img

Bavicha wahoji uteuzi kina Halima Mdee na wenzake 18

November 26, 2020

 

Kuapishwa kwa wanachama 19 wa Chadema kuwa wabunge wa Viti Maalum kumezidi kuibua hali ya sintofahamu baada ye leo Alhamisi Novemba 26, 2020 Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kueleza orodha ya makada hao imetoka kwa nani.

Kauli hiyo imetolewa leo na mwenyekiti wa baraza hilo,  John Pambalu katika mkutano wake wa waandishi wa habari kuzungumzia sakata la wanachama hao kwenda kuapa bungeni.

Pambalu amesema baraza hilo linaunga mkono msimamao wa Chadema juu ya wanachama  hao kwenda kinyume na mwongozo wa chama hicho.

“Tunaunga mkono watu hawa waitwe ili waweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Kamati Kuu ya chama ambayo inawakilishwa na vijana hatukuwahi kujadili na kupitisha orodha ya Viti Maalum.”

“Kwa kuwa chama hakijapitisha na katibu mkuu hakuwahi kusaini kuonyesha chama kimeteua mbunge wa viti maalum, sisi kama vijana tunaitaka Tume ya uchaguzi ijitokeze na kusema majina waliyoyapitisha walipewa na nani,” amesema Pambalu.

Hata hivyo,  jana Mwananchi Digital lilizungumza na mkurugenzi wa NEC, Dk Wilson Mahera kutaka ufafanuzi kuhusu uteuzi huo na kutaka waulizwe Chadema.

Wanachama waliokwenda kuapishwa bungeni ikidaiwa kuwa si kwa baraka za Chadema ambacho msimamo wake ni kutopeleka wabunge kutokana na kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa.

Wengine ni Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau,  Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao,  Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake baada ya kuapishwa, Mdee alisema walikuwa na baraka za chama hicho huku Matiko ambaye alizungumza na Mwananchi Digital akieleza kuwa yeye alipewa habari kuhusu kwenda kuapishwa Dodoma na mamlaka ambayo hakuiweka wazi.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *