img

Mzozo wa Tigray Ethiopia: Mji mkuu wa Tigray ‘unakabiliwa na mashambulio makali’

November 28, 2020

 

Mji mkuu wa jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia unakabiliwa na mashambulio makali ya kutoka kwa vikosi vya serikali, wafanyakazi wa misaada na maafisa wa eneo hilo wanasema.

Eneo la kati kati ya mji wa Mekelle linashambuliwa kwa “makombora,” chama tawala katika jimbo la Tigray kinasema.

Jeshi la Ethiopia limekuwa likikabiliana na wapiganaji wa Tigray People’s Liberation Front (TPLF) kwa wiki kadhaa sasa.

Linasema kuwa linatarajia kuchukua udhibiti wa mji huo kutoka mikononi mwa TPLF katika kipindi cha siku chache zijazo , lakini litajizuia kuwadhuru karibu raia 500,000 wanaoishi katika mji huo.

Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa, na maelfu ya wengine kutoroka makwao baada ya jeshi la Ethiopia kuteka miji yao.

Awali majeshi ya Ethiopian yalisema kuwa yameteka mji wa Wikro, ulioko kaskazini mwa Mekelle, miongoni mwa miji mingine katika eneo hilo.

Ni vigumu kuthibitisha hali ya vita hivyo kwasababu mfumo wa mawasiliano ya simu na intaneti umekatizwa katika jimbo la Tigray.

Ni nini kinachojiri kwa sasa katika mji mkuu wa Tigray?

Kiongozi wa TPLF Debretsion Gebremichael ameambia shirika la habari Reuters kupitia ujumbe wa simu kwama mji wa Mekelle unakabiliwa na “mashambulio makali ya makombora”, na kuongeza kuwa vikosi vya serili vimeanza oparesheni ya kuteka mji huo.

Taarifa tofauti kutoka kwa TPLF, iliyoripotiwa na shirika la habari la AFP, inatoa wito kwa “jamii ya kimataifa kulaani mashambulio hayo ya angani kwa kutumia ndege za kivita kutekeleza mauaji”.

Pia imelaumu serikali ya Eritrea kwa kuhusika na mashambulio katika mji wa Mekelle.

Wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada na wanadiplomasia wameambiwa na wakazi kuwa kwamba walisikia milipuko kaskazini mwa mji huo

Serikali ya Ethiopia haijatoa tamko lolote kuhusiana na shambulio lake la hivi punde. Siku ya Ijumaa ilisema imeingia kilomita 20 ndani ya mji huo na umeanza “awamu ya mwisho” ya oparesheni yake dhidi ya TPLF.

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisemana kuwa vikosi vya taifa “havitashambulia” maeneo yanayokaliwa na raia.

“Usalama wa Waethiopia mjini Mekelle na maeneo mengine katika jimbo la Tigray unaendelea kupewa kipaumbele na serikali kuu,” Billene Seyoum aliongeza.

Katika mkutano siku ya Ijumaa, Bwana Abiy aliwaambia wajumbe wa usalama wa Afrika kwamba raia watalindwa.

Hata hivyo, suala la mazungumzo ya amani halikuzungumziwa na wajumbe hao hawakuruhusiwa kuzuru jimbo la Tigray.

Chama cha TPLF, ambacho kinadhibiti mji wa Mekelle, kimeapa kuendelea na mapigano.

Umoja wa Mataifa umeonya uwezekano wa kufanyika kwa uhalifu wa kivita ikiwa majeshi ya Ethiopia yatashambulia Mekelle.

Pia imeelezea hofu yake kuhusu kukosekana kwa njia ya wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu kufika eneo hilo.

Siku ya Alhamisi wanajeshi wa Ethiopia walipelekwa katika mpaka wa Tigray na Sudan, kuzuia watu wanaokimbia ghasia kuondoka nchini, kwa mujibu wawakimbizi.

Mwandishi wa BBC Anne Soy , akiwa upande wa mpaka wa Sudan aliona makumi ya wanajeshi wa Ethiopia, katika eneo hilo hali ambayo imepunguza idadi ya watu wanaovuka kuingia Sudan.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *