img

Mbinu 7 za kukurahisishia kusoma Vitabu unapokuwa na shughuli nyingi

November 23, 2020

Kama nilivyoeleza kwenye makala mbalimbali kuwa kusoma vitabu kuna manufaa mengi sana ambayo kila mtu mwenye maono anapaswa kuyapata.

Vitabu hubeba maarifa kemkem ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kukusaidia kubadili maisha yako.

Hata hivyo bado watu wengi wanashindwa kusoma vitabu jinsi ipasavyo. Ikiwa unapenda kusoma vitabu lakini una shughuli nyingi, basi karibu nikushirikishe mbinu kadhaa zitakazo kuwezesha kusoma vitabu kwa urahisi.

1. Tumia simu yako

Karibu kila mtu leo ana simu ya kisasa ya mkononi (smartphone), hata hivyo bado watu wengi hawafahamu nguvu au matumizi adhimu yanayopatikana kwenye simu hizo. Ni ukweli usiopingika kuwa ulimwengu wa kutumia simu kama kifaa cha kupiga na kupokea simu pamoja na kutuma na kupokea ujumbe mfupi umepitwa na wakati.

Kwa kupitia simu yako ya mkononi unaweza kufanya mambo lukuki kama vile kupata huduma za afya, kupata huduma za kifedha, kupata habari na burudani, kujipatia kipato, kutunza kumbukumbu, kujiongezea maarifa, n.k.

Hivyo basi, ili uweze kusoma vitabu kwa urahisi, ni vyema ukaitumia simu yako ya mkononi kama kifaa kwa ajili ya kusoma vitabu mbalimbali; unaweza kuvipakua na kuvisoma wakati wowote au ukavisoma moja kwa moja kwenye mtandao wa intaneti.

2. Azima vitabu vingi kuliko uwezo wako

Unapoazima vitabu vingi kuliko uwezo wako, moja kwa moja vitakuhamasisha ufanye bidii kuvimaliza kabla ya wakati wa kuvirudisha haujafika.

Kamwe usikubali kitabu kirudi bila kusomwa, hivyo tumia muda wako vyema na pangilia ratiba yako kwa njia ambayo itakuwezesha kutimiza lengo lako.

3. Tafuta mshindani

Ili uhamasike zaidi kusoma vitabu hata ikiwa una shughuli nyingi, ni vyema ukatafuta mtu utakayeshindana naye kwenye swala la kusoma vitabu.

Mnaweza kujiwekea lengo la kukamilisha vitabu au kitabu fulani kabla ya muda fulani au hata kujiwekea zawadi kwa atakayekuwa wa kwanza kukamilisha lengo hilo.

4. Jiwekee lengo la kusoma kurasa kadhaa

Hata kama una shughuli nyingi, jiwekee lengo la kurasa unazotakiwa kusoma kila siku. Ikiwa umejiwekea lengo la kusoma kurasa 10 kwa siku, basi hakikisha unazikamilisha.

Unaweza kusoma kila mahali, ukiwa unakula, unatembea au hata ukiwa umepumzika kwa muda.

5. Soma unapoamka na unapokwenda kulala

Ikiwa mchana unakuwa na shughuli nyingi sana, basi jiwekee lengo la kusoma vitabu kila unapoamka au unapolala. Tenga angalau dakika 30 kila mara unapoamka na unapokwenda kulala na usome kurasa kadhaa za kitabu.

Kwa kuhakikisha unalitimiza lengo hili, utaweza kusoma vitabu vingi sana kwa urahisi bila kupangua ratiba yako ya mchana yenye shughuli nyingi.

6. Soma unaposafiri

Ukiwa unasafiri ni muda mzuri sana wa kusoma vitabu; ni jambo la kushangaza unasafiri safari ya siku nzima alafu bado unasema huna muda wa kusoma vitabu. Muda wote uliokuwa kwenye basi au ndege uliutumiaje?

Unapojiandaa kwa safari, andaa pia kitabu cha kusoma kwenye safari hiyo; ikiwa ni vigumu kubeba kitabu kilichochapishwa, soma basi vitabu kwa kutumia simu yako ya mkononi.

Ikiwa unasoma vitabu vya kiingereza unaweza kuvibadili kuwa sauti kwa kutumia programu kama vile Balbolka ili uvisikilize badala ya kuvisoma.

7. Pitia upya matumizi yako ya muda

Je, unapata muda wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram au YouTube? Je unapata muda wa kucheza gemu au kutazama filamu?

Ikiwa unapata muda wa mambo haya, basi unatakiwa kuacha kulalamika kuwa huna muda wa kusoma vitabu bali pitia upya matumizi yako ya muda.

Ni vyema ukapangua au kupunguza mambo yasiyokuwa na msingi kwenye ratiba yako ili uutumie muda unaoupoteza kwa ajili ya kusoma vitabu.

Hitimisho

Naamini baada ya kusoma makala hii hutoshindwa tena kusoma vitabu kwani mbinu hizi zitakuwezesha kusoma vitabu hata kama una shughuli nyingi.

Ni muhimu sana kuweka malengo, kuwa na nidhamu ya matumizi ya muda ili usikose tunu inayopatikana kwenye vitabu.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *