img

Madiwani watakiwa kutoendeleza makundi

November 24, 2020

 Na Hamisi Nasri, Masasi 

   CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kimewataka madiwani wa chama hicho ambao wanaendeleza makundi yasio na tija ndani ya chama kuacha vitendo hivyo badala yake waungane pamoja ili kusimamia miradi ya maendeleo inayoletwa na serikali kwenye maeneo yao.

  Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Masasi na mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Masasi,Edward Mmavele alipokuwa akizungumza na madiwani hao katika kikao cha uchaguzi wa kuchagua wenyeviti wa halmashauri ya mji Masasi pamoja na halmashauri ya wilaya ya Masasi, uchaguzi huo umefanyika katika ukumbi wa chama cha mapinduzi wilaya hiyo.

  Mmavele alisema kuwa wapo baadhi ya madiwani wa chama hicho ambao bado wanaendeleza makundi ambayo yalijitokeza katika uchaguzi uliomalizika oktoba 26 mwaka huu na kwamba makundi hayo hayana tija kwa sasa na yanapaswa kufunjwa mara moja.

  Alisema kuendeleza makundi ndani ya chama ni hatari na kunalenga kutaka kukichafua chama ikiwa ni pamoja na kuzorotesha jitahada za chama hicho katika kutekeleza ilani ya uchaguzi pamoja na miradi ya maendeleo.

  Alisema kwa sasa ni wakati muhafaka wa kufunja makundi yote yaliyopo ndani ya chama na kuungana pamoja  ili kuweza kukipigania chama katika kusimamia maendeleo ambayo yanalenga kuwadumia wananchi wa wilaya ya Masasi. 

  Mmavele alisema kila diwani aliyepita katika eneo lake kwenye uchaguzi ni kwamba wananchi wake wamempa ridha na kumuamini kuwa anauwezo wa kuwasemea matatizo yao na kuwaletea maendeleo na sio kwenda kujiunga katika makundi ya kujengeana chuki,uhasama na madiwani wenzake.

   ‘’Naomba tuyavunje makundi kwani uchaguzi umeshapita hakuna sababu ya kuendeleza makundi miongoni mwetu bali turudi pamoja na tufanye kazi ili tukijenge chama na tuwahudumie wananchi wetu,”alisema Mmavele 

   Alisema kuendeleza makundi ni kujiweka katika hatari ya kuweza kupoteza nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa mwaka 2025 kwa vile uwepo wa makundi hayo wenda yakadumu mpaka uchaguzi ujao.

  Mmavele alisema kuna hatari kubwa ya kuwa na makundi na moja ya hatari hizo ni pamoja na kushindwa kufanya vikao halali vya vyama hasa katika ngazi ya vijiji.

  Alisema uwepo wa makundi pia unaweza kuchangia kushindikana kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutotoa huduma stahiki kwa wananchi.

  Naye Ibrahim Chiputula ambaye ni mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi alisema ushirikiano ni jambo jema kuliko kuwa na makundi yasio na tija ambayo yatapelekea kukipa dosari chama cha mapinduzi.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *