img

Pongezi kwa Rais Magufuli kwa ushindi wa kishindo

November 5, 2020

Na MAHESH SHAH


TANZANIA imekamilisha Uchaguzi Mkuu, hatua ambayo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya demokrasia.

Pongezi nyingi kwa Rais mteule, Dk. John Magufuli ambaye ameshinda kwa kishindo.

Dk. Magufuli ameshinda kwa kupata kura 12,516,252 ambayo ni asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa.

Tundu Lissu kutoka chama cha upinzani cha Chadema ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,933,271 ya kura zote zilizopigwa.

Katika uchaguzi huo, jumla ya Watanzania  15,91950 walipiga kura hizo wakati waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 29,754,699; hii ni kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“John Magufuli ndio mshindi wa uchaguzi, amepata kura nyingi halali kuliko wagombea wengine, amechaguliwa kuwa Rais wa Tanzania na Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais,” ilikuwa ni kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, wakati akitangaza matokeo hayo siku mbili baada ya uchaguzi.

Ni rasmi sasa mgombea wa chama tawala nchini ambacho ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amechaguliwa tena kwa ushindi wa kishindo.

Pamoja na kuwapo kwa dosari za hapa na pale, ni bayana kuwa kwa matokeo hayo Tanzania imekamilisha zoezi hilo muhimu na sasa ni wakati wa kurejea pamoja kwa ajili ya kuujenga uchumi wetu ambao tayari umeanza kuchanua.

Hii ina maana kwamba Rais mteule, Dk. Magufuli anayetarajiwa kuapishwa leo Alhamisi ya Novemba 5, katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, anakwenda kumalizia kazi yake aliyoianza Novemba 5 mwaka 2015 ya kuujenga uchumi wa Tanzania.

Katika kipindi kifupi cha miaka mitano ya uongozi wake, tayari Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye uchumi ikiwa ni sambamba na kufanikiwa kuingia kwenye uchumi wa kati.

Ni bayana kwamba ushindi wa CCM umetokana na juhudi kubwa za Rais kwenye kulipigania taifa hili kupata maendeleo, ikiwa ni mafanikio ya miradi mingi chini ya uongozi wake, Watanzania wameona kazi kubwa aliyofanya rais ndani ya miaka mitano iliyopita.

Usemi uliotumika mara kwa mara wakati wa kampeni ya urais kuwa, ‘Magufuli ndio tumaini letu’ na ni Rais wa wanyonge, wapiga kura hao ndio aliofanikisha ushindi mkubwa kwa Rais Magufuli.

Utendaji aliyoonyesha ndani ya miaka mitano ilikuwa tumaini tosha kwa Watanzania kumchagua tena kipindi kingine cha miaka mitano.

Watanzania wameonesha upendo mkubwa kwa Rais Magufuli kwa kumchagua tena, ushindi hivyo ushindi wake ni ushindi wetu sote, itoshe kusema almasi yetu tuliyoichagua imemeremeta.

Tanzania ilikuwa inahitaji Rais anayependa kufanya kazi na tumempata ndio maana hata ilani ya CCM ya 2020-25 ni kubwa zaidi kuliko ya 2015-20 hii ni kutokana na Rais anataka maendeleo na yuko tayari kufanya kazi kwa kutuondolea changamoto zote.

Itoshe kusema 2025 taifa litakua pazuri zaidi, rais yeyote anayeweka mbele maslahi ya taifa, rais huyo hawezi kukosa upendo kutoka kwa wananchi wake na wala hawezi kuangushwa.

Chama kilisema kasi zaidi, kazi zaidi ndio maana hata katika kura za maoni za ubunge CCM kilipendekeza viongozi vijana, ili kuongeza spidi ya kazi katika taifa letu.

Rais anaamini urais sio cheo tu bali ni majukumu ya kuliongoza taifa katika mwelekeo wa maendeleo.

Uchaguzi umekwisha sasa ni wakati wa kuungana, tuweke utaifa kipao mbele tuungane sote kuwa kitu kimoja na nguvu zetu tuelekeze kwenye maendeleo ya Taifa hili ndio la faida kwetu sote.

Kwani siasa tumezimaliza katika kipindi cha takribani miezi mitatu, ambapo tulishuhudia kila chama kikifanya siasa kupitia majukwaa ya kampeni zenye mtifuano mkali baina ya wagombea wa nafasi ya urais na ngazi mbalimbali nchini.

Ilikuwa bayana kwamba CCM ilikuwa na sera thabiti ambazo zilikuwa kwenye ilani yake kikijibunia maendeleo yaliyofanyika ndani ya miaka mitano kwa kauli mbiu “Tumetekeleza kwa kishindo- Tunasonga mbele kwa pamoja”.

Pamoja na ushirndani mkali kutoka kwa Chadema ambazo zililenga kauli mbinu ya” Haki, Uhuru na Maendeleo ya Watu”.

Kimkakati,Chadema kilitumia muda mwingi kukosoa utekelezaji wa mambo kadhaa katika utawala uliopita na kujinasibu kutekeleza misingi ya Haki, Uhuru na kuwaletea wananchi maendeleo yanayoakisi mahitaji yao halisi.

Hivyo ni dhahiri kuwa Watanzania walipima na kutafakari kwa kina utashi wa Rais Magufuli wa  kisiasa kwa jinsi alivyoweza kutekeleza kwa mafanikio makubwa ya Ilani ya uchaguzi wa chama chake kuanzia nidhamu maofisni,udhibiti wa raslimali za nchi, ujenzi wa miundo mbinu ya barabara, madaraja,meli, upanuzi wa bandari,maji, elimu, afya, upanuzi wa viwanja vya ndege, ununuzi wa ndege, umeme vijijni kuongeza kasi ya ukusanyaji kodi,watumishi wa umma kupunguzia kodi kulingana na kipato cha mishahara ijulikanayo kama PAYE na maeneo mengine ya kiuchumi.

Aidha,upo ushahidi wa wazi wa kitakwimu kuhusu jitihada hizi na ambazo haziwezi kubezwa.

Kipimo kikubwa cha mafanikio ni pamoja na Tanzania kuingia kwenye Uchumi wa Kati (middle income country) kwa mujibu wa taarifa ya  Benki ya Dunia iliyotolewa tarehe 1 July 2020. Aidha, Shirika la Fedha Duniani(2017),World Economic Forum(2018)zote zimeonyesha wazi kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi hivyo kuwa nchi ya 28 kati ya 186 pamoja na mambo mengine imeweza kusimamia kwa ufanisi matumizi ya fedha za umma.Aidha, Takwimu zilizotolewa kwenye utafiti wa African Global Survey mwaka 2019 zinasema asilimia 72 ya wananchi wanaimini serikali yao kwa jinsi inavyopambana na rushwa na ufisadi ukilinganisha na asilimia 13 mwaka 2015 wakati serikali hii inaingia madarakani.

Hivyo imani ya wananchi kwa serikali yao imeogezeka sana.

Jambo la pili ambalo liliwashawishi Watanzania wengi wamuone Rais Magufuri kuwa anafaa kuchaguliwa kuongoza tena ni staili yake ya uongozi wa  kipekee na uwezo wake wa kuona mbali,uchapaji kazi, uzalendo na  ujasiri wa kufanya maamuzi magumu na kuyasimamia ili mradi yana maslahi ya taifa. Ipo mifano kuthibitisha hili kama vile ujenzi wa bwawa la umeme la Julius Nyerere kwa kutumia fedha za ndani na kuwa ujenzi wa  bwawa hilo lilipingwa na mataifa makubwa, kuhamishia makao makuu serikali Dodoma,ujenzi wa SGR na suala la ugonjwa wa Korona kwa jinsi alivyolishughulikia kwa ushupavu na ujasiri mkubwa.

Pasipo shaka uongozi wa aina hii ni wa kutukuka na huwezi kuchelea kuupigia kura ya ndiyo.

Kimsingi, yako mengi yaliyofanyika kipindi hiki kifupi cha miaka mitano hivyo Watanzania walikuwa na kila sababu ya kumchagua.

Kwani wananchi wengi wanakiri kuhusu mafanikio haya.

Nimalizie kwa kuwaomba Watanzania wote tushirikiane na rais wetu kujenga uchumi wetu kwa manufaa ya Tanzania kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0682 554 444

The post Pongezi kwa Rais Magufuli kwa ushindi wa kishindo appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *