img

Ni kuwakosesha haki wagombea kucheleweshewa rufaa zao,on September 17, 2020 at 9:31 am

September 17, 2020

NA ANNA HENGA TANZANIA ni taifa la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi. Kushiriki kupiga kura au haki ya kuchagua viongozi wa kisiasa imeainishwa katika ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (toleo la 2005) na Katiba ya Zanzibar ya 1984 (toleo la 2010). Haki za binadamu hususani
The post Ni kuwakosesha haki wagombea kucheleweshewa rufaa zao appeared first on Gazeti la Rai.,

NA ANNA HENGA

TANZANIA ni taifa la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi. Kushiriki kupiga kura au haki ya kuchagua viongozi wa kisiasa imeainishwa katika ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (toleo la 2005) na Katiba ya Zanzibar ya 1984 (toleo la 2010).

Haki za binadamu hususani haki ya kisiasa na kiraia zinafafanua uchaguzi wa kidemokrasia kuwa ni mchakato muhimu unaostahili wananchi kushiriki, ili kuweza  kupata viongozi wa ngazi mbalimbali za serikali.

Napenda kuendelea kutilia mkazo maana ya uchaguzi kuwa ni mchakato wa kuwapata viongozi wa serikali kwa njia ya kidemokrasia kupitia sanduku la kura kama ambavyo inatarajiwa kufanyika hapa nchini katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

NEC NA MAAMUZI YA RUFAA ZA WAGOMBEA

Mwanzoni mwa mwezi, NEC ilitoa taarifa kwa umma kuhusu idadi ya rufaa za ubunge na udiwani ambapo zilifikia jumla 557 kuanzia Septemba Mosi.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi bado inashughulikia rufaa za wagombea wa ubunge na udiwani zilizowasilishwa kwao ili kutolewa maamuzi. Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika tovuti rasmi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni kwamba hadi kufikia Jumatatu Septemba 14, Tume imeweza kushughulikia rufaa 361 za wagombea ubunge na udiwani na kuwarejesha wagombea 178 kwa mchanganyiko wa ubunge na udiwani kati ya jumla ya rufaa zote 557 mchanganyiko wa wagombea wa ubunge na udiwani zilizowasilishwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Tangu kuwasilishwa kwa rufaa hizo kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, baadhi ya wagombea kutoka vyama vya upinzani walioenguliwa wamekuwa na shauku kubwa ya kutaka kupata mrejesho juu ya rufaa zao ili wajue hatma yao katika uchaguzi huu unaotarajiwa kufanyika ifikapo Oktoba 28.

Mkurugenzi wa Habari, Mawasiliano ya Umma na Uenezi wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohammed Ngulangwa  kama alivyoripotiwa na chombo cha habari cha kimataifa DW, anaona kuchelewa kutoa maamuzi kwa wakati kunawapa wasiwasi mkubwa wanasiasa wengi hasa wa vyama vya upinzani wanaotamani kufanya kampeni na kueleza sera zao kwa wananchi, suala ambalo ni kinyume kabisa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayompa kila raia wa Tanzania haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi katika Ibara ya 21(i).

Kwa miaka mingi serikali ya Tanzania kupitia viongozi na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa demokrasia ikiwemo asasi za kiraia wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kulinda demokrasia na utawala bora hapa nchini, hivyo ni vyema kuhakikisha kila mtu ana jukumu la kulinda demokrasia yetu.

Madhara ya kuenguliwa kwa wagombea

Iwapo rufaa za wagombea walioenguliwa zinazoendelea kufanyikiwa kazi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi zitachelewa zaidi ya hapa, madhara yake ni kwamba wagombea hawa watachelewa kufanya kampeni zao kama ambavyo wagombea wengine wanafanya.

Madhara mengine ni pamoja na kukosekana kwa usawa baina ya wagombea wa chama tawala na wale wa vyama vya upinzani jambo ambalo si sawa kwa mujibu wa ratiba na Kanuni za Uchaguzi.

Imekuwa ni mara ya pili kutokea katika historia ya uchaguzi hapa nchini kwa wagombea wengi wa upinzani wa nafasi za ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu kuenguliwa kwa sababu mbalimbali zinazolalamikiwa kuwa hazina mashiko.

Mtindo huu wa kuenguliwa kwa wagombea wa vyama vya upinzani pekee ulitokea kwa mara ya kwanza katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana  jambo liliwakosesha wananchi haki yao ya kupiga  kura.

Yapo madhara makubwa sana yanayotokana na maamuzi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya kukataa rufaa za baadhi ya wagombea kwa kuwa baadhi ya wananchi kutoka katika majimbo mbalimbali watanyimwa haki yao ya kupiga kura.

Kwa kawaida karatasi inayotumika katika zoezi la kupiga kura ndio kielelezo ambacho mpiga kura anajivunia kuweza kumchagua mgombea kuwa kiongozi wake. Mchakato huu wa kupiga kura humpa mwananchi hamasa na anaweza kujivunia kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi ambapo ni pamoja na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Ikumbukwe kwamba, Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya Umoja wa Mataifa na kikanda na kuwa sehemu yake. Mikataba hiyo ni pamoja na Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu [Ibara ya 21(2) na (3)]. Vilevile Tanzania imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Haki za Kisiasa (ICCPR, 1966).

Hivyo Tanzania inawajibika kuendelea kulinda misingi ya demokrasia, hususan kuhakikisha kuwa viongozi wanaochaguliwa katika ngazi mbalimbali za serikali wanapatikana kupitia uchaguzi  zinazoaminika na zinazoratibiwa na kuendeshwa kwa namna inayofuata misingi ya kidemokrasia.

Rai kwa NEC kuhusu elimu ya mpigakura wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ikiendelea kushughulikia rufaa za wagombea wakumbuke pia kutoa elimu ya mpigakura kwa manufaa ya wananchi kwani ni jukumu lao.

Nikiwa kama mdau mkubwa wa demokrasia na utawala bora, napenda kuhitimisha kwa kutoa rai kwa Tume ya Taifa ya uchaguzi kutilia mkazo katika kutoa Elimu ya Mpiga kura kwa wananchi, ili wananchi waweze kuelewa vyema kuhusiana na mchakato mzima wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kinaipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoa Elimu ya Mpiga Kura nchi nzima, kuratibu na kusimamia taasisi au asasi za kiraia zinaweza kutoa elimu ya mpigakura.

Hata hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa vibali kwa taasisi na asasi zilizoomba kutoa Elimu ya mpigakura ili kufanya kazi kwa kushirikiana na Tume kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kushiriki kupiga kura.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

The post Ni kuwakosesha haki wagombea kucheleweshewa rufaa zao appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *