img

Uchaguzi Tanzania 2020: Upi mustakabali wa mgogoro wa wabunge wa viti maalum Chadema?

November 26, 2020

  • Na Ezekiel Kamwaga
  • Mchambuzi

Dakika 7 zilizopita

Wafuasi wa Chadema Tanzania

WATALIANO wana msemo mmoja wa kuelezea kuhusu tukio ambalo vyovyote utakavyofanya, kuna watakaofurahi na kuna watakaonuna. Hutaweza kuwaridhisha wote. Msemo huo; Situazione Senza Soluzione (Situation Without Solution) unasadifu mazingira yanayokikuta Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika wakati huu.

Wabunge 19 wa chama hicho kupitia utaratibu wa viti maalumu juzi wameapishwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, kuwa wabunge wa Bunge la 12; kinyume na msimamo wa chama chao ambacho kinaamini kitendo hicho kinahalalisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu – uliokipa ushindi wa asilimia 84 chama tawala cha CCM.

Kwa namna yoyote unavyoliangalia jambo hili; huoni makosa ya upande mmoja katika jambo hili. Kwa upande mmoja, hii si mara ya kwanza kwa vyama vya upinzani Tanzania kukataa kutambua matokeo ya uchaguzi lakini bado vikaingia katika Bunge au Baraza la Wawakilishi – lakini, unaweza pia kuelewa kwanini wapo wanaopinga hatua hiyo ya Chadema kwa sababu ya namna uchaguzi wenyewe ulivyofanyika.

Hii ndiyo ile hali ya kuwa na jambo ambalo suluhusho lake haliko wazi kama ambavyo Wataliano wanazungumzia katika msemo wao huo. Hata hivyo, pasi na shaka yoyote ile, huu unaweza kuwa mtihani mkubwa zaidi kukikumba Chadema katika miaka ya karibuni na huu ndiyo mtihani wa kwanza wa chama hicho katika muongo huu mpya.

Kwanini tukio hili si la kawaida

Tundu Lissu kushoto ndiye aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema
Maelezo ya picha,

Tundu Lissu kushoto ndiye aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema

Tukio la wabunge hao 19 kuapishwa jijini Dodoma lilikuwa la kushtukiza kwa sababu mbili kubwa; mosi kutokana na ukweli kuwa wengi hawakutaraji litokee kwa vile uongozi wa juu wa chama hicho kupitia kwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, ulishasema halitawezekana lakini la pili namna ulivyofanyika.

Katika historia ya Bunge la Tanzania, hii ilikuwa mara ya kwanza kwa kundi kubwala wabunge kuapishwa kwa wakati mmoja wakati hakuna mkutano wa Bunge unaoendelea. Mara zote wabunge wa Tanzania wamekuwa wakiapishwa wakati wa Bunge na ndiyo sababu ilibidi Ndugai afafanue kuwa kanuni zinataka wabunge waapishwe mbele ya Spika na si lazima iwe wakati wa vikao vya mhimili huo wa dola.

Wabunge walioapishwa ni Halima Mdee, Grace Tendega, Esther Matiko, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed.

Wengine ni Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Rwamlaza.

Katika mazungumzo yangu yasiyo rasmi na pande hizi mbili nimebaini hoja mbili zinazokinzana. Kundi la wabunge hao linaloongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee, linaamini kwamba hakuna jambo la ajabu kuingia bungeni hata kama uchaguzi wenyewe haukuwa halali.

“Katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 1995, Chama cha Wananchi (CUF) kilipokwa ushindi lakini wajumbe wake wakaingia katika Baraza la Wawakilishi. Mwaka 2010, sisi Chadema tuligomea matokeo ya uchaguzi mkuu wa wakati ule lakini tukaingia bungeni.

“Mwaka 2015, tuligomea pia matokeo kiasi kwamba wakati Rais John Magufuli alipoingia bungeni kufungua rasmi Bunge la 11, wabunge wa upinzani tulitoka ndani ya Bunge. Hata hivyo, sote tuliingia bungeni na kuendelea na shughuli zetu. Kwanini mwaka huu iwe tofauti kwamba hata bungeni tusishiriki?”alihoji mmoja wa wabunge walioapishwa juzi aliyezungumza nami kwa masharti ya kutotajwa jina katika uchambuzi huu.

Wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema wakati wa kumchagua mgombea wa Chadema
Maelezo ya picha,

Wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema wakati wa kumchagua mgombea wa Chadema

Ni hoja za namna hii ndizo zinazozua maneno katika baadhi ya duru za kisiasa kwamba tatizo kubwa la safari hii ni kwamba wanaofaidika na uamuzi huu ni wanawake watupu na kuwa katika miaka ya nyuma wanaume walikuwa wakifaidika lakini safari hii hawatakuwemo bungeni.

Chadema kama chama, kimekasirishwa na ukweli kwamba wanachama wake hawa, kupitia Bawacha, wameamua kufanya maamuzi pasipo maelekezo rasmi kutoka katika chama. Mtazamo wa chama na kwamba endapo hili litaruhusiwa, chama hakitakuwa tena na uwezo wa kitaasisi wa kuzuia wanachama wake kufanya wanachokitaka pasipo kujali chama kinataka nini.

Kwa lugha ya Kireno, Chadema inataka wanachama wake wafuate kile kinachoitwa Áligna Correcta (msimamo mmoja – mstari mmoja); ikimaanisha wanachama wanatakiwa kusikiliza maelekezo ya chama peke yake na si vinginevyo.

Kwa kawaida, orodha ya wabunge wa viti maalumu wa chama hupelekwa kwa Spika wa Bunge kupitia barua inayoandikwa na Katibu Mkuu wa chama. Katika tukio hili, Mnyika hakuandika barua kama utaratibu ulivyo na hadi sasa haijawekwa wazi ni nani aliyeandika barua hiyo.

Hata hivyo, Mdee ameitengeneza Bawacha kuwa mojawapo ya ngome kuu za Chadema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Nguvu na ushawishi wa Bawacha umekua kiasi kwamba katika uchaguzi mkuu uliopita, Chadema iliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagombea ubunge wanawake majimboni kuliko chama kingine chochote cha siasa hapa nchini.

Katika mazungumzo yangu na baadhi ya wabunge walioapishwa, nimebaini kwamba katika hatua hii ambayo ni uamuzi wa Bawacha nzima, Kamari pekee inayocheza ni kuwa na wabunge wachache wenye uwezo, jasiri na watakaokuwa na uwezo wa kujenga hoja nzito bungeni.

Ndiyo sababu, katika mikoa zaidi ya 30 hapa nchini, Bawacha imewachuja wanasiasa hao kwa kuangalia uwakilishi wa mikoa yao, uwezo na umri; wakichanganya wabunge wazoefu na wengine wanaoingia kwa mara ya kwanza.

Nimeambiwa kwamba wabunge waliopitishwa wamepigiwa kura na kushinda katika maeneo yao kupitia Bawacha na Kamari inayochezwa hapa ni kuwa wanawake hawa watachapa kazi kwa namna na viwango vya kawaida vya Chadema.

Kwa sababu uamuzi huu ni wa Bawacha – na kuna taarifa kwamba wengi wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wanaunga mkono hatua hii ya wabunge wanawake kuamua kukubali kuapishwa; uamuzi wowote wa kutumia mtulinga unaweza kufanya hali hii teketeke kuwa mbaya zaidi.

Mgogoro au tufani katika kikombe?

Jambo pekee ambalo limelifanya jambo hili kuwa kubwa kuliko ambavyo lingeweza kuwa ni namna baadhi ya viongozi mashuhuri wa Chadema walivyoamua kutoka hadharani na kuonyesha kutokubaliana na hali hii.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa, Halima alimshukuru Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwa kuwaruhusu waapishwe – moja kwa moja akitaka kuonyesha picha kwamba hakuna tatizo lolote na pengine akitaraji jambo hili kumalizwa kupitia vikao vya chama.

Hata hivyo, Mnyika, Mkuu wa Mawasiliano na Itifaki wa Chadema, John Mrema pamoja na aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Rorya, Ezekia Wenje, wameandika katika mitandao ya kijamii maelezo ya kuonyesha kwamba kitendo hicho kimekiuka misingi ya chama hicho na Wenje ameenda mbali kwa kupendekeza wanawake hao wafukuzwe kwenye chama.

Si Mbowe wala Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, ambao wametoa msimamo wao hadharani kuhusu jambo hili. Hata hivyo, kwa namna lilivyo sasa, ni Mbowe pekee anayeweza kulifanya likatoka kuwa tufani katika kikombe ( a storm in a tea cup) na kuwa suala la mawasiliano mabaya tu.

Mbowe ni veterani wa migogoro ndani ya chama hicho. Yeye amekuwa kiongozi wakati chama kikipitia katika misukosuko ya kifo cha aliyekuwa Makamu wake, marehemu Chacha Wangwe, mgogoro dhidi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, uliotishia kukipasua chama hicho na kuondoka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa.

Tofauti ya kinachoendelea sasa na mingine ya huko nyuma ni kuwa wakati ule alikuwa anashughulika na migogoro ya watu binafsi dhidi yake au chama lakini sasa ni watu takribani 19 – wote wakiwa wanawake. Katika mazingira ya kisiasa ya sasa duniani; hakuna mwanasiasa anaweza kushinda vita dhidi ya wanawake.

Freeman Mbowe kushoto na viongozi wengine wa Chadema

Chadema kinaweza kuwafukuza wanachama wake hawa kwa sababu ya kukiuka taratibu za chama. Huko nyuma, CCM iliwahi kuwafukuza uanachama wake akina Sofia Simba na wenzake kwa sababu ya kukataa utaratibu uliotumika kumpitisha John Magufuli kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi wa mwaka 2015. Kwa hiyo suala la kukiuka utaratibu ni suala nyeti kwa vyama vya siasa.

Tofauti ya Chadema na CCM wakati ule ni kwamba chama tawala kilichukua maamuzi hayo wakati kimeshinda uchaguzi na kwa kiasi kikubwa kikiwa kinaungwa mkono na wengi wa wanachama wake.

Mazingira ya kisiasa ya Chadema kwa sasa hayakifanyi kuwa katika msingi imara wa kuchukua maamuzi haya. Uamuzi wa kukubali kwenda bungeni umefanywa na jumuiya nzima ya chama ambayo kwa sasa ndiyo yenye nguvu na ushawishi zaidi miongoni mwa jumuiya nyingine za chama hicho na kuwafukuza itakuwa sawa na chama kujikata miguu chenyewe.

Kuwa bungeni kwa Chadema kutakipa chama hicho fursa nyingine ya kupata jukwaa la kueleza mipango yake, kuisema serikali na kuzidi kuiatamia demokrasia ya vyama vingi hapa nchini ambayo kwa sasa haiko katika hali ya kiafya kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.

Hatua hii ya wabunge wa Chadema pia ni muhimu kwa sababu itasaidia kupunguza machungu kwa wengine. Kwa mfano, mbunge mpya, Nusrat Hanje, alikuwa na kesi mahakamani na hakuwahi kupewa dhamana lakini ametolewa mara baada ya kupitishwa kuwa mbunge. Sasa ana fursa ya kuendesha mapambano yake akiwa bungeni. Hii ndiyo tafsiri ya kuatamia demokrasia.

Ninafahamu kwamba akina Mdee hawatazungumza chochote hadharani kukisema chama chao kwa sababu wote ni wanachama watiifu kwa Chadema na kwa wao, hatua yao hii ni sehemu ya mapambano ya kudai demokrasia hapa nchini.

Lakini, kwa sababu sasa wamekuwa wanasiasa wazoefu pia, wanajua kwamba kinga yao pekee kwa sasa ni wingi wao. Wanajua pia kwamba wao ni wanawake na uamuzi wowote utakaofanywa na wanaume dhidi yao – hautakuwa na athari nzuri kwa chama chao.

Katika Kiswahili cha Kimakonde; hali hii ya Chadema inaweza kuelezwa katika msemo mmoja tu; Ndani Ntiti, Nje Ntiti – wale walio ndani ya chama wanataabika na hatua za kuchukua dhidi ya kundi hili na wabunge hawa ambao wako nje ya wafanya maamuzi, nao hawana raha huko waliko.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *