img

Simba Yazinasa Siri za Wanigeria

November 25, 2020

WAMEKWISHA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mabosi wa Simba kuzinasa mkononi siri zote zinazowahusu wapinzani wao, Plateau United ya Nigereia ikiwemo staa wao matata.

 

Simba wamepata siri hizo ikiwa ni siku chache kabla ya kucheza na Plateau kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali, huku wakielezwa, Junior Salomon raia wa Benin ndiye mtu wa kumchunga kutokana na madhara aliyokuwa nayo.

 

Msafara wa kikosi cha Simba, jana Jumanne uliondoka jijini Arusha kuelekea nchini Nigeria tayari kwa mechi yao ya kwanza ya michuano hiyo itakayochezwa wikiendi hii kabla ya ile ya marudiano kati ya Desemba 4-6 jijini Dar.

 

Chanzo kutoka ndani ya kambi ya Simba iliyowekwa kwa muda jijini Arusha, kimeliambia Spoti Xtra, kuwa wataenda Nigeria na nyota 23 pekee ambapo kuna panga kubwa limepitishwa kwa wachezaji wakiangalia nidhamu, viwango na majeruhi.

 

Pia chanzo hicho kimeongeza kuwa, wakati wakielekea Nigeria, tayari wana taarifa zote muhimu kuhusu wapinzani wao hao ambapo kocha wa kikosi hicho, Sven Vandenbroeck amepanga kwenda kucheza soka la kushambulia kwa ajili ya kumaliza shughuli ugenini.

 

“Kwa sasa tuna siri zote za wapinzani wetu Plateau United kabla ya kucheza nao, ikiwemo ya mtu hatari ambaye tunatakiwa kumuangalia zaidi.

 

“Huyo ni Junior Salomon raia wa Benin ambaye ndiye mtu muhimu kikosini hapo, hivyo lazima achungwe kwa dakika zote. “Lakini pia wachezaji wanatakiwa kwenda kushambulia na kupata ushindi kwenye mechi hii na kumaliza kila kitu kabla ya kurudi Dar kurudiana nao.

 

“Juu ya watu ambao wanaenda huko ni kwamba kumepita panga kubwa ambapo ni wachezaji 23 tu ndiyo wanaoenda. “Katika listi hiyo wameondolewa wale ambao nidhamu zao zimeonekana kuwa mbovu, walioshuka viwango pamoja na majeruhi wa muda mrefu,” kilisema chanzo hicho.

MWANDISHI WETU

The post Simba Yazinasa Siri za Wanigeria appeared first on Global Publishers.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *