img

Siku ya Mtoto wa Kike Duniani iwe kichocheo kukuza utu, heshima ya wanawake

October 15, 2020

NA DK. HELLEN KIJO BISIMBA


OKTOBA 11 ya kila mwaka ni Siku ya mtoto wa Kike Duniani. Mwaka huu siku hii iliangukia Jumapili na pamekuwa na shughuli mbalimbali katika kuiadhimisha.

Nilitafakari sana maana ya siku hii na iwapo ina faida yoyote kuwepo kwake. Tafakari hii ilikuja kutokana na mwenendo wa jinsi wanawake na watoto wa kike hadi sasa wanavyochukuliwa katika jamii yetu.

Hasa ukiangalia matamko mbalimbali ya viongozi na hasa kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu na katika mambo mengi yanayowakuta wanawake na mabinti katika jamii yetu.

Mwaka 1994 nilishiriki katika mkutano wa wanawake wa Afrika kuandaa mkutano wa Wanawake Kimataifa uliokuja kufanyika Beijing mwaka 1995. Mkutano huo ulifanyikia Dakar Senegal na huko tulikuwa na mjadala mkubwa iwapo tuweke suala la mtoto wa kike katika maazimio ya haki za wanawake.

Wapo walioona itakuwa ni kuchanganya masuala ya watoto katika ajenda yetu ya wanawake. lakini sauti iliyozidi ni ile iliyotamka kuwa mwanamke huanza akiwa mtoto wa kike. Tukiweza kuijenga haki na heshima ya mtoto wa kike akifikia kuwa mwanamke tayari ana vazi la haki na heshima.

Tukisubiri hadi awe mwanamke ndio tuanze kuangalia haki hizo atakuwa amekwisha kujeruhika na hata kuathirika. Ilikubalika kuibeba ajenda hiyo na tulipofika Beijing ilikubalika na ndio maana Tamko la Beijing limekuwa Tamko la kwanza la Umoja wa Mataifa kuweka bayana haki za mtoto wa kike likiwa ni lengo mkakati la kumi na mbili.

Mwaka 2011 Desemba 19 Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio namba 66/170  lililoitaja Oktoba 11 kuwa ni siku ya mtoto wa kike ulimwenguni kwa kutambua changamoto mahususi zinazomkuta mtoto wa kike katika ulimwengu huu.

Tangu mwaka huo siku hii imekuwa ikiadhimishwa kote ulimwenguni. Mwaka huu kauli mbiu ilikuwa ‘Sauti Yangu, Usawa Wetu Ujao’. Mwaka huu pia imeanzishwa kampeni kubwa mtambuka inayoitwa Kizazi cha Usawa ambayo ni harakati thabiti kuelekea usawa wa kiijinsia.

Mambo ya kuzingatia ikiwa ni pamoja na haki ya maisha salama, elimu na afya bora na si kwa mabinti tu bali hadi kwa wanawake.  Inasemekana watoto wa kike wakisaidiwa katika umri huo watakuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko katika jamii ya heshima na haki kwa mwanamke.

Yapo madai ya watoto wa kike kwa jamii. Wanahitaji kuishi wakiwa huru dhidi ya ukatili wa kijinsia, mila zinazowanyanyasa na kuwakandamiza na ukimwi. Wanataka  kujifunza stadi mpya za maisha kuelekea kesho waitakayo, huku wakiongoza kuwa kizazi cha wanaharakati wanaohimiza mabadiliko ya kijamii.

Haya ni muhimu sana kwenye jamii. Kwa miaka ambayo tumeanza kuzungumzia haki na usawa wa wanawake katika jamii usingetegemea kuwa katika kipindi hiki ungeweza kukutana na mambo ya kibaguzi dhidi ya wanawake au watoto wa kike au unyanyasaji na ukatili ambao tunausikia kila uchao.

Kuna yale watu wote wanayokubaliana kuwa si sawa na kuna yale wengine huona hayana madhara. Tunaposikia kuna mume kamkata mke wake mkono kama tulivyosikia hivi karibuni huko Arusha karibu kila mtu anasikitika, kulaani na kusema ‘huyu mwanamume katili sana’. Tukisikia mtu akimtukana mwanamke au akiutukana uanawake wachache wanaona ni tatizo wakisema ‘hilo si tusi tu?’ Haya mambo yanahusiana, maana kumtusi mtu ni kuonyesha kutomheshimu na kumdharau na ikizidi ndio unaweza kuinua mkono kumpiga kofi na ikizidi zaidi hata kumkata panga.

Tulipomsikia Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi akimtazama mganga (Daktari) katika  halmashauri hiyo na kutaka kujua iwapo ameolewa ili ikiwezekana yeye amuoe, watu wengine walisema huo ulikuwa ni utani.

Wengine hatukukubaliana na utani wa aina hiyo, kwani yule mganga wa kike alikuwa kazini na alikuwa na sifa zaidi ya kuangaliwa kama chombo cha kuolewa. Yule mkuu alichofanya ilikuwa kumvua udaktari na kumvika uanawake wa kuolewa hiyo kwa mtazamo wa kijinsia ni dharau ya hali ya juu.

Katika kampeni zinazoendelea tulimsikia mgombea urais kwa tiketi ya CCM ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli akimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Temeke, nilitegemea kusikia wasifu wa mgombea yule na uwezo wake hadi chama chake kikamuamini kuwa mgombea.

Lakini badala yake alielezewa kuwa ni mwanamke mweupe ambaye rais anataka achaguliwe ili yeye rais akiendelea kuwa rais aweze kumsikiliza kwa urahisi kwa kuwa ni mweupe.

Mjadala mkubwa uliibuka katika tamko hili wengine wakisema ulikuwa utani. Hatutegemei utani katika mambo ya muhimu kama hayo, tunataka mtu aelezewe kwa sifa zake si kwa rangi yake na kwa vile ni mwanamke watu wanaanza kufikiria mambo mengine nje ya nafasi nyeti hiyo ya ubunge.

Baada ya hapo nimemsikia mgombea mmoja akisema anapeleka malalamiko kwenye tume ya maadili dhidi ya mgombea katika jimbo analogombea aliyediriki kutamka kuwa huyo kwa vile ni mwanamke, hataweza kuwatumikia wananchi wakati akiwa kwenye hedhi. Hii ni dhihaka na fedheha kwa watoto wa kike na wanawake wote akiwemo mama wa huyo mwanamume aliyetamka hivyo.

Tunapoangalia kwa muktadha mpana tunaona kuwa maneno ya aina hii yanawalenga zaidi wanawake ili kuwadhoofisha na kuwafanya wasiangaliwe kwa uwezo walionao na kwa sifa walizonazo kwa kuwa jamii hasa ya wanaume bado ina mgogoro wa kutaka kuwaona wanawake si sawa na wao.

Ningetamani sana kuwa na mjadala na hawa wanaume watatu niliowataja hapo juu kujua hasa walipokuwa wanatoa kauli hizo walizipima na kujua ukubwa wa madhara ya kauli kama hizo? Huyu mmoja ameweza kufikiri na kuamua kupeleka malalamiko.

Kwanza ni kwa vile amesemwa na mpinzani wake wakati wa uchaguzi. Vinginevyo ingeweza kunyamaziwa tu na hata sasa wapo watakaomwambia asijihangaishe hilo ni dogo tu. Yule aliyesemewa na mkuu wa mkoa alionesha kuinama na kucheka tu kwa vile aliyemnenea ni mkuu wake wa kazi na jamii iliyozunguka pale walikuwa wanacheka hata angeona vibaya na kutaka kufuatilia angeweza kuambiwa aache kabisa. Huyu aliyekuwa ananadiwa yeye aliinama kuonyesha shukrani kwa mkuu wake na hata sasa msomaji anaweza kuwa ananishangaa kuwa, ‘kwani kuna tatizo gani?’

Hapo ndipo tatizo linapoanzia kiasi cha kutakiwa kuwa na Siku ya Mtoto wa Kike. Siku moja mtu tunayefahamiana vizuri kabisa alifika nyumbani akamkuta wajukuu akamuinua mmoja mdogo mvulana na kumrusharusha juu.

Alipotaka kumchukua mjukuu wangu wa kike ili afanye hivyo, huyo mjukuu wa miaka mitano alimwambia ‘sitaki kubebwa na wewe, tumeambiwa shuleni tusibebwebebwe na watu tusiowajua’.

Watoto wa kike wakianza kujitambua tangu wadogo wakikataa utani usio na tija kama ‘mchumba’ n.k hapo heshima yao itaanza kuonekana na kusimama ndani ya jamii na watakuwa wakiwa katika hali hiyo na jamii haitapata nafasi ya kuwadhihaki kwa maneno ya kuwashusha wakidhani wanawasifu.

Lugha za kibaguzi na kiudhalilishaji ndizo huzaa ukatili wa kijinsia, ubaguzi na kutothamini wanawake kuanzia wakiwa watoto wa kike. Hii siku ya mtoto wa kike iwe siku yakuyaanika yale yote yanayotweza utu wa mtoto wa kike na mwanamke na kuinua yale yote yaliyo matamanio ya kuinua utu na heshima ya mtoto wa kike akiwa ni mwanamke ajaye.

Hili ni la wote kuanzia wazazi, walimu, marafiki, majirani, viongozi wa ngazi zote. Watoto wa kike wajenge harakati za kuwakomboa watoto wa kiume dhidi ya hali hizi kwani nao wakikua katika hali hizo ndio hujitokeza kuwa wanaume wabaguzi na wanyanyasaji kama tunavyoona katika jamii zetu. Kila mtu anastahili heshima.

0713 337 240

The post Siku ya Mtoto wa Kike Duniani iwe kichocheo kukuza utu, heshima ya wanawake appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *