img

Lucy Lameck: Mwanaharakati wa Tanzania ambaye barabara ya Ujerumani kupewa jina lake

November 29, 2020

  • Uchambuzi na Rashid Abdallah
  • BBC Swahili

Dakika 7 zilizopita

Barabara hiyo ya Wissmannstraße inatarajiwa kubadilishw ajina mwaka ujao

Maelezo ya picha,

Barabara hiyo ya Wissmannstraße inatarajiwa kubadilishw ajina mwaka ujao

Historia ya Tanganyika ambayo ni Tanzania ya sasa haikamiliki bila ya kutaja majina ya wanawake waliosimama katika mapambano ya uhuru. Kisha wakaendelea kuwika katika siasa za baada ya uhuru, moja ya majina hayo ni Lucy Selina Lameck Somi.

Lucy Lameck anakumbukwa kama mwanamke aliyetoa mchango mkubwa katika harakati za kupigania Uhuru wa Tanganyika, akiungana na mwanamke mwingine maarufu Bibi Titi Mohamed.

Bi Lucy alikuwa ni mwanasiasa na mwanaharakati. Alipinga ukoloni wa Uingereza, alipinga ubaguzi na alikuwa mtetezi mkubwa wa wanawake.

Ushujaa huo umelifanya taifa la Ujerumani kubadili jina la mtaa wa Wissmann na kupewa jina la Mtanzania huyo.

Katika siasa za Tanganyika kabla na baada ya uhuru 1961, jina la Lucy Lameck liliingia katika kundi la wanasiasa maarufu kama Oscar Kambona, Lawi Sijaona, Nsilo Swai, Tewa na wengine walikuwa katika baraza la kwanza la mawaziri la Tanganyika na baadaye Tanzania.

Akiwa mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Wanawake-UWT, alijiamini kiasia cha kukabiliana na wanasiasa wanaume katika kile kinachojulikana kama ‘mfumo dume’ wa wakati huo.

Bendera ya Tanzania

Harakati zake katika TANU

Tanganyika African National Union (TANU) kilikuwa chama kilichotawala Tanganyika na Tanzania hadi muungano wa chama hiki na Chama cha Afro-Shirazi cha Zanzibar na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977.

TANU chini ya waasisi wake wa wakati huo kiliendesha harakati za kudai uhuru wa taifa la Tanganyika dhidi ya Ukoloni wa Uingereza. Harakati hizo ndizo zilizoliibua jina la Lucy Lameck.

Baada ya kumaliza mafunzo ya uuguzi 1950, Lucy alikataa kufanya kazi katika mfumo wa matibabu wa kikoloni wa Uingereza na kuchagua kufanya kazi ya ukarani.

Katika kitabu cha ‘Nyerere and Africa: End of an Era’, mwandishi Godfrey Mwakikagile anaeleza, “tawi la TANU Moshi lilipofanya mkutano wake wa kwanza, mmoja wa wahudhuriaji alikuwa ni mwanamke kijana aliyeitwa Lucy Lameck”.

Akitokea katika familia ya wakulima kwao Moshi, akiwa bado kijana hakuachwa tena nyuma katika mapambano ya kudai uhuru.

Nimemuuliza mwanahistoria nguli wa Tanzania, Mohammed Said; ni vipi alikuwa na umuhimu mkubwa katika harakati za TANU?

“Lucy alikuwa mwanamke msomi ndani ya TANU. Kwa kushirikiana na wanawake wengine Halima Selengia, Amina Kinabo, Mama Bint Maalim waliifanya TANU kuwa na nguvu Moshi”.

Mohammed anaendelea, “katika matawi yote ya TANU Tanganyika, hakuna tawi lililopata nguvu kutoka kwa wanawake kama tawi la Moshi Mjini. Akina Mama hao walileta ngoma ya Msanja ambayo ilichangamsha chama”.

Baadae Lucy kwa ufadhili alisoma katika Chuo cha Ruskin, huko Oxford, Uingereza na chuo kingine huko Michigan, Marekani kabla ya kurudi Tanzania na kuingia katika siasa moja kwa moja.

Bi Lucy alikuwa mpinzani wa wazi wazi wa ukoloni. Katika mahojiano yaliyochapishwa Febuari 1960 na jarida la Jet la nchini Marekani, aliulaumu ukoloni kwa umasikini uliokuwepo Tanganyika.

Katika mahojiano Lucy alieleza juu ya ukoloni wa Uingereza kuwa, “utaondoshwa na kurudishwa England hivi punde”.

Siasa baada ya uhuru

Mwaka 1960 aliingia mara ya kwanza katika Bunge la Tanganyika baada ya kuteuliwa na Waziri Mkuu wa wakati huo Julius Nyerere kuwa Mbunge, kabla ya kuchaguliwa na wananchi katika Bunge la Kitaifa la Tanzania mwaka 1965.

Mwaka 1962 aliandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa Waziri, akishika nafasi ya waziri mdogo wa Shirika na Maendeleo ya Jamii 1965 hadi 1970. Kisha aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya kati ya 1967 na 1972.

Mwanasiasa Mkongwe nchini Tanzania, Pius Msekwa, anamkumbuka Lucy akiwa Bungeni, “alikuwa ni mwanamke mwenye ujasiri na uthubutu kwa sababu wakati ule haukuwa mwepesi kwa mwanamke”.

Mtetezi wa wanawake

Alipiga vita mila na desturi zilizokinza kufikiwa usawa wa kijinsia. Alipigania hali bora ya wanawake katika maisha mara baada ya uhuru.

Kwa kushirikiana na wanawake wengine Bungeni walitaka kupitishwa sheria dhidi ya wanaume wanaowapa mimba watoto wa kike, walipe faini, wafungwe ama watunze watoto.

Inaelezwa kuwa Bi Lucy alilaani kitendo cha kuwafukuza shule watoto wa kike waliopata mimba.

Kwa kushirikiana na wanawake wengine Lucy Lameck alileta vitenge kama vazi la taifa kwa wanawake wa Tanzania.

Uamuzi wa kubadili jina unatokana na nini?

Kwa mujibu wa maoni ya mwaandishi habari mkongwe na mchambuzi Mohammed AbdulRahman anaeishi Ujerumani kwa muda mrefu ni kwamba; “uamuzi huo una lengo la kufuta historia mbaya ya Utawala wa Ujerumani katika Tanganyika”.

Anafafanua; “katika kile kilichokuwa kikijulikana kama Deutsch OstAfrika (Afrika Mashariki ya Ujerumani) iliyozikusanya Tanganyika, Rwanda na Burundi 1885 hadi 1918. Hermann von Wissmann alishutumiwa kwa mauaji ya raia akiwa gavana wa Ujerumani katika eneo hilo”.

Wissmann ndiye aliongoza vita dhidi ya Abushiri ibn Salim al-Harthi, aliyekuwa kiongozi wa upinzani wa ukoloni wa Wajerumani katika maeneo ya Pangani na pwani ya Tanzania ya leo mnamo 1889.

Mwanahistoria Mohammed Said anaeleza, “Hermann von Wissmann alifanya mauwaji makubwa. Ndiye aliyemkamata na kumyonga Abushiri kisha akaendesha vita sehemu nyengine katika Tanganyika”.

Historia inaonesha ukoloni wa Ujerumani una msururu mrefu wa tuhuma za kufanya mauaji na maovu dhidi ya binaadamu hata nje ya iliokuwa Tanganyika. Pia, Afrika Kusini Magharibi inayojulikana leo kuwa Namibia, maelfu ya watu wa kabila la Herero waliuwawa.

Kwa miaka kadhaa sasa Namibia imekataa malipo ya fidia hadi kwanza Ujerumani itambuwe mauaji yale kuwa ya Kimbari, jambo ambalo mkoloni huyo wa zamani amekataa kulikubali.

Wachambuzi wanaashiria kwamba hatua hii ya kuupa jina la Lucy Lameck mtaa huo katika jiji la Berlin, kwa upande mwengine itakuwa na manufaa zaidi kwa Tanzania katika suala la kuvutia watalii wengi zaidi.

Tukio hili linalohusiana na Lucy litaweza kuwakumbusha wahusika juu ya haja ya kuwapa heshima inayostahiki mashujaa sio tu wa kisiasa lakini pia katika harakati nyengine za kijamii, ambao wengi wamesahauliwa.

Mwendazake Lucy Selina Lameck Somi alizaliwa mwaka 1934 na kuaga dunia Machi 1993.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *