img

Ummy Mwalimu afanya ziara Bandari ya Tanga ahaidi kuwa balozi wa kuitangaza

November 26, 2020

 

MBUNGE wa Jimbo la Tanga (CCM) Ummy Mwalimu leo amefanya ziara ya kutembelea Bandari ya Tanga na kufanya mazungumzo na uongozi wake kuona namna inavyofanya shughuli zake huku akiwahaidi kuwa balozi wao katika kuitangaza ili kuvutia wafanyabiashara kuitumia.

Ummy ambaye alifika Bandarini hapo ikiwa ni ziara yake ya siku moja kuona namna uboreshwaji wa Bandari hiyo ulivyofanywa jambo ambalo alikuwa akilipa nguvu wakati wa kampeni zake zake huku akiridhishwa na kazi iliyofanywa na katika uboreshaji.

Alisema lengo la kuitembelea ni kufanya mazungumzo na uongozi wa Bandari hiyo kwa lengo la kuangalia utendaji wao,mikakati yao na changamoto ambazo wanakabiliana nazo ili kuona namna ya kuzifikisha kwenye mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi.

Mbunge Ummy alisema moja ya vipaumbele vyake wakati akiomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa Jimbo hilo ilikuwa ni kuhakikisha bandari hiyo inakuwa kichocheo cha kasi ya ukuaji wa uchumi wa Jiji la Tanga.

Alisema maboresho hayo ya Bandari ya Tanga yatawezesha kwa mwaka meli kubwa 400 kutia nanga Bandarini kutoka meli 157 na hivyo kuongeza fursa za ajira,uchumi wa wakazi wa mji huo ikiwemo mzunguko wa kibiashara.

Mbunge huyo alimshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kuwapatia fedha Bilioni 256 ambapo sasa kazi ya kuongeza kina na kufanya upanuzi wa Bandari hiyo awamu ya pili unaendelea na utasaidia kuifanya bandari hiyo kuwa bora zaidi ya awali.

Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Donald Ngaire alisema Bandari hiyo ipo kwenye maboresho makubwa ya uboreshaji wa miundombinu pamoja na huduma.

Alisema awamu ya pili ya utekelezaji wa kazi hiyo umeshaanza na utatekelezwa kwa miezi 22 ambapo mara baada ya mradi huo kukamilika utawezesha meli kubwa kutia nanga gatini na hivyo kuongeza kiwango cha mzigo unaohudumiwa.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *