img

MIAKA 21 BILA NYERERE Alikubali, kuheshimu kanuni ya DMU 

October 15, 2020

NA ALOYCE NDELEIO


JANA Oktoba 14 ilikuwa ni kumbukizi ya miaka 21 tangu  Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipoaga dunia katika Hospitali ya St. Thomas nchini Uingereza alikokuwa akipatiwa matibabu.

Yapo mambo mengi ambayo yanamwelezea Baba wa Taifa na ambayo huenda mengine yamefichika machoni mwa jamii au baadhi ya wanajamii wanashindwa kuyatambua kutokana na kufichika kwake.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kanuni ambazo zilikuwa zinasimamia masilahi ya jamii na kwamba ukiukaji wake ilikuwa ni kuidhalilisha jamii na hata kudhoofisha ustawi wake.

Kwa kutambua utajiri wa rasilimali zilizokuwepo nchini alitumia na kuiheshimu kanuni ya ukomo wa kutumia ili manufaa yaweze kuwafikia wote.

Kanuni hiyo ya ukomo wa kutumia  kwa lugha ya Kiingereza Diminishing Marginal Utility (DMU) ni tahadharisho la kuondokana na ulafi na kwamba kutumia kwa kadri ni busara zaidi.

Jambo lililo wazi linaloonesha kuwa alikuwa na ukomo wa kutumia ni kule kuwa kiongozi ambaye hakujilimbikizia mali kwani kipindi anaondoka madarakani busara ilitumiwa na vyombo vya dola kwa kumjengea nyumba ambayo inamfaa mtu aliyepigania uhuru wa nchi.

Tofauti na viongozi wengine ambao wanajulikana kujilimbikizia rasilimali fedha nje ya nchi hakufanya hivyo na hata aliweza kufikia hatua ya kupunguza mshahara wake akisema, “Mshahara wangu mnajua ni kiasi gani?… ni mkubwa mno… mshahara wangu naupunguza kwa asilimia 20 kuanzia sasa hivi … nchi hii ya ovyo; mishahara minene mno.”

Inasadifu kusema kuwa ni ili kuthamini na kuiheshimu kanuni ya DMU aliziweka kanuni zitakazotumiwa na wale waliopewa dhamana ya uongozi na ambazo wengi wamezikiuka kwa kuwa walafi na hata kujitanua wao wenyewe pamoja na wana wao.

Rejea ya kanuni zilizotumiwa na Baba wa Taifa katika kuishi na kuiheshimu kanuni ya DMU ni pamoja na inayosema “Rushwa ni adui wa haki sitapokea wala kutoa rushwa.”

Ukiukwaji wake unaweza kuonekana kwenye huduma za kijamii ambapo rushwa  imejipenyeza kwa kina. Hali hiyo imeshamiri hata kwenye baadhi ya mikataba na imewafanya baadhi ya watu kujilimbikizia mali zilizopatikana kwa rushwa na kuwavunga wanajamii kuwa wamevuja jasho kumbe wamevuna jasho.

Kutokana na kukosekana kwa DMU miongoni mwa wanasiasa ni sahihi kusema kuwa kanuni nyingine aliibua Baba wa Taifa inayosema “Binadamu wote ni ndugu zangu” nayo imekiukwa kutokana na kujengeka kwa matabaka.

Katika mazingira hayo ni dhahiri kuwa hicho ndicho chanzo cha kuibuka kwa matabaka makubwa mawili ambayo ni ya wavuna jasho na ya wavuja jasho na hivyo kujenga taswira ya wapanda ngazi na washuka ngazi ambao kamwe hawawezi kushikana mikono.

Kuwepo kwa matabaka hayo ni dhihirisho kuwa ile kanuni nyingine nzuri inayosema “Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma,” ilipigwa kisogo na matokeo yake  walio masikini kuendelea kuwa maskini, wakidhulumiwa haki zao na kutokana na uwezo wao kuwa ni duni kubakia machoni kuwa ni wajinga.

Kukosekana kwa DMU miongoni mwa baadhi ya viongozi akisi ya mawazo inakwenda kwenye miaka 10 ya awali ya uhuru (1961-71), ambapo Tanzania ilikuwa nchi inayosifika kwa kuwa na viongozi waadilifu, wasiopenda rushwa. Lakini taratibu mambo yalibadilika kutokana na viongozi kushindwa kutekeleza Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa vitendo.

Katika mfumo wa utawala wa chama kimoja cha siasa, Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ilikuwa  na sera zilizotungwa na ngazi za juu za uongozi wa taifa na kushushwa chini kwa utekelezaji bila wanazuoni kutoa ushauri wala wananchi (watekelezaji) kuombwa kwanza maoni.

Sera hizi zilikosa umaarufu kwa sababu hiyo na pia kutokana na ulaghai wa watekelezaji katika daraja la kati waliokuwa “wanaimba ujamaa” na “kucheza kibeberu”. Watekelezaji hao ndio wamekuwa viongozi wengi wa ngazi za juu wa CCM na taifa hili hivi sasa.

Baba wa Taifa  Mwalimu Julius Nyerere (1922-1999), alisema na kufanya mambo mengi. Mwalimu aliwahi kukiri kwamba serikali yake (1961-84) iliwahi kufanya makosa kadhaa ambayo yalistahili kurekebishwa au kuachwa kabisa na uongozi unaoendeleza taifa hili.

Pamoja na kukiri makosa, Mwalimu aliwahi kulalamika katika hotuba zake kwamba kuna mambo mengine mazuri aliyoasisi ambayo anadhani viongozi waliofuata wameyapuuza bila sababu za msingi. Mojawapo ya mambo mazuri aliyodai yanamepuuzwa ni “Miiko ya Uongozi” katika Azimio la Arusha.

Kwa mtazamo wa Mwalimu Nyerere, mwanasiasa hawezi kuwa kiongozi bora kama ana tamaa ya kujilimbikizia mali na kwamba ni lazima kuwepo na udhibiti maalumu dhidi ya wanasiasa wenye tamaa za kujitajirisha wanaotafuta uongozi wa juu wa taifa ili kujipatia na kujilimbikizia mali.

Dhana hii ya Mwalimu Nyerere imetupwa jalalani na baadhi ya viongozi wengi wa leo. Matokeo ya kupuuzwa kwa dhana hiyo ni kukithiri kwa ufisadi na rushwa kabambe serikalini na uhuru wa raia wengi fukara kutoweka. Hapa ndipo yakazaliwa matabaka mawili ya walalahoi na walalahai.

Haishangazi leo hii kuwepo madai kwamba rasilimali za umma zilitumiwa na kunufaisha watu wachache ambao ndio walijiona wana meno ya kutafuna na kuwaacha walalahoi kwamba wao wana mapengo na ni vibogoyo wakiendelea kuwa hoi maradufu.

Leo hii wavuna jasho wamekosa uzalendo na kuziona benki zetu hazifai na wanakimbilia kuficha fedha ughaibuni wakijua wazi kuwa hazitafahamika. Lakini hoja ya msingi ni kwamba fedha hizo zimepatikana kwa kuzingatia zile kanuni njema zilizohubiriwa enzi za chama kimoja na itikadi moja?

Kama fedha za aina hiyo zimepatikana kinyume na kanuni kama hizo ina maana kuwa kumekuwepo ulafi wa kujilimbikizia na kwa ulafi huo ndio kudhihirisha kuwa walio wengi hawapo kwenye kanuni ya kutosheka ya DMU na wala hawawezi kuikubali.

Kinachoonekana machoni mwa walio wengi  hivi sasa ni ushindani wa kumiliki kama si kuhodhi baadhi ya rasilimali na hivyo kuyaweka makundi ambayo hayana fursa ya kuzifikia rasilimali hizo kwenye  hali mbaya zaidi ya kujiona kuwa ni tabaka linalopuuzwa, kudharauliwa na kuwa ni tabaka la wanyonge.

Hata hivyo hatari itakayokuwepo baadaye ni kwamba kadiri tabaka la wanyonge litakavyokuwa linakandamizwa nalo linakuwa kwenye mkakati wa kujikomboa. Ndani ya mfumo wa kidemokrasia tabaka hilo huonesha ubavu wake wakati wa kura na haiyumkini huleta mabadiliko.

Kwa vyovyote vile kumbukizi ya Hayati Baba wa Taifa inatakiwa kuoionesha jamii jinsi ambavyo ubunifu wa kanuni wa alioufanya ulivyokuwa ni kuheshimu na kuyaishi maisha kwa kuzingatia DMU kwa ajili ya ustawi wa taifa.

The post MIAKA 21 BILA NYERERE Alikubali, kuheshimu kanuni ya DMU  appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *