img

Uchaguzi Uganda 2021; Mambo matano ya kuzingatiwa katika uchaguzi mkuu

November 27, 2020

  • Na Markus Mpangala
  • Mchambuzi, Tanzania

Dakika 9 zilizopita

Matukio mbalimbali yanaonesha kuwa vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi nchini Uganda limekuwa likivuruga mikutano ya kampeni ya wagombea wa upinzani

Kinyang’anyiro cha nafasi ya urais nchini Uganda ndicho chenye mvuto zaidi kuliko kingine kikiwa kimebeba hekaheka nyingi, ufuasi mkubwa, matumaini, na hamasa miongoni mwa wapigakura kote nchini humo. Uganda ni taifa la pili la Afrika mashariki kufanya uchaguzi mkuu wake wa Januari 14 mwaka 2021 baada ya Tanzania iliyokamilisha uchaguzi wake Oktoba 28 mwaka huu, huku Kenya likiwa taifa taifa lingine linatakalofuatia katika mlolongo huo ifikapo mwaka 2022.

Nchini Uganda jumla ya wagombea 11 wanachuana kwenye nafasi ya urais huku wakifanya mikutano ya kampeni katika Kaunti 353, sawa na wilaya 134, majiji 8 pamoja na mji mkuu wake wa Kampala kwa muda wa siku 60 pekee, lakini taswira ya uchaguzi huo imekuwa yenye kuashiria hali hasi na chanya.

Matukio ya kukamatwa wagombea wa upinzani, hamasa ya wapigakura, kuibuka kwa wagombea binafsi nafasi ya urais,kampeni zilizojaa vitisho na matumizi makubwa ya vyombo vya dola, ‘kifo cha UKAWA ya Uganda’ pamoja na mgomo wa vyombo vya habari kurusha matangazo ya mikutano ya kampeni ya mgombea wa chama cha NRM Yoweri Museveni ni miongoni mwa mambo yanayoangaziwa katika kukua ama kudidimia kwa siasa za vyama vingi nchini Uganda.

Ajenda za wagombea wa urais nchini humo zimejikita katika rushwa, umasikini, miundombinu, kuboresha huduma za jamii, kuzalisha ajira kwa vijana,kusimamia uhuru wa kujieleza, kulinda usalama wa raia na mali zao. Na haya ni mambo matano ya kuzingatia yenye athari katika uchaguzi huo;

Mwenendo wa vyombo vya dola na vikundi vya kisiasa

Matukio mbalimbali yanaonesha kuwa vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi nchini Uganda limekuwa likivuruga mikutano ya kampeni ya wagombea wa upinzani. Matukio kama vile ya kuzuia kufanya mikutano ya hadhara na kumkamata mgombea wa Robert Kyagulanyi, ambaye aliwekwa rumande katika kituo cha polisi cha Nalufenya , vurugu zilizotokea kati ya Novemba 18 na 19 jijini Kampala ambapo polisi walivuruga mikutano ya kampeni ni mambo ya kufuatiliwa.

Mgombea mwingine Patrick Amuriat ameripotiwa kukutana na vizuizi vya vyombo vya dola wakati anaingia katika jiji la Arua kupitia mji wa Lemerijoa, ambako idadi kubwa ya askari walizingira njia za kuingia na kutoka maeneo hayo.

Aidha, jambo lingine ni kuibuka kwa vikosi vinavyofanya fujo dhidi ya vyama vya upinzani au chama tawala. Vikundi hivyo vimetajwa na duru za usalama kuwa vinafanya kazi ya kuvuruga mikutano ya kampeni ya wapinzani wao.

Kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu kwa jirani zao Tanzania, nako nchini Uganda mabango yenye matangazo ya wagombea wa nafasi mbalimbali kutoka vyama vya upinzani yamekuwa yakiondolewa na askari hali ambayo imelalamikiwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kutokuwa na mizani sawa ya kufanya shughuli za kampeni za uchaguzi mkuu. Mabango yaliyolengwa zaidi ni yale ya mgombea wa NUP, Robert Kyagulani.

Mgomo wa vyombo vya habari

Ingawaje haikutarajiwa lakini imeripotiwa kuwa vyombo vya habari nchini Uganda vimegoma kutangaza habari za kampeni za mgombea wa chama cha NRM. Hili ni jambo ambalo limeleta gumzo kubwa nchini Uganda, ambapo msimamo wa vyombo hivyo ni kushinikiza uwanja sawa katika kampeni za uchaguzi nchini humo.

Mijadala kupitia mitandao ya kijamii, tovuti, vyombo vya habari vya ndani na nje vimeripotiwa kugoma kurusha matangazo ya moja kwa moja (Live) ya redio na runinga mikutano ya kampeni ya mgombea wa NRM, Yoweri Museveni.

Mpinzani mkuu wa rais Yoweri Musevei
Maelezo ya picha,

Bobi Wine

Hatua ya vyombo vya habari kugoma kurusha matangazo hayo ni kutokana na kukamatwa kwa mgombea wa upinzani Robert Kyagulanyi na baadaye kuachiliwa huku baadhi ya wafuasi na wananchi wengine wakijeruhiwa wakati wa zoezi hilo.

Baadhi ya raia wa Tanzania wanaoishi na kusoma vyuo mbalimbali nchini Uganda wamemwambia mwandishi wa makala haya, “kulikuwa na jambo la kushangaza, televisheni zinarusha vipindi vya muziki wakati Museveni alikuwa akihutubia watu kule Moroto.

Unajua hapa Uganda wagombea wanafanya kampeni wilaya 134 sawa na majimbo 353, kote huko ni ndani ya siku 60 za kampeni. Sasa fujo hizi wanazofanyiwa wapigakura na wanasiasa kunaswa na vyombo vya dola ni mtihani kwa wanahabari na mwelekeo wa taifa lenyewe. Wamezima kabisa mikutano ya Museveni,”

‘Uganda bila UKAWA ya mwaka 2016’

Nguvu kubwa ya ushindi wa Museveni imetajwa kutoka ufalme wa Buganda katikati ya taifa hilo. Kulinda na kuheshimu utawala wa kifalme wa Buganda ni miongoni mwa eneo muhimu linalotengeneza nguvu ya Museveni licha ya madai kuwepo mzozo baridi baina ya pande hizo mbili.

Upande wa kambi ya upinzani nguvu zao zilitegemea umoja wao. Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2016, muungano wa vyama vya upinzani ulimuunga mkono mgombea Amama Mbabazi ambaye alionekana kuwa na nguvu zaidi wakati wa uchaguzi huo. Kwenye uchaguzi huo Mbabazi aligombea baada ya kuachana na chama cha NRM, lakini uchaguzi wa mwaka 2021 mwanasiasa mwenye nguvu amejijenga binafsi kupitia muziki.

Lakini kuelekea uchaguzi wa mwaka 2021, mwanasiasa mwenye nguvu ni Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bob Wine. Mwanasiasa huyu anazidi kumpa changamoto Museveni kuliko wakati wowote wa uchaguzi wa Uganda.

Rais Yoweri Musevei

Uhuru wa Tume ya Uchaguzi na Mahakama

Kama zilivyo nchi zingine linapofika suala la uchaguzi mkuu, Uganda nayo imekuwa ikishuhudia malumbano makali juu ya uaminifu wa Tume yao (EC). Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kumekuwa na uhaba wa uhuru katika tume yeneywe na miongoni mwa viongozi wake. Taswira waliyonayo baadhi ya wapigakura na wanasiasa kwa ujumla ni mashaka juu ya mwenendo wa tume kusimamia uchaguzi huru na haki. Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2016 asilimia 89 za kura za maoni zilitaka mabadiliko katika Tume na michakato yote ya uchaguzi mkuu.

Aidha, tume hiyo imekuwa ikikabiliwa na ukata kutokana na bajeti hafifu,udanganyifu wa majina ya wapigakura na vituo vya kupigia kura na uhesabuji wake. Uchaguzi huo unahusisha wagombea 11 walioanza kampeni tangu Novemba 19 mwaka huu; John Katumba, Robert Kyagulanyi Ssentamu, Mugisha Muntu,Henry Tumukunde, Norbet Mao, Joseph Kabuleta Kiiza, Patrick Amuriat Oboi, Fred Mwesigye, Nancy Linda Kalembe, Willy Mayambala na Yoweri Museveni.

Kizza Besigye

Mwaka 2001, Kizza Besigye alishindwa kufurukuta katika Mahakama ya Rufani baada ya jaribio la kupinga ushindi wa Yoweri Museveni. Mwaka 2006, 2011 kesi nyingine ya kupinga ushindi wa Museveni ilifunguliwa, licha ya Mahakama kukiri dosari kwenye baadhi ya taratibu za uchaguzi, lakini haikufuta matokeo ya uchaguzi. Msuguano wa mwaka 2016 ndani ya mhimili huo wa dola unatajwa kuwa huenda ukawa chachu ya kufanya uamuzi wa kupingwa matokeo ya uchaguzi mwaka huu ikiwa utatokea.

Hofu ya ugonjwa wa corona

Kampeni za uchaguzi mkuu zinafanyika huku kukiwa na tishio la ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Corona, ambapo Mkurugenzi wa Shirika la Afya barani Afrika, Dk. Matshidiso Moeti akibainisha kuwa ugonjwa huo unatarajiwa kusambaa zaidi kutoka na mikusanyiko ya kampeni na kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka kama vile krismasi.

Virusi vya corona

Mtandao wa gazeti la kila siku la Daily Monitor umeripoti kuwa baada ya miezi 8 kupitia serikali ya Uganda imeruhusu safari za Mabasi kutoka nchi hiyo kwenda nchini Tanzania. vilevile limeripoti taarifa ya kijana Baroda Kayanga Watongola mwenye umri wa miaka 27 kuwania ubunge jimbo la Kamuli huku kukiwa na kumbukumbu ya mzazi wake Hajat Rehema Watongola kufariki kwa ugonjwa wa corona mnamo Novemba 14 mwaka huu. Baroda ameomba kugombea nafasi hiyo kuziba pengo la mzazi wake ambaye alikuwa na ndoto za kuwania jimbo hilo.

Tafsiri yake ni kwamba ipo hofu ya ugonjwa wa corona ambayo imesababisha Tume ya uchaguzi nchini humo kutoa angalizo kwa viongozi wote wa timu za kampeni kuzingatia masuala muhimu ya kuepukana na ugonjwa huo.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *