img

Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na tafakuri ya Uchaguzi Mkuu 2020

October 15, 2020

NA FREDERICK FUSSI

JANA Oktoba 14, Taifa letu tumefanya kumbukumbu ya Siku ya Mwalimu Nyerere na kuadhimisha miaka 21 tangu alipotuacha. Mwalimu Nyerere anakumbukwa kama alama ya uhuru, umoja na mshikamano wa Taifa letu.

Watu wengi hupenda kumnukuu Baba wa Taifa katika hotuba zao na maandiko yao ili kujaribu kuzipa uhai hoja wanazozielezea kwa hadhira zao. Hadhira yetu kama Taifa ipo kwenye mchakato wa uchaguzi utakaohitimishwa kwa wananchi waliojiandikisha kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu. Baba wa Taifa alizungumzia mada mbalimbali kuhusu demokrasia na uchaguzi. Matamshi yake yamebakia kuwa urithi wa Taifa letu. Sisi tuliobakia hatuna budi kuishi na kuenzi kwa vitendo wosia uliotolewa na Mwalimu Nyerere.

Katika moja ya maandiko yake “Tumetoka wapi, tuko wapi, tunakwenda wapi” Mwalimu Nyerere alizungumzia masuala kadhaa ya kidemokrasia na uchaguzi. Moja ya jambo alilozungumzia ni haki ya uraia ya kugombea uongozi wa nchi yake kuanzia ngazi ya kijiji hadi ngazi ya Taifa. Katika nukuu ya kitabu hicho, Baba wa Taifa alisema: “Aidha, raia wa Tanzania hawezi akanyang’anywa haki ya kugombea uongozi wa nchi yake tangu ngazi ya kijiji hadi ngazi ya Taifa. Iwapo wapo wasio na uwezo huo kutaka kuwa Rais, hiyo ni shauri nyingine. Lakini haki ninayo watakaohukumu kama nina uwezo au sina uwezo ni wananchi” mwisho wa kunukuu.

Tukiutathimini uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyia mwaka 2019 uliohusisha uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2020, je haki ya wananchi kutoa hukumu kwa kuchagua viongozi wao iliheshimiwa ipasavyo? Je kama Taifa tulitunga sheria za uchaguzi ili kuwaondolea wananchi haki ya kuchagua na kuchaguliwa? Je uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 tumezingatia wosia wa Baba wa Taifa wa kutowanyang’anya raia wa Tanzania haki yao kugombea udiwani na ubunge? Sehemu kubwa ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka ule wa 2019 tulishuhudia kukiwa na wimbi kubwa la wagombea waliopita bila kupingwa na wagombea wengine kuenguliwa kwenye mchakato wa uchaguzi kwa sababu ya makosa ya kiufundi ya kinachodaiwa kutojaza vizuri fomu zao za kuomba uongozi. Kasoro hizo za kushindwa kujaza fomu ipasavyo ni ndogo ukilinganisha na uzito wa haki ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka kupitia sanduku la kura.

Matokeo ya hili ni kuwa na kundi kubwa la viongozi waliopitishwa kuwa viongozi kwa njia ya kasoro za kisheria au kitaalamu na kukosa kabisa viongozi wenye uhalali wa kukubalika na jamii ya watu inayowaongoza.

Huu ndio msingi wa hoja ya Mwalimu Nyerere katika demokrasia kuwa ni muhimu Watanzania wakapewa haki yao ya kuchagua viogozi wanaowataka wao.

Unapokuwa na kundi kubwa la viongozi ambao wamepatikana kwa mbinu za kasoro za kisheria na kitaalamu basi unakuwa na jamii inayoongozwa kwa misingi isiyokuwa na baraka, heshima na uhalali wa kijamii ambao ni muhimu endapo tunataka kuwa na maendeleo ya kweli.

Hakuna mwananchi anaweza kudai uwajibikaji wa kiongozi ambaye hawakumpigia kura na kiongozi mwenyewe anaweza kupata kiburi kutosikiliza maoni ya wananchi wanaomzunguka kwa sababu hawakumchagua wao, alichaguliwa kwa kasoro za kitaalamu na kisheria za wapinzani wake kushindwa kujaza fomu inavyotakiwa.

Mnapokuwa na ushindani wa demokrasia ya vyama vingi basi ushindani wenyewe haupaswi kuwa wa kasoro ya kisheria na kitalaamu, la hasha, ushindani unapaswa kuwa ule wa ubora wa sera za maendeleo ambazo wagombea watazinadi wakati wa kampeni.

Mgombea endapo akipita bila kupingwa hakuna sheria inayomlazimisha kujipitisha mbele ya wapiga kura kunadi sera zake za maendeleo kwa sababu tayari anakuwa ametangazwa kuwa mshindi.

Sasa hapa tujiulize swali moja, Huyu mgombea anakuwa ni mshindi wa nini? Ameshindaje uchaguzi endapo hakunadi sera zake na wananchi wapiga kura hawakuzikiliza ili kuzipitisha kwenye mizani yao? Kwa hiyo katika mazingira ya namna hii moja kwa moja unabaini kuwa huyu si mshindi kwa maana ya mshindi bali ni sawa tu na mgombea wa nafasi ya kiti maalumu.

Ndio atakuwa hana tofauti na mgombea wa kiti maalumu kwa sababu za viti maalumu anazifahamu yule anayemteua mgombea fulani kuwa diwani au mbunge wa viti maalumu. Na sisi tunajua viti maalumu ni kwa ajili ya watu wanyonge kwenye jamii na kuwa mifumo ya kijamii imewanyima wao fursa za kuwa viongozi kwa hiyo tunawatengenezea viti maalumu ili angalau nafasi zao ziwepo kwenye vyombo vya maamuzi, sauti zao zisikike.

Ikiwa wewe ni mgombea wa ubunge au udiwani na umepita bila kupingwa ndani ya kata yako au jimbo lako, hukunadi sera zako ili kwa ubora wa sera zako ndio wananchi wakuchague, unakuwa na toafuti gani na mbunge au diwani wa kiti maalumu?

Unakuwa ni mbunge au diwani maalumu kwa sababu hukuchaguliwa kwa wananchi kutimiza haki yao ya kupiga kura. Hilo pengine linakuwa jambo bora kabisa ndani ya chama chako cha siasa lakini ni jambo la ovyo kabisa mbele ya macho ya jamii kwa sababu hawakukuchagua wao, isipokuwa uliteuliwa kwa misingi ya kasoro za kisheria na kitaalamu.

Katika nukuu nyingine Mwalimu Nyerere bado anasisitiza ile haki ya Mtanzania kupiga kura endapo ana sifa zote za kutakiwa kupiga kura.

Nyerere anasema: “Jambo limekosewa ni la msingi. Nidyo maama napenda kulisema kwa nini ni la msingi linahusu haki yangu na yako ya kupiga kura. Hii ni haki ya uraia. Madhali wewe ni raia wa Tanzania [huna kichaa, huko gerezani, umetimiza umri unaotakiwa wa miaka kumi na minane] una haki ya kupiga kura. Ni haki yako ya uraia.” Mwisho wa nukuu. Sasa hapa tujiulize kwa pamoja ni sawa kuwa na sheria ya uchaguzi inayoondolea wananchi haki yao ya uraia ya kupiga kura? Nadhani sio sawa kuwa na sheria za uchaguzi ambazo zinatumiwa kuwaengua wagombea kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi na kuwapitisha wagombea wengine bila kupingwa. Dhana ya kupita bila kupingwa ingekuwa na nguvu zaidi endapo bado tungekuwa na mfumo wa chama kimoja, kwamba chama A, hakikuwa na wagombea wengine ambao wangesimama na mgombea wenzao katika uchaguzi. Lakini ni jambo lisiloingia akilini mkiwa katika mfumo wa vyama vingi eti inatokea mnakuwa na wagombea waliopita bila kupingwa kwa njia ya kuwaengua wagombea wa vyama vingine kwa sababu zozote zile za kitaalamu au za kisheria za kushindwa kujaza fomu ipasavyo. Haki ya kuwa raia haiwezi kuondolewa kwa sheria zilizotungwa ama Bungeni au kwenye baraza la madiwani. Ukizaliwa na ukawa raia wa Tanzania, na katiba imetamka bayana kuwa endapo una miaka kumi na minane na ulijiandikisha kupiga kura, na haki hiyo ikaondolewa na sheria ya uchaguzi kwa kuengua wagombea, na wengine kupita bila kupingwa kwa mtindo huo huo basi mfumo wa uchaguzi unakuwa na kasoro za kikatiba.

Katiba yetu imetamka bayana kwenye ile ibara ya 8 kuwa Serikali itapata madaraka yake kutoka kwa wananchi. Je mtu akipita bila kupingwa kwa sababu ya kasoro za kisheria za kutoweza kujaza fomu ipasavyo ile dhana ya kikatiba ya Serikali kuwekwa na wananchi inakwenda wapi? Ni muhimu sheria zetu za uchaguzi zikaweka utaratibu ambao mgombea akikosea kujaza fomu yake apewe nafasi ya kurekebisha kasoro za fomu hizo ili aweze kugombea na wananchi wenzake wapate fursa ya kutimiza matakwa ya kikatiba ya haki ya uraia ya kuchagua au kuchaguliwa.

Ni muhimu sheria za uchaguzi zikaundwa kwa kuzingatia matakwa ya kikatiba ya kutowanyima fursa wananchi ya kupiga kura na kuchagua viongozi wao. Hivyo ndivyo ambavyo tunaweza kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo na vitendo vyenyewe ni kuhakikisha wananchi walioomba kugombea wanagombea na wananchi waliojiandikisha kupiga kura wanapiga kura bila vizuizi vyovyote vya kisheria.

The post Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na tafakuri ya Uchaguzi Mkuu 2020 appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *