img

Wajibu wa wadau wa uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu

October 15, 2020

NA ANNA HENGA


KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inampa kila raia wa Tanzania haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi katika Ibara ya 21(i).

Kwa miaka mingi wadau mbalimbali wa uchaguzi wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kulinda demokrasia na utawala bora nchini Tanzania.

Mojawapo ya shughuli wanazofanya wadau wa uchaguzi ni pamoja na kutoa elimu ya mpiga kura, kutoa elimu ya uraia pamoja na kuwajengea uwezo wananchi katika ngazi mbalimbali kuhusu umuhimu wa ushiriki wao katika masuala ya utawala wa nchi.

WADAU WA UCHAGUZI NI AKINA NANI?

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwafahamu wadau wa uchaguzi hapa nchini kwa kuwa kila mdau wa uchaguzi ana umuhimu mkubwa sana wakati huu wa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani hapa nchini.

Tunapozungumzia wadau wa uchaguzi mara nyingi tunamaanisha wananchi wenyewe, vyombo vya habari, Serikali na vyombo vyake, Mahakama, Tume ya Uchaguzi, vyama vya siasa pamoja na asasi mbalimbali za kiraia.

Ninayo hamasa kubwa kuweza kuzungumzia wadau wa uchaguzi pamoja na michango yao katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea kuwachagua wawakilishi watakaoongoza na kusimamia rasilimali za nchi yetu katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika nchi ya kidemokrasia tofauti na nchi zenye mfumo wa kifalme, uongozi unapatikana kutokana na ridhaa ya wananchi kupitia uchaguzi. Ridhaa hiyo hutolewa kwa watu wachache ambao watakuwa wanawakilisha sauti ya wengi na maamuzi kwa niaba ya wananchi wenyewe.

Dhana ya uchaguzi wa viongozi au wawakilishi itapoteza maana endapo kutakuwa na uwezekano wa kiongozi kupatikana bila kupitia mchakato wa uchaguzi ulio wazi, haki, sawa na wa kuaminika.

Pia endapo taasisi zinazosimamia uchaguzi zitabeba mamlaka ya kupitisha watu wasiochaguliwa kuwa viongozi hata kama uchaguzi haujafanyika dhana ya umuhimu wa uchaguzi itapoteza maana.

Kwa maana hiyo wananchi wenyewe ni moja kati ya wadau muhimu wa uchaguzi hapa nchini pamoja na nchi nyingine zenye mfumo wa kidemokrasia. Kuna umuhimu mkubwa sana wa wananchi kujitambua na kutafuta maarifa muhimu na kuelewa kiundani kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi.

Moja kati ya wajibu muhimu wa wananchi katika nyakati za uchaguzi ni kujiandikisha na kuhakiki taaarifa zao za mpigakura katika daftari la kudumu la mpiga kura na kushiriki kupiga kura.

VYOMBO VYA HABARI

Kifungu cha 18 cha Katiba ya Tanzania ya Mwaka 1997 kinaeleza kuwa: Kila mtu (a) ana haki ya kutoa maoni na kueleza mawazo yake; (b) ana haki ya kutafuta, kupata na/au kutoa taarifa bila kujali mipaka ya kitaifa;(c) ana uhuru wa kuwasiliana na uhuru wa kulindwa dhidi ya kuingiliwa mawasiliano yake; na (d) ana haki ya kupewa habari wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu ya kimaisha na shughuli za watu na pia kuhusu masuala muhimu kwenye jamii.

Kama ambavyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatoa uhuru wa kupewa habari wakati wote kuhusu matukio muhimu ya kimaisha ni dhahiri kwamba vyombo vya habari ni mdau mkubwa wa uchaguzi. Vyombo vya habari mara zote vimekuwa na mchango mkubwa katika kutoa taarifa mbalimbali kuhusu masuala ya uchaguzi ikiwemo kampeni za uchaguzi.

Zipo taarifa mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi ambazo kwa kiasi kikubwa ni lazima vyombo vya habari vishiriki kwa kiasi kikubwa kufikisha hizo taarifa kwa wananchi.

Kwa mfano katika uzinduzi wa kampeni za kisiasa katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu, vyombo vya habari vilirusha matangazo ya moja kwa moja kuutaarifu uma kuhusu matukio hayo muhimu.

Ingawa vyombo vya habari vinapitia changamoto mbalimbali kama vile sheria kandamizi lakini vinaendelea kutekeleza majukumu yake kama mdau wa uchaguzi kutoa taarifa mbalimbali kuhusua uchaguzi.

Zipo sheria nyingi zinazokandamiza vyombo vya habari na hivyo kupunguza uwezekano wa wananchi kupata taarifa mbalimbali zinazohusu uchaguzi nchini Tanzania.

Moja kati ya sheria ambazo zinaendelea kuminya uhuru wa kujieleza kupitia baadhi ya vifungu vyake ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Upatikanaji Habari ya mwaka 2016 na Kanuni za Maudhui ya Mtandao. Sheria hizi hazina mchango chanya katika upatikanaji wa taarifa mbalimbali za uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28  mwaka huu.

Tangu nchi ya Tanzania irudi katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 serikali imekuwa na mchango mkubwa sana katika hukakikisha michakato ya uchaguzi zinakuwa Huru na za Haki.

Hata katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu serikali kupitia vyombo vyake kama vile polisi pamoja na Takukuru, ina wajibu wa kuhakikisha amani na utulivu vinatawala kipindi chote cha uchaguzi.

Kwa kuanza Jeshi la polisi lina majukumu makubwa yafuatayo katika uchaguzi; Jukumu la Ulinzi maafisa wa polisi wanatakiwa sio tu kutoegemea upande wowote na kutompendelea mtu yeyote bali wanatakiwa kuonekana kutoegemea upande wowote na kutompendelea mtu yeyote kwa misingi ya aina yoyote ile kama vile umri, jinsia, ulemavu, hali ya kijamii au kiuchumi, maoni ya kisiasa, kabila, dini au sababu nyingine zozote zile.

Kuzingatia Usawa; Katika kipindi hiki cha uchaguzi hasa wakati huu wa kampeni Maafisa wa jeshi la polisi wanapaswa kuwa waangalifu jinsi wanavyoshughulikia matukio mbalimbali hususan mivutano baina ya vyama vya siasa.

Maofisa wa polisi wanapaswa kuepuka matendo yanayoweza kutafsiriwa kwamba ni ya upendeleo, yasiyozingatia usawa, uonevu na yenye shinikizo la kisiasa. Katika wakati wa uchaguzi maofisa wa polisi hawapaswi kutumia nguvu kubwa kupita kiasi.

Kwa masikitiko makubwa tumeshuhudia matumizi makubwa ya nguvu kama vile mabomu ya machozi na kurushwa kwa risasi katika kipindi cha kampeni za uchaguzi huu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu. Kwa kawaida katika kipindi muhimu kama hiki cha uchaguzi nguvu inaweza kutumika pale tu ambapo ni lazima na ikiwa itatumika kuwe na uwiano na kosa lililotendwa na si vinginevyo.

Matumizi ya nguvu kupita kiasi hususan katika kipindi cha uchaguzi na hasa siku ya kupiga kura ni jambo linaloweza kutafsiriwa vibaya na wananchi ndani ya nchi pamoja na jamii ya kimataifa.

MAHAKAMA

Kama mdau mojawapo wa uchaguzi, Mahakama ina mchango mkubwa sana katika uchaguzi mkuu. Moja kati ya jukumu muhimu la mahakama wakati wa uchaguzi mkuu ni kuamua mashauri mbalimbali yanayohusu uchaguzi pale yanapojitokeza kwa kuhakikisha usawa mbele ya sheria kwa vyama vyote au mtu binafsi.

Hapa nchini kwa kawaida kuna mahakama za ngazi mbalimbali mahakama za juu zinapokea rufaa dhidi ya kesi za ngazi za chini na mahakama ya rufaa. Yote kwa yote mahakama ina mchango mkubwa katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa kufuata mfumo wa kidemokrasia.

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka katika tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mwaka1993 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilianzishwa chini ya Ibara ya 74 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.Kwa mujibu wa Ibara ya 74(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Kifungu cha 4(4) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Na. 1 ya1985), Mkurugenzi wa Uchaguzi ndiye Katibu wa Tume ambaye pia huteuliwa na Rais.

Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa mdau mkubwa wa uchaguzi, mratibu mkuu na msimamizi mkuu wa shughuli zote za uchaguzi.Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama mratibu mkuu wa uchaguzi tayari wameshafanya mambo muhimu kama vile; maandalizi ya uchaguzi ambayo yamejumuisha michakato mbalimbali ikiwemo uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura, uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kuandaa kanuni, maadili ya uchaguzi, maelekezo mbalimbali, kuandaa bajeti ya uchaguzi, kuboresha mifumo ya Tehama na ununuzi wa vifaa vya uchaguzi.

VYAMA VYA SIASA

Vyama vya siasa hapa nchini ndio mdau mama wa uchaguzi tangu kuanziashwa kwa vyama vingi mwaka 1992. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ndio yenye jukumu la ufuatiliaji wa mienendo ya vyama vya siasa kutokana na kuwa na mamlaka ya kisheria ya kusajili na kufuta vyama vya siasa.

Vyama vya siasa 15 vimefanikiwa kupata mgombea wa kiti cha Rais katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika ifikapo Oktoba 28 mwaka huu. Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na wagombea wengi wa kiti cha Rais na kwa mujibu wa taarifa kutoka katika tovuti rasmi ya Msajili wa Vyama vya Siasa hadi sasa vyama vyenye usajili wa kudumu ni 19 na chama kimoja kina usajili wa muda na maombi ya vyama 16 bado yanafanyiwa upembuzi.

ASASI ZA KIRAIA

Asasi za kiraia zimekuwa mdau mkubwa  sana wa uchaguzi hapa nchini na wamekuwa wakishiriana na wadau wengine wa uchaguzi kama vile Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu unafanyika katika misingi ya kidemokrasia.

Katika uchaguzi mkuu huu unaotarajia kufanyika Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa vibali kwa Asasi za Kiraia ili ziweze kushiriki katika utoaji wa Elimu ya Mpiga kura katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kuwapatia mwongozo wa utoaji elimu. Ushirikiano kati ya wadau hawa una umuhimu mkubwa sana kwa kuwa wote wanalenga kufanikisha Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa mwaka 2020.

Nikiwa kama mdau wa haki za binadamu naamini katika haki ya kiraia na kwamba kila raia ana haki ya kushiriki katika siasa  na kupiga kura .Kushiriki katika kupiga kura ndio msingi wa kupatikana kwa uongozi bora katika nchi ya Tanzania. Kwahiyo napenda kutoa rai kwa serikali, wananchi pamoja na asasi za kiraia nchini Tanzania kushirikiana ili kuweza kupata viongozi bora kupitia siasa safi.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

The post Wajibu wa wadau wa uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *