyeajiriwa mwenye umri wa zaidi ya miaka 45 na kubainisha anayedaiwa kuajiriwa akiwa amemaliza chuo mwaka 1994 bali uhakiki umebaini alizaliwa mwaka 1995 na alimaliza elimu ya cheti mwaka 2015.

Amesema wanaendelea kufanyia marekebisho mfumo huo ili makosa kama hayo yasiweze kujirudia tena, na wameanza kuhakiki majina upya moja moja kupata uhalali wa majina hayo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt Laurian Ndumbaro amesema makosa mengi yamejitokeza baada ya waombaji wengi kufanya makosa mengi kwenye uombaji.

Amesema ajira 13000 zinatolewa kwa awamu mbili ambapo kwa awamu ya kwanza wameajiri walimu 8000 na awamu ya pili wataajiri walimu 5000 kwa mwaka huu wa fedha 2020 hadi 2021, huku akitoa onyo kwa walimu waliogushi masomo ambayo hawakusomea kwa lengo la kupata kipaumbele watakaobainika wataondolewa kwenye mfumo moja kwa moja.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo amesema kuna walimu walifanya udanganyifu ambapo kwa walimu wa Sekondari wanatakiwa kuomba masomo mawili tu waliyosomea lakini kuna baadhi ya walimu walijaza masomo matatu katika maombi yao.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *