img

Ghasia za uchaguzi wa 2007 Kenya: Ufufuzi wa kesi za ghasia hizo wadaiwa kuchochewa kisiasa

November 24, 2020

Dakika 14 zilizopita

wafuasi wa upinzani walikabiliana na maafisa wa polisi Jijini nairobi

Maelezo ya picha,

Wafuasi wa upinzani walikabiliana na maafisa wa polisi Jijini Nairobi

Viongozi mbali mbali nchini Kenya wamemshutumu mkurugenzi wa uchunguzi wa mashtaka ya jinai nchini Kenya George Kinoti kufuatia hatua yake ya kufufua kesi za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/08.

Kiongozi wa chama cha kisiasa cha Narc Kenya Martha Karua amesema kwamba hatoomba msamaha kwa kumuwakilisha rais wa zamani Mwai Kibaki mwaka 2007 baada ya jina kulitaja jina lake katika kesi hiyo.

Karua amesema kwamba waathiriwa wa ghasia hizo wanapaswa kupata haki na kuwatahadharisha wakosoaji wake kwa kumuhusisha na kesi hizo kwa misingi kwamba ndiye aliyekuwa wakala mkuu wa Kibaki katika jumba la mikutano la Kenyatta International Conference Center KICC.

Jumba hilo lilitumika na Tume ya uchaguzi nchini ECK ambayo sasa imebadilika na kuwa Tume huru ya uchaguzi na mipaka kama makao makuu ya kujumlisha kura zilizopigwa.

“Watu waliowaagiza wafuasi wao kuua, kupora na kutekeleza ghasia kama njia ya kuchukua mamlaka kwa nguvu, wanapaswa kubeba msalaba wao wa kusababisha ghasia za PEV. Huwezi kufuta historia kwa kutumia jina langu kuwasafisha, wala huwezi kunitisha au kunizuia kwa kusema uwongo” .

“Siombi msamaha kabisa kwa kuwa wakala wa Kibaki katika jumba la KICC, kituo cha kujumlisha hesabu ambapo Raila Odinga (kiongozi wa ODM) alikuwa na Orengo James (Seneta wa Siaya) kama wakala wake mkuu. Sihitaji msamaha kutoka kwa mtu yeyote wala sitawahi kumtafuta yeyote kwa kuwa wakala wa Kibaki na mfuasi wake wakati huo, “Karua alituma ujumbe wa twitter akisema.

Wakitoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii , viongozi mbalimbali walitaja hatua hiyo ya bwana Kinoti kama ilioshinikizwa kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2022.

Seneta wa Nakuru Susan Kihika alimshutumu bwana Kinoti kwa kujaribua kuchochea jamii na kuzua hali ya wasiwasi nchini

Aliionya serikali kwa kutumia vifaa vya serikali kwa lengo la kuwanyamazisha wapinzani wa kisiasa.

”Munapomtumia mtu kama Kinoti ili kujaribu kuongeza wasiwasi na kuchochea jamii dhidi yazo utajua wanatapatapa. Tunatumai hawatawauwa watu , kuchoma nyumba ili kuhakiki taarifa ya kinoti”, alichapisha ujumbe katika mtandao wa twitter, akiongezea kwamba Wakenya wanapaswa kuishi kwa amani.

Kwa upande wake Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot alitaja hatua hiyo kama ya aibu akisema kwamba Kinoti hatofanikiwa zaidi ya Shirika la haki za kibinadamu la Kenya Human Rights na tume ya kuchunguza ghasia za baada ya uchaguzi CIPEV .

“Ni aibu sana kwa bwana Kinoti kuzua tena masuala kama hayo yasioisha kwa kuwatumia waathiriwa wa ghasia hizo za 2007. Hawezi kusema kwamba ana uwezo kufanya uchunguzi zaidi ya KNHRC na tume ya waki”, alisema.

Ameitaka serikali kuzifufua upya ripoti mbili za tume zilizochunguza ghasia hizo iwapo ni kweli hatua yao haikuchochewa kisasa.

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwah naye alimshutumu Kinoti kwa kutumiwa na mawakala na matapeli kukabiliana kisiasa.

Upande wake Seneta Mutula Kilonzo Jnr pia aliingilia mjadala huo aksema kwamba ufufuzi wa kesi hizo kwa lengo la kuwatishia watu binafsi unapaswa kuchunguzwa.

Alishangazwa kwanini vifaa vya usalama vya serikali vilikosa kupata ushahidi mwaka 2008 ili kuwashtaki wahusika kabla ya kubadilika na kudai kwamba vinaandaa kesi kali dhidi ya washukiwa.

Je Mkurugenzi huyo wa uhalifu wa Jinai alisema nini?

Siku ya Jumatatu mkurugenzi huyo wa jinai aliahidi kuwasilisha mahakamani kesi nzito yenye ushahidi dhidi ya washukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 baada ya kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya waathiriwa katika makao makuu ya jinai.

Alisema kwamba maafisa wa polisi tayari wamekusanya sampuli 118 za kesi kutoka kwa mashahidi na walalamishi ambazo zinashirikisha kesi 48 za kuwafurusha watu kwa kutumia nguvu katika makaazi yao.

Alisema kwamba ana matumaini katika ukusanyaji wa ushhaidi akisema kwamba polisi wataanzaa kesi kali ambayo wahalifu hawataweza kuikwepa. Tutabeba biblia na kuapa mbele ya mahakama tukisema kwamba mtu huyu alimuua mwenzake na kuchukua ardhi yake, alisema.

Akizungumza kwa hasira, Kinoti alizungumzia kuhusu kiongozi mmoja wa dini ambaye alifariki mbele ya washambuliaji wake akiwa amepiga magoti akiwaomba kumwachilia lakini hawakumsikiza.

Nendeni muone idadi ya atoto waliochomwa. Mbao waliwachwa kama vipande vya kuni….kama makaa, wazee ambao hawawezi kutembea walichomwa , alisema, akitaja taarifa alizopewa na mashahidi.

Ghasia za baada ya uchaguzi

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/8 kiongozi wa upinzania Raila Odinga alisema kuwa wafuasi wa aliyekuwa rais Mwai Kibaki ‘walimuibia kura’ hali iliyowapelekea kufanya maandamano na ghasia.

Punde baadaye, hali iliyoibuka ilikuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa misingi ya ukabila, hususan katika maeneo ya watu wengi wenye mchanganyiko wa makabila,.

Takriban watu 1,000 waliuawa na wengine laki sita kuachwa bila makao. Wakenya wanne akiwemo rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walikabiliwa na mashtaka katika mahakama kuhusu uhalifu wa kivita iliopo the Hague mwezi Aprili. Hatahivyo kesi hiyo ilikosa ushahidi wa kutosha na kutupiliwa mbali na mahakama hiyo, huku washukiwa hao wakiachiliwa huru.

Source link

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *