img

Athari za kuwafukuza wanachama 19 wa Chadema

November 30, 2020

  • Rashid Abdallah
  • Mchambuzi, Tanzania

Dakika 11 zilizopita

Mbunge na aliyekuwa Kiongozi wa Chadema tawi la wanawake, BAWACHA

Baada ya uchaguzi wa Oktoba 2020 kuisha, vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania vimejikuta katika njia panda ya kisiasa, si upande wa Tanzania Bara pekee, hadi Zanzibar.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kulikuwa na kitendawili cha ikiwa wapeleke majina ya Wabunge wa viti maalum ama la. Kitendawili hiki kilikuwa na jawabu tofauti kutoka kwa wafuasi wa chama hicho na wachambuzi wa siasa.

Mambo yaligeuka baada ya kundi la Wabunge 19 wanawake kutoka Chadema kufanya uamuzi wenye utata wa kwenda Bungeni na kuapishwa na Spika Job Ndugai, kuwa wabunge wa Bunge la 12.

Siutofahamu sasa imekuwa kati ya uongozi wa juu wa chama hicho wakiungwa mkono na sehemu kubwa ya wafuasi wa chama dhidi ya wabunge 19. Bado mambo yako moto.

Upande wa Zanzibar, chama kikuu cha upinzani ACT Wazalendo nacho kiko katika njia panda ya kisiasa. Bado wamejifungia wanajadili ikiwa waingie katika serikali ya Umoja wa Kitaifa au la.

Mjadala huo una maoni tofauti. Na uamuzi wowote watakaouchukua, utaleta maoni kinzani vilevile kutoka kwa wafuasi wao na wafuatiliaji wa siasa. Hilo ni la kusubiri na kuona.

Siri iliyo wazi, wapinzani wamewekwa katika kona Bara na Visiwani.

Maswali mengi majibu machache

Tukirudi kwa Chadema. Namna uchaguzi ulivyokwenda, malalamiko ya wizi wa kura na kura feki, kwa wengi wanaamini chama chao kinapaswa kukaa nje ya Bunge na serikali kwa ujumla.

Faida kubwa ya kisiasa kwa uamuzi wa aina hiyo ni kuibakisha heshima ya chama kwa wafuasi wake. Ila kwa upande mwingine watapoteza nafasi ya kuwa katika Bunge, kisiasa hiyo haitwi faida.

Wengine wanaona upinzani kushiriki katika Bunge ni kuhalalisha kile wanachoamini ni ubakwaji wa demokrasia katika uchaguzi uliopita. Je, kutoshiriki ama kuwa nje kutawapa uhakika wa kuchochea mageuzi katika taasisi zinazosimamia uchaguzi kwa faida ya uchaguzi wa 2025?

Wanachama wa Chadema

Pia kuna swali dume; Wabunge 19 kuwapeleka Bungeni kungesaidia kubadilisha lolote mbele ya Wabunge wengi wa CCM? Je, katika uwanja wa siasa ni sahihi kuhitimisha kuwa uwepo wao Bungeni hautokuwa na manufaa yoyote kwa upinzani?

Kimsingi kadhia hii ina maswali mengi yasiyo na majawabu ya uhakika. Wala hakuna uamuzi sahihi moja kwa moja, kila uamuzi una athari yake kisasa. Ni mtanange ambao umekaa vibaya kwa upinzani kwa kila sura.

Upinzani unahitaji kuwa na maamuzi ya kupunguza athari hasi za kisiasa ambazo wanaweza kuzipata. Kwa sasa athari haziepukiki tena, lakini zinaweza kupunguzwa makali kwa maamuzi ya busara.

Ni ipi hatari ya kuwafukuza wanachama 19?

Katika kikao cha Novemba 27, Kamati kuu ya Chadema ilikubaliana kwa kauli moja kuwavua uanachama wanachama wao 19 walioapishwa Bungeni.

Kuwafukuza wanasiasa ambao daima walikuwa na nguvu katika chama, ni namna ya kuonesha kwamba chama hakivumilii wale wanaohesabiwa kuwa wasaliti.

Upinzani hautokufa kwa kuondoshwa hao. Utaendelea kubaki ukiwa dhaifu katika ngome ya wanawake. Kutakuwa na kazi mpya na kubwa ya kujenga ngome nyingine ya akina mama.

Ikiwa wanachama hao wataridhia uamuzi wa kufukuzwa. Upande pekee utakaonufaika na hilo ni chama tawala; ngome ya wanawake iliyokuwa ikiwasumbua hatimae imedondoshwa.

Katika sekeseke hili chama pekee chenye ulazima wa kuwa na uangalifu mkubwa kuhusu uamuzi upi ni bora kufanya ni Chadema.

Kwanini chama tawala kinasimama na wabunge wa upinzani?

Sheria ndiyo inalazimisha Wabunge wa kuteuliwa kutoka upinzani baada ya uchaguzi kuisha. Ingawa dalili zinaonesha viongozi wa chama tawala wanataka wabunge hao wawepo katika Bunge.

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Bashiru Ali, na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Chama hicho, Humphrey Polepole, kwa nyakati tofauti wametoa kauli zinazoashiria kuwaunga mkono wanasiasa hao 19. Nini sababu?

Bunge la Tanzania

Wiki chache zimepita tangu Tanzania ijadiliwe kuhusu uwezekano wa kuwekewa vikwazo katika Bunge la Ulaya, ikishutumiwa mambo mengi ikiwemo kuminya demokrasia na kukandamiza upinzani.

Takwa la chama tawala kuona Bunge lenye upinzani, ni katika mbinu ya kuzisafisha au kurekebisha siasa za nchi hii ambayo inaoneshewa vidole. Bunge bila upinzani litazidisha zile kauli kwamba upinzani unakandamizwa, na kuhatarisha Tanzania kuwekewa vikwazo.

Kwa upande mwingine wa kisiasa, chama tawala kinasimama na wabunge 19 kwa maslahi ya kisiasa. Upinzani unapoingia katika mgogoro huishia kuwa dhaifu.

Hivi ni kama vita vya panzi, mnufaika mkubwa atakuwa kunguru ambaye katika sakata hili ni chama tawala. Mvurugano wa chadema ni nafuu kwa CCM.

Chama tawala kina maslahi katika jicho la kitaifa na kimataifa kusimama na wabunge 19.

Ni upi mzizi wa migogoro ya sasa ya kisiasa?

Mzizi wa tatizo sio upinzani kushindwa kuendesha siasa zao vizuri. Tatizo linaanzia pale nchi inapokuwa na vyombo vyenye walakini katika kusimamia uchaguzi.

Inaonekana haki haitendeki kama inavyotegemewa. Chaguzi zinakuwa na mashaka mengi. Na hapo ndipo tatizo linapoanza. Haya yanayotokea sasa ni matokeo tu ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiri zaidi vyama vya upinzani.

Kuna mambo mengi yenye kuashiria uchaguzi uliopita ulikuwa na kasoro nyingi. Uchaguzi unapokumbwa na kasoro, kuna uhakika gani waliotangazwa kushinda ndio walioshinda kweli?

Ikiwa uchaguzi bila ya video za kura feki unawezekana, bila kushikana mashati kwa kuwatoa wasimamizi wa uchaguzi, bila kunyoosheana vidole juu ya masanduku yaliyojazwa kura kabla uchaguzi. Bila ya majeruhi na tuhuma za mauaji. Pengine ingesaidia pia kutokuwepo migogoro ya namna hii baada ya uchaguzi.

Utawala bora ni msingi wa ujenzi wa demokrasia imara. Utawala bora maanake ni kuwajibika kwa uadilifu zile taasisi za kiuongozi. Ikiwa ni Tume ya Uchaguzi au Jeshi la Polisi, ni kutekeleza majukumu yao bila upendeleo wala ukandamizaji.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *