img

Mzozo wa Tigray Ethiopia: Waziri Mkuu Abiy anadai jashi limetwaa kikamilifu eneo la Tigray

November 29, 2020

Dakika 4 zilizopita

Ethiopian soldiers

Maelezo ya picha,

Mamia wameuawa huku maelfu wakilazimika kuhama makazi yao

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anasema vikosi vya serikali sasa hivi vimechukua “udhibiti kamili” wa eneo la kaskazini la Tigray.

Mapema, wanajeshi waliingia mji wa Mekelle na kuendeleza mashambulizi dhidi ya chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF).

Kiongozi wa TPLF ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa nalo litaendelea “kulinda haki yake” na “kupigana na wavamizi hawa hadi mwisho”.

Mamia ya raia wameuawa huku maelfu walilazimika kuhama makazi yao kwasababu ya vita.

Mapigano haya yalianza mapema mwezi huu baada ya Bwana Abiy kutangaza oparesheni dhidi ya TPLF, chama cha eneo, kwa kukishutumu kushambulia makao makuu ya jeshi la Ethiopia eneo la Mekelle la kaskazini.

Wakati huohuo, ubalozi wa Marekani katika nchi jirani ya Eritrea umesema milipuko sita imesikika katika mji mkuu wa Asmara Jumamosi jioni.

Awali, vikosi vya Tigray vilirusha makombora upande wa Eritrea ambayo wanaishutumu kwa kuunga mkono serikali ya Ethiopia katika wiki kadhaa za mapigano.

Bado haijafahamika ikiwa matukio ya hivi karibuni huko Asmara yanauhusiano wowote na mapigano yanayoendelea Tigray.

Serikali inasema nini?

Katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa Twitter, Bwana Abiy alisema jeshi linadhibiti kiukamilifu mji wa Mekelle na kwamba hatua hii “inaadhimisha mwanzo wa oparesheni ya kijeshi ya awamu ya mwisho”.

“Ninafuraha kuwafahamisha kuwa tumekamilisha pia tumesitisha oparesheni ya kijeshi eneo laTigray,” alisema.

Jeshi hilo lilikuwa limeachilia huru maelfu ya wanajeshi waliokuwa wamekamatwa na TPLF na sasa linadhibiti uwanja wa ndege na ofisi za eneo, Bwana Abiy alisema, akiongeza kuwa oparesheni hiyo imetekelezwa na “kuzingatia maslahi ya raia”.

Kumekuwa na hofu ya kitakachotokea kwa raia 500,000 wanaoishi mji huo.

Taarifa ya Bwana Abiy imesema kuwa vikosi vya serikali “vitaendelea na jukumu lake la kuwakamata wahalifu wa TPLF na kuhakikisha wanakabiliwa na mkono wa sheria”.

Taarifa za mapigano hayo ni vigumu sana kuzithibitisha kwasababu simu zote, ama za mkononi au za mezani, na mawasiliano ya mtandao katika eneo la Tigray yamekatizwa.

Map of Tigray region
Presentational white space

Je TPLF imejibu vipi?

Katika ujumbe mfupi uliotumwa kwenye shirika la habari la Reuters, kiongozi wa TPLF Debretsion Gebremichael hakusema moja kwa moja kuhusu hali halisi ilivyo sasa hivi lakini alisema kuwa vikosi vya serikali: “Unyama wao unaweza tu kupigilia msumari uamuzi wetu wa kupigana na wavamizi hawa hadi mwisho.”

Aliongeza: “Hii inahusu kulinda haki yetu ya kujitetea.”

Bado haijulikani mahali alipo Bwana Gebremichael.

Taarifa ya awali iliyotolewa na TPLF, na kuripotiwa na Shirika la habari la AFP, ilisihi “jamii ya kimataifa kushutumu mashambulizi ya silaha na ndege za kivita na mauaji ya halaiki yanayoendelea”.

Pia iliishutumu serikali ya Eritrea kwa kujihusisha na mashambulizi yanayotekelezwa katika mji wa Mekelle.

Wachambuzi wanasema TPLF huenda sasa hivi linajitayarisha kurejea milimani na kuanzisha vita vya msituni dhidi ya vikosi vya serikali.

Wasiwasi juu ya usaidizi wa kibinadamu ni upi?

Umoja wa Mataifa ilikuwa imeonya uwezekano wa kutekelezwa kwa uhalifu wa kivita ikiwa jeshi la Ethiopia litashambulia mji wa Mekelle.

Pia imeonesha wasiwasi wake kuhusu kushindwa kwa wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu kufikia eneo hilo.

Serikali ya Ethiopia Alhamisi ilisema kuwa “njia inayotumiwa kutoa misaada ya kibinadamu” inayosimamiwa na serikali itafunguliwa, na kuongeza kuwa “imejitolea kushirikiana na mashirika la Umoja wa Mataifa … kulinda raia na wale wote wenye uhitaji”.

Vilevile, Alhamisi vikosi vya Ethiopia vilipekwa katika mpaka ya Tigray na Sudan, na kuzuia raia wanaotoroka vita nchini humo, kulingana na wakimbizi.

Mwanahabari wa BBC Anne Soy ambaye yuko upande wa mpaka wa Sudan, anasema ameshuhudia makumi ya wanajeshi wa Ethiopia ambako kumesababisha kupungua kwa idadi ya wanaovuka mpaka na kuingia Sudan.

Katika mkutano Ijumaa, Bwana Abiy aliwaambia wajumbe wa Amani wa Afrika kuwa raia watalindwa.

Hata hivyo hakukuwa na ishara zozote zilizoashiria kufanyika kwa mazungumzo ya amani na wajumbe hawakuruhusiwa kutembelea eneo la Tigray.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *