img

Promota wa Kiduku adaiwa kutapeli mabondia, polisi wamsaka

November 23, 2020

INAELEZWA promota wa pambano la ngumi za kulipwa kati ya Mtanzania, Twaha Kiduku na Sirimongkhon Lamthuam raia wa Thailand anatafutwa na polisi wa kituo cha Kilwa Road kufuatia madai ya kutowalipa mabondia fedha zao akiwemo Kiduku na watoa huduma wengine waliokuwepo katika pambano hilo lililochezwa mwezi uliopita.

Katika pambano hilo ambalo lilifanyika kwenye Ukumbi wa PTA jijini Dar, Kiduku alifanikiwa kuibuka na ushindi wa TKO ya raundi ya saba ambayo ilitokana na mpinzani wake kudai bega lake kushtuka kutokana na makonde makali ya Kiduku.

Uchunguzi uliofanywa na Championi Ijumaa umebaini kuwa mabondia wote waliocheza kwenye pambano hilo, walikuwa wamelipwa malipo nusu na

wengine hawakulipwa kabisa hali iliyosababisha promota huyo kuingia mitini na kila anapopigiwa simu hutoa sababu mpya.

Championi lilifanikiwa kumpata Kiduku ambaye amekiri kutomaliziwa pesa zake hadi jana jioni na promota huyo na kudai kuwa kila akimpigia simu amekuwa haipokei.

Baadhi ya mabondia waliokiri kumdai promota huyo anayetafutwa na polisi ni Juma Misumari na kocha wake kutoka Morogoro, Twaha Kiduku, Maono Ally na Jongojongo kutoka Bagamoyo na Alphonce Mchumia Tumbo.

Baadaye gazeti hili lilimtafuta bondia wa zamani Chaurembo Palasa ambaye alimdhamini kwa watu waliotoa huduma kwenye pambano hilo, amekiri kutafutwa kwa promota huyo kutokana kitendo cha kushindwa kulipa watu wanaomdai fedha zao kwa kazi waliyomfanyia.

“Kwanza nilikamatwa kwa sababu yake maana nilimdhamini katika baadhi

ya mambo lakini ajabu hadi sasa hajalipa na hapatikani, nilichofanya nimekata RB katika Kituo cha Barabara ya Kilwa na anatafutwa kwa sababu suala hilo wanamdai wapo wengi sana,” alisema Chaurembo.

Alipotafutwa promota huyo kwa njia ya simu hakuweza kupokea licha ya kuita kwa muda mrefu kabla ya kutuma ujumbe wa kumtaka mwandishi ajitambulishe na hata alipofanya hivyo hakuweza kupokea simu yake.

Ibrahim Mussa,

Dar es Salaam

The post Promota wa Kiduku adaiwa kutapeli mabondia, polisi wamsaka appeared first on Global Publishers.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *