img

Anza kufuga kuku watano (5) upate zaidi ya kuku mia moja (100) ndani ya wiki saba

November 29, 2020

Hebu anza na kuku Watano (5) tu Majike  wenye Rika/Umri mmoja (au wanaokaribiana). Watunze vizuri kwa kuwapatia chakula kilicho  na mchanganyiko kamili wa viini lishe
vinavyotakiwa katika mwili wa kuku, yaani; wanga, protini, calcium, chumvichumvi, madini joto nk. Wawekee na Jogoo mmoja mzuri wa kienyeji/ kizungu/chotara (kama nilivyoeleza hapa chini juu ya uchaguzi wa majogoo).

Wanapoanza kutaga watayarishie mahali pazuri/Kiota kizuri cha kutagia na kuatamia kwa kuwajengea viota ndani ya banda.

Hakikisha mahali hapo hapavuji wala hapapati unyevunyevu wala joto kali sana. Hakikisha mahali hapo pana usalama wa kutosha (mahali wanyama hatari kama vicheche, pakashume, nyoka nk hawawezi kufika).

Kuku wakiendelea kutaga na sasa ukaona wanakaribia kuatamia, Anza kuchagua aina ya mayai unayotaka kuku wako walalie. Hii inamaanisha kuwa; ukichagua mayai makubwamakubwa hayo yanakuwa na vifaranga majogoo na mayai madogomadogo mara nyingi huwa ni ya vifaranga majike.

Acha kuwawekea mayai ya mviringo kama mpira! Hakikisha kuku wote wanasubiriana ili walalie/ waatamie kwa pamoja. Weka mayai 12 hadi 15 kwa kila kiota cha kuku 1 kulingana na umbo la kuku wako.

Kuku anaweza kutaga hadi mayai 30 kwa kila msimu wa kutaga unapofika. Unaweza kutumia mayai machache kati ya 30 kwa kumuatamishia kuku wako huku mayai mengine yakisubiri awamu ya pili ya kuatamiwa.Kwa mfano ukiwawekea kuku wako hao watano, Kuku 5 x Mayai 12 =Mayai 60.

Kwa kawaida kuku huatamia/hulalia mayai kwa siku 19 hadi 21/24 tu hadi anapototoa vifaranga. Hakikisha unawawekea kuku walioatamia chakula chenye viini lishe vya kutosha na maji mengi karibu na viota vyao ili wakitoka kwenye viota vyao wale chakula mara moja na kunywa maji kisha warudi haraka kwenye mayai yao. Hii itasaidia kuangua mayai yote 12/15 bila kuharibu yai hata moja.

Au hata yakiharibika basi hayataharibika mengi kama ukiacha kuwawekea chakula waende kufukuzana na panzi na vyakula majalalani huko nje na kuchelewa kurudi kwenye mayai yao.

Wakati ukisubiria siku hizo 21/24 anza kujenga kibanda kidogo ndani ya banda kubwa ulilojenga awali au jikoni au andaa boksi kubwa na gumu kwaajili ya kutunzia vifaranga watakaoanguliwa ndani ya siku 21/24 zijazo.

Baada ya kuku hao 5 kuangua vifaranga wako 60 hapo ndipo kazi kubwa ya kulea vifaranga inapoanza. Elewa kuwa ili upate mafanikio haraka hakikisha kuwa kazi ya kulea vifaranga inakuwa yako na siyo ya kuku! Kwanza, Unatakiwa kuondoa na kuchoma moto/kufukia mabaki yote ya mayai na kuboresha usafi wa banda lote ili kuepusha magonjwa kama vile kuharisha, viroboto, papasi nk.

Hapo unaweza kuwatoa vifaranga wako wote 60 mmojammoja kadri wanavyoanguliwa hadi kufikia kifaranga wa mwisho, yaani Yule wa 60 na kuwaweka katika kibanda kidogo/boksi ulichokijenga na kuwawekea mayai mengine mama zao (yale 15/18 kati ya 30 uliyoyabakiza) ili waatamie tena kwa siku 21 hadi 24 zingine.

Unapotoa kifaranga kutoka kwa kuku aliyeatamia humfanya kuku yule ashindwe kutoka kwenye mayai maana hana mtoto wa kulea.

Akimaliza kuangua mayai yote na ukamuwekea mengine ni rahisi kwake kuendelea kuatamia maana atasubiri kupata vifaranga na ndipo atajikuta amelalia kwa siku 21 zingine bila wasiwasi.

Kwa kufanya hivyo utakuwa tayari umejipatia vifaranga/kuku zaidi ya 100 ndani ya wiki 7 tu! Sasa Unatakiwa kuwajali sana kuku hawa wanaolalia kwa mara ya pili kwa kuwapa chakula cha kutosha, maji, majani ya makongwe, mchicha, mchunga nk ili wapate vitamini na madini mengine muhimu kwa afya zao.

Fanya hivyo hata watakapokuwa wametotoa na ukawanyang’anya vifaranga. Hii itawasaidia ili wasinyonyoke sana manyoya maana kuku wengi hunyonyoka manyoya wanapoatamia. Kwa kufanya hivi, kuku wako watakaa kwa wiki 2 hadi 3 bila vifaranga na kisha wataanza kutaga tena na kuatamia kama mwanzo.
,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *