img

Mfahamu Elpidix Gosbert kijana aliyezaliwa na uwezo wa kula chupa, wembe

November 30, 2020

Imezoeleka kuona mambo kama haya kwenye michezo ya viini macho maarufu kama ‘mazingaombwe’ lakini hii ni tofauti kwa kijana anayefahamika kwa jina la Elpidix Gosbert (20) kutoka wilayani Ilemela Mkoani Mwanza ambaye anasema amezaliwa na uwezo wa kula wembe na chupa.

Elpidix ambaye ni mshiriki mara mbili wa Shindano la kusaka vipaji la Bongo Star Search (BSS, 2019 na 2020) amekulia katika kijiji cha Kanyamukula, kata ya Kamachumu, wilayani Mreba mkoani Kagera ambapo anaeleza kujikuta na uwezo wa kutafuna na kumeza Chupa pamoja na nyembe kama chakula kingine.

Anasema amelelewa na Shangazi yake na alipokuwa mdogo, wakati akisoma darasa la tano shule ya Msingi, alianza kujifunza kuimba ili kufikia ndoto ya kuwa muimbaji mkubwa nchini.

Elpidix, Mwenye ndoto ya uimbaji alianza kushiriki mashindano tofauti shuleni hapo huku ikiwa ni dhamira yake kutokushindwa ambapo alifanyia mazoezi vitu mbalimbali vya tofauti kama kuchomwa mwili moto, kutafuna chupa na wembe na kuvimeza huku lengo lake kubwa likiwa ni kupata kutoshindwa kwenye mashindano ya vipaji ili kufikia adhima ya kupata umaarufu.

Anasema aliendeleza michezo hiyo ambapo baada ya taarifa kuwafikia wazazi nyumbani walimupiga marufuku kufanya vitu hivyo kwa tahadhari ya kutoathirika kiafya lakini aliendeleza kwa kujificha ficha.

FAMILIA INAMCHUKULIAJE?

Elpidix ambaye ni mtoto wa pekee kwa baba na yake anasema baada ya kuonekana tabia yake ya kula chupa na nyembe hawezi kuiacha familia na marafiki wa karibu walianza kumutenga na kumuona kama mtu wa ajabu, kiasi cha kufananishwa na washirikiana.

Anasema ilifikia hatua Shangazi yake alianza kuuza mali walizoachiwa na baba Elpidix ili apate hela ya kwenda kwa waganga wa kienyeji kwa madai kuwa ameachiwa mtoto wa ajabu na hawezi kuishi naye hivyo alihitaji msaada ili aweze kusitisha tabia ya kijana huyo kula chupa na wembe.

Anasema ameshawaruhusu familia kufanya lolote kama wanahisi ni mshirikina lakini yeye anaamini hiyo ni moja ya sanaa tu ambapo kama kuna mtu hamuamini basi anaweza kumufuata muda wowote na na kitu pekee ili kujionea na anachohitaji yeye ni nyembe na chupa tu.

Elipidix anasema, mfano alipokuwa ndiyo anaanza kula chupa na wembe alishawahi kupelekwa kwa waganga wa kienyeji kama mara nne  na watu wake wa karibu kwenye familia ambapo waganga walisisitiza kuwa ni mtu wa kawaida.

Anasema ili kudhihirisha kwamba hatumii dawa na uwezo wake ni wa asili amekuwa ni muumini mzuri wa kanisa katoliki na amebatizwa ndani ya kanisa hilo na huhudhuria ibaada za makanisa mengine ya kiroho ambapo alishawahi kwenda kwa mzee wa upako Dar es Salaam ambapo ulipofika dua za kuombea mapepo alisikiliza ilia aone kama anayo yataondoka lakini cha ajabu hakikutokea chochote.

CHANGAMOTO ALIZOKUTANA NAZO

Anasema katika harakati za maisha aliwahi kwenda kuishi Dar es Salaam na dada mmoja ambaye alimusaidia, wakati anaishi huko alikutana na majaribu mengi ya kishirikina lakini hakuwahi kupata tatizo lolote ambapo kuna siku dada mwenye nyumba alikuta asubuhi kuna damu ndani ya nyumba akaamua kumufukuza kwa kuhisi kijana huyo ndiyo mshirikina.

Anasema alishawahi kushiriki mashindano na vijana wengine zaidi ya 30 wanaokula wembe na chupa kwa kutumia dawa lakini yeye aliibuka mshindi kwa sababu alifahamu michezo yao na hakutaka kuingia kwenye michezo hiyo ya kishirikina.

Elipidix anasema changamoto kubwa aliyowahi kukutana nayo maishani mwake ni pale ambapo  siku moja alikuwa klabu alipoonekana anawaonyesha watu waliobishana juu ya uwezo wake akataka kupigwa kwa kumuhofia alikuwa ni mwizi.

Kuhusu mahusiano ya kimapenzi Elipidix anasema kuna wakati anapitia changamoto kupata mwenza kwa wale mabinti wanaomfahamu kwa kudhani yeye ni mshirikina.

Anasema aliwahi kumtongoza binti mmoja kujaribu kumushawishi awe mpenzi wake lakini binti huyo kwa kujua tu mimi nina uwezo wa kula chupa na nyembe alikataa na kuniambia hataki kuwa na mimi kwa sababu nitamutoa kafara.

USHIRIKI MASHINDANO YA BSS

Elipidix anasema alianza kushiriki mashindano ya BSS mwaka 2019 lakini aliingia kama muimbaji tu hakuonyesha uwezo wake mwingine alionao na hakufanikiwa kupata nafasi.

Anasema mwaka huu 2020 pamoja na kuimba pia aliamua kuonyesha uwezo wake wa kula chupa na nyembe kwa majaji na wengi walishitushwa na uwezo huo na hadi sasa ni kama imemufungulia milango kwa sababu anapokea simu kutoka mikoa tofauti wakihitaji kufanya naye kazi kwenye matamasha.

MATARAJIO NI YAPI.

Anasema yeye suala la kula chupa na nyembe haoni kama kitu kikubwa sana lakini anapambania mziki ndiyo anaamini kipaji kitakachomupa maisha ingawa ataendelea pia kuonyesha kipaji chake cha kula wembe na chupa kama kitu chake cha ziada alichonacho.

Anasema kwa yeyote aliye tayari kufanya naye kazi na kuendeleza vipaji hivyo viwili basi yupo tayari, kwani bado hana meneja maalumu hivyo atahakikisha anajituma na kutendea haki matakwa ya mashabiki wake ambapo kwa mtu yeyote atakayekuwa na nia ya kufanya naye kazi basi amtafute kupitia simu namba 0689-838-268

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *