img

Tanzania: Wanachama 19 wa Chadema wavuliwa uanachama

November 27, 2020

Uamuzi huo ulitokana na maazimio ya Kamati Kuu ikiyokutana leo Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, wanachama hao wana nafasi ya kuomba radhi kwa maandishi ili kurejeshewa uanachama wao.

Aidha wana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30 kupnga uamuzi huo wa Kamati kuu.

Mapema Ijumaa, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Mahera leo Ijumaa alisema katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika alimuandikia barua Novemba 19, 2020 yenye orodha ya majina ya wanachama wanaopendekezwa kuteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum na kwamba tume hiyo ilitumia orodha hiyo kuteua wabunge wa viti hivyo.

Kikao cha kamati kuu ya Chadema kilikuwa kimeitishwa ili kuwajadili wanachama wao walioapishwa Novemba 24 kuwa wabunge wa viti maalum mjini Dodoma.

Hatua hiyo ya kuapishwa ilipingwa na viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho wakieleza kuwa hakikuyapitisha majina yao na kuitaka tume hiyo kusema ukweli.

Walengwa ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Kufuatia kuapishwa kwao, Mnyika alifanya mkutano na wanahabari na kueleza kuwa hakuna kikao kilichokaa na kupitisha majina hayo na kuyapeleka NEC lakini leo tume hiyo imemtaja Mnyika kuwa aliwasilisha majina hayo.

Lakini katika taarifa yake kwa umma, Mahera alisema, “ifahamike kwamba katibu mkuu wa Chadema alimuandikia mkurugenzi wa NEC barua yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/20/TU/05/141 ya Novemba 19 ambayo iliwasilisha orodha ya majina ya wanachama wanaopendekezwa kuteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum.”

“Tume ilitumia orodha iliyowasilishwa na Chadema kuteua wabunge wa viti hivyo. Hivyo, wabunge wanawake wa viti maalum wa Chadema waliteuliwa kwa kuzingatia taratibu zote za kikatiba na kisheria,” aliongeza.

Pamoaja na viongozi wa chama, wajumbe wengine wa kikao caha Ijumaa walikuwa ni John Heche, Mchungaji Peter Msigwa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, Boniface Jacob, Suzan Kiwanga, John Mrema, Julius Mwita, Rodrick Rutembeka, Patrick Ole Sosopi, Hashim Juma na John Pambalu, ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza la vijana wa chama hicho.

-Imetayarishwa na Idd Uwesu, VOA, Dar es Salaam

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *