img

Majaliwa apiga marufuku tozo ya unyaufu kwenye korosho

November 30, 2020

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza waendesha maghala kuacha kutoza tozo ya upungufu wa uzito wa korosho ghafi zilizohifadhiwa ghalani (unyaufu) kwa wakulima na wanunuzi kwa kuwa tozo hiyo imeshaondolewa.

Majaliwa alitoa agizo katika kikao kati yake na wakuu wa mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma, makatibu wakuu wa Ofisi ya Rais-Tamisem, Kilimo, Viwanda na Biashara pamoja Mrajisi wa Ushirika.

Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maghala na Waendesha Maghala wote wa mikoa hiyo.

“Mimi niliwaita kuwaambia kuwa wasimamizi wa maghala hampaswi kukata tozo ya unyaufu iwe ni kwa wakulima au wanunuzi kwa sababu tozo hii haina uhalisia na haijathibitishwa na vyombo husika, hakuna unyaufu unaotokea katika kipindi kifupi cha kuhifadhi korosho, hayo yote ni mawazo yenu tu.

“Hizi korosho wala hazikai miezi mitatu kama ilivyoelekezwa kwenye kanuni hii, korosho zinakusanywa, mwezi wa 10, mnada nao unaanza mwezi wa kumi uleule na baada ya hapo kuna minada ya kila wiki, minada ipo mingi, unyaufu mnaoukata unatokana na nini?” alihoji Waziri Mkuu.

Sambamba na hilo Waziri Mkuu ametoa siku tano kwa waendesha maghala kuandaa taarifa kuhusu ni kiasi gani cha korosho ambazo wamechukua kutoka kwa wanunuzi kama tozo ya unyaufu, hivyo atatuma timu maalum kwa ajili ya kazi hiyo.

“Na ninyi waendesha maghala naleta timu huko kuja kupita kila ghala kuona msimu huu wote mmechukua korosho za unyaufu kiasi gani, kwa hiyo nawapa siku tano kila mmoja akaandae taarifa ya korosho zilizochukuliwa kutokana na unyaufu katika ghala lake, kwa maghala yaliyopo mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma kuona nani amechukua unyaufu na kwa kiasi gani,”alisema Majaliwa.

Kufuatia hali hiyo, Majaliwa alimuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara kumuondoa katika nafasi yake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maghala Odilo Majengo kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya Serikali kuhusu kusitisha tozo ya unyaufu katika zao la korosho.

“Mkurugenzi wa Bodi ya Maghala ulidharau maagizo ya Serikali na hatuwezi kuishi hivyo katika Serikali, tulikwambia uache lakini ukaendesha zoezi hili kwa sirisiri na unasema hayo ni matamko ya kisiasa, kwa nini tubaki na wewe kwenye nafasi hii?” aliuliza Majaliwa.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *