img

Serikali ijayo kupunguza msongamano wa watu magerezani?

October 15, 2020

NA JAVIUS KAIJAGE


TUNAPOELEKEA katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu, kupitia katika mikutano ya kampeni za vyama vya kisiasa tumekuwa tukisikia sera tofauti katika ilani za vyama husika kama njia mojawapo ya kutufanya tuwe na uamuzi kabla na wakati wa kupiga kura.

Kupitia mikutano hiyo wagombea wamekuwa wakitajitahidi kuzungumzia masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Ajabu ukifuatilia kwa karibu katika kampeni hizo ambazo kimsingi ziko katika siku za lala salama, wagombea wamekuwa na kigugumizi kuwazungumzia wananchi wao ambao wako magerezani wakiteseka kwa kukosa uhuru wao.

Kimsingi magereza yetu kutokana na sababu mbalimbali yamejikuta yakiendelea kuwa na msongamano wa watu licha ya Rais Dk. John Magufuli kujitahidi kupunguza watu hao katika kipindi chake kifupi cha miaka mitano ya uongozi wake.

Akiwa katika mwendelezo wake wa  kutembelea Gereza Kuu Butimba, Msajili wa Mahakama Kuu katika kanda ya Mwanza Frank Mahimbali, Oktoba 2 mwaka huu alifanya ziara yake katika gereza hilo kwa lengo la kuzungumza na  wafungwa/mahabusu kama njia mojawapo ya kutatua changamoto zilizopo.

Katika kuzungumza na wafungwa/mahabusu Msajili alianza kwa kupokea risala ya mahabusu ambayo kimsingi ndani mwake ilielezea kero mbalimbali zinazowakabili zikiwemo kucheleweshwa vikao, kuachiwa huru na kukamatwa tena, watoto wadogo kuendelea kuletwa magerezani n.k.

Akijibu hoja za kwenye risala hiyo pamoja na malalamiko mengine mbalimbali yaliyotolewa na mahabusu hao, Msajili alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo ni ufinyu wa bajeti ya kuandaa vikao na wala si kwamba mahakama zinatamani wao waendelee kukaa magerezani.

Aidha Msajili huyo aliendelea kuwaambia mahabusu ya kuwa changamoto nyingine ni uwepo wa kesi nyingi katika kanda hii kwani takwimu zinaonyesha kuwa kuna kesi zipatazo 320 ambazo zinahitaji kufanyika kwa vikao vipatavyo 20.

Kimsingi changamoto hii ya ufinyu wa bajeti kwa ajili ya kuendeshea shughuli za kimahakama imeendelea kupelekea msongamano mkubwa wa watu magerezani hususan mahabusu.

Awali Mkuu wa Gereza Kuu Butimba, Afande Kamishna Msaidizi wa Magereza Benard Chiwanyi Mugabu akimkaribisha  Msajili huyo katika himaya yake, alimpa  taarifa iliyoonyesha kuwa  palikuwepo na idadi ya wafungwa 577  na mahabusu 799 na hivyo kufanya jumla ya wote kuwa 1376 katika  siku hiyo.

Ikumbukwe kuwa Gereza Kuu Butimba lilivyojengwa lina uwezo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu 924, hivyo kwa sasa kuwa na idadi ya watu 1376 maana yake kuna ziada ya watu 452 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 48.9.

Ongezeko hili la wafungwa na mahabusu katika Gereza Kuu Butimba linaweza kuwa linaakisi hali ya msongamano katika magereza yetu hapa nchini hususani yale magereza makubwa yenye kawaida ya kuhifadhi mahabusu wenye kesi kubwa.

Suala la ufinyu wa bajeti kuendelea kuwa kisingizio cha kuwaweka watu magerezani lina madhara makubwa katika taifa lenye   malengo ya kuwa nchi ya viwanda ili kujenga uchumi imara.

Nasema watu kuendelea kuwa magerezani kutokana na ufinyo wa bajeti kuna madhara kiuchumi kwani kwa vyovyote vile serikali itaendelea kuwajibika kuwahudumia watu hao katika mahitaji ya chakula, mavazi na matibabu bila kusahau nguvu kubwa ya kuajili na kuwalipa mishahara watumishi kwa maana ya maafisa na askari magereza.

Ndiyo serikali ya awamu ya tano imekuja na mkakati kabambe wa kuhakikisha magereza yote nchini yanajitegemea kwa kila nyanja ikiwemo kuwalisha walioko magerezani lakini pia mkakati huo utaendelea kuwa na kikwazo kikubwa katika kutimiza malengo.

Kikwazo kinakuja kutokana na kwamba katika sheria za nchi zilizopo siyo watu wote waliomo magerezani hutakiwa kufanya kazi kwa lengo la kutimiza mkakati wa kujitegemea.

Katika miongoni mwa makala niliyowahi kuandika katika gazeti hili yenye kichwa: ‘‘Simbachawene kukabiliana na changamoto za Magereza?’’ nilionyesha  vikwazo katika Jeshi la Magereza kujitegemea.

Makala hiyo niliyoiandaa mara baada ya George Simbachawene kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, nilidadavua changamoto ambazo atakumbana nazo ikiwemo Jeshi la Magereza kujitegemea ili kutimiza ndoto za Rais Magufuli.

Kuanzia katika aya ya 14 ya makala hiyo  niliainisha baadhi ya changamoto hizo kwamba katika Magereza yenye zaidi ya wafungwa  wapatao 13,000 kipindi Simbachawene akiapishwa  si kila mfungwa angeweza kufanya kazi kutokana na  taratibu na sheria zilizopo.

Kuna wafungwa waliohukumiwa kifo lakini adhabu zao hazitekelezwi na hawa licha ya kutojulikana wawekwe upande gani aidha  wabadilishiwe adhabu kwa kupewa kifungo cha maisha ili wafanye kazi au adhabu yao itekelezwe ili kupunguza bajeti, lakini  wameendelea kula bure chakula bila kuelewa hatima yao.

Changamoto nyingine ni mifumo ya sheria ambazo hutoa vifungo virefu visivyoleta tumaini, kwa mfano hivi sasa katika magereza wapo wafungwa wengi wa vifungo vya maisha na wengine wa miaka 30 na kuendelea.

Kimsingi adhabu za namna hii kisaikolojia humfanya mhusika kukata tamaa na hivyo kutofanya kazi kwa kujituma na wakati mwingine kama hakuna ulinzi imara mfungwa anaweza kujitoa mhanga kwa kutoroka au kufanya lolote ikiwemo kuhatarisha usalama wa askari anayemchunga.

Serikali yetu haina utaratibu wa kutoa mitaji au pesa za kujikimu kwa mfungwa/wafungwa wanaomaliza vifungo vyao na hivyo wahusika kujihisi wanafanya kazi si katika kujituma kama binadamu bali ni kwa sababu wanatumikia adhabu.

Sheria zetu bado hazijaruhusu mahabusu ambao hawajahukumiwa, kufanya kazi pindi wawamo magerezani wakisubiri mashauri yao na hivyo kuendelea kuwa mzigo kwa magereza kwani wao hulala na kula bure na inasemekana katika baadhi ya Magereza hapa nchini mahabusu ni wengi kuliko wafungwa mfano mmojawapo ni Gereza Kuu Butumba lenye wafungwa 577 ilihali mahabusu wakiwa 799.

Ni ukweli usiopingika suala la mahabusu kuendelea kuwa wengi magerezani huku taratibu na sheria zilizopo vikiwa haviwaruhusu wao kufanya kazi,  hakika ni mzigo kwa serikali na ni mzigo kwa wasimamizi wa magereza kwa maana ya maafisa na askari.

Ni kweli kuna changamoto ya bajeti na suala la Usalama wa nchi ni muhimu kwani huwezi kuwaachia mahabusu hawa kihorera bila kupata uhakika wa visababishi vya tuhuma zao lakini kuna kila sababu kupunguza kwa kutoa hukumu haraka  ili wahusika watumikie adhabu zao za vifungo kwa kufanya  kazi za uzalishaji mali au kuwaachia huru hususan wenye kesi ambazo hazina mbele wala nyuma.

Si haki hata kidogo magereza yetu kuendelea kuwa na mahabusu wengi ambao kimsingi kesi zao zinaweza  kudhaminika.

Si haki hata kidogo kuendelea kuwashikilia magerezani mahabusu ambao ni wahamiaji haramu ilihali pangefanyika utaratibu wa haraka wakasafirishwa na kurudi katika nchi zao.

Si haki hata kidogo kuendelea kuwashikiria mahabusu watoto ambao kimsingi  kesi zao zinaweza kuendelea kusikilizwa wakiwa chini ya uangalizi maalumu huko nje.

Si haki hata kidogo mahabusu kuendelea kuwa magerezani kwa muda mrefu mpaka miaka mitano, kumi na zaidi ya hapo kwa kisingizio cha upelelezi bado unaendelea.

Yote kwa yote serikali ijayo isipoliangalia kwa jicho pevu suala la msongamano magerezani ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na ongezeko la mahabusu wasiofanya kazi, hakika uchumi wa nchi unaweza kujeruhika kwa namna moja au nyingine.

Email:  HYPERLINK “mailto:javiusikaijage@yahoo.com” javiusikaijage@yahoo.com, Simu: 0756521119

The post Serikali ijayo kupunguza msongamano wa watu magerezani? appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *