img

Jubilee yapandisha joto la siasa Kenya,on September 17, 2020 at 7:30 am

September 17, 2020

NA ISIJI DOMINIC MSHIKAMANO ndicho kitu muhimu kinachohitajika hususan zikiwa zimebaki takribani miezi 21 kabla ya Kenya kufanya uchaguzi mkuu lakini kwa hali ilivyo hilo halionekana ndani ya chama tawala cha Jubilee. Ile iliyokuwa Jubilee ambayo iliungwa mkono kila kona ya nchi na ikijivunia umoja ulioletwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto,
The post Jubilee yapandisha joto la siasa Kenya appeared first on Gazeti la Rai.,

NA ISIJI DOMINIC

MSHIKAMANO ndicho kitu muhimu kinachohitajika hususan zikiwa zimebaki takribani miezi 21 kabla ya Kenya kufanya uchaguzi mkuu lakini kwa hali ilivyo hilo halionekana ndani ya chama tawala cha Jubilee.

Ile iliyokuwa Jubilee ambayo iliungwa mkono kila kona ya nchi na ikijivunia umoja ulioletwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto, sasa inaonekana kuelekea kumegeka vipande vipande.

Dalili zilianza kuonekana baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, lakini kidole cha lawama kilinyooshewa kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, baada ya tukio la Machi 9 mwaka 2018 pale Raila alipokutana na Rais Uhuru na kukubaliana kushirikiana kuunganisha Wakenya.

Ndani ya chama hicho tawala kukaibuka makundi mawili yaliyopachikwa; Tangatanga na Kieleweke ambapo kundi la Tangatanga linamuunga mkono Naibu Rais Ruto na lile la Kieleweke linamuunga mkono ushirikiano uliopo kati ya Rais Uhuru na kiongozi wa ODM, Raila.

Hoja kuu ya kundi la Tangatanga ni Uhuru kutekeleza kile wanachokidai makubaliano ya mwaka 2013 kwamba wamuunge mkono Uhuru kuongoza Kenya kwa miaka 10 na baadaye yeye afanye hivyo kwa kumuunga mkono Ruto ili naye awe Rais wa Kenya kwa miaka 10 mengine.

Nayo kundi la Kieleweke linataka makubaliano kati ya Rais Uhuru na Raila yaheshimike na siasa za uchaguzi mkuu zisubiri hadi mwaka 2022 wakisisitiza huu ni muda wa kutekeleza ahadi ambazo viongozi walitoa kwa wananchi.   

Mpasuko ulioko Jubilee sasa unaanza kujidhihirisha kuwa hauna uhusiano na Raila mbali ni wa ndani kwa ndani, hadi imefika kiasi cha wanachama kutaka upande ambao hauridhiki kuondoka. Je, ni nani atakayeamua kuondoka?

Aliyekuwa Kiongozi wa Wengi Bunge la Seneti ambaye pia ni Seneta wa Elgeyo Marakwet na mshirika wa karibu wa Naibu Rais Ruto, Kipchumba Murkomen, alimwelekezea lawama Rais Uhuru akimshutumu kupanga mipango ya kumfadhaisha Naibu Rais katika safari ya kutimiza ndoto zake za kuingia Ikulu.

Lakini wandani wa Rais Uhuru wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe na baadhi ya mawaziri wanadai Ruto ndiye aliyejichimbia kaburi kwa kile walichodai ‘kuanza mapema kampeni za urais’.

“Matatizo ambayo yanamzonga Naibu Rais hayana uhusiano na Raila Odinga, hayo matatizo yana kila kitu kuhusu Uhuru Kenyatta na kujipangia mwenyewe,”alisema Murkomen wakati akifanya mahojiano na Citizen TV.

Katika mahojiano tofauti, Murathe alisema: “Hatujui nani atakuwa rais ajaye, lakini tunafanya kazi kwa bidii kujua nani hawezi kuwa rais.”

Ni malumbano mazito ndani ya Jubilee ambacho hakijafanya mkutano mkuu wake kwa muda mrefu, isipokuwa Rais Uhuru kuwaita iwe ni Ikulu au ukumbi wowote wabunge na maseneta wa chama hicho endapo kuna kitu anahitaji kipitishwe bungeni.

“Kama nikikutana na Rais Kenyatta leo, nitamuangalia machoni na kumwuliza ni kosa lipi moja ambalo linafuta kila kitu ambacho William Ruto alimfanyia kuanzia mwaka 2002 hadi kushinda uchaguzi wa kwanza na ule wa marudiano wa pili,” alisema Murkomen.

Lakini kama kawaida, kauli hiyo ya aliyekuwa Kiongozi wa Wengi Bunge la Seneti likajibiwa na Makamu Mwenyekiti wa Jubilee.

“Watu wanaenda kanisani na kuapa mbele ya watu na Mungu kwamba wanaoana hadi kifo kiwatenganishe, lakini bado wanatalakiana. Siasa ni nguvu; ikiwa ulianza kwa tabia nzuri na ukabadilisha tabia yako njiani, basi ni vyema ujue kila mtu ana haki ya kubadilisha mawazo yake juu ya msimamo,”alisema Murathe.

Naibu Rais ni mtu aliyetengwa katika serikali aliyosaidia kubuniwa mwaka 2013 na 2017 na hili linaonekana wazi baada ya majukumu yake kukabidhiwa Waziri wa Usalama, Dk. Fred Matiang’i, lakini hilo halimtikisi Ruto katika azma yake ya kuwania urais 2022.

Mawaziri nao wamejikuta wakijitosa kwenye malumbano ndani ya chama tawala wengi wakihoji ni kwa utashi wao au wanapokea maelekezo? Waziri wa Mazingira, Keriako Tobiko, alisema Naibu Rais Ruto ni karani katika serikali ya Rais Uhuru.

Akizungumza hivi karibuni katika Msitu wa Loita uliopo Kajiado, Tobiko alimshutumu Ruto na washirika wake kwa kutomheshimu Mkuu wa Nchi wakati yeye (Ruto) ni karani wa Rais kama walivyo mawaziri wengine.

“Heshima ni ya pande mbili. Kama hauwezi kumheshimu Rais basi haustahili kuheshimiwa na mtu yeyote. Kama haitoshi, Naibu Rais ni karani kwa Rais na kama ninavyomheshimu Rais hata pia Naibu Rais lazima amheshimu,”alisema Waziri huyo wa Mazingira.

Kauli hiyo ya Waziri Tobiko, ilimwibua Seneta wa Elgeyo Marakwet, Murkomen, ambaye naye pia aliitwa karani kwa kumkosoa Rais Uhuru kwa kukubali matamshi ya dharau yanayotolewa na mawaziri dhidi ya naibu wake.

“Bila ya baraka za Rais, hawa mawaziri wasingeweza kumtukana Naibu Rais. William Ruto sio karani wa mtu yeyote. Alichaguliwa pamoja na Rais na bila yeye, Uhuru asingekuwa Rais na Tobiko asingekuwa karani. Katika serikali zinazofanya kazi, Tobiko angefutwa kazi,” Murkomen aliandika katika mtandao wake wa kijamii.

Ruto anapata utetezi kwa washirika wake lakini Murathe anaendelea kumkalia kooni akiwa tayari ameshamwondoa Naibu Rais huyo miongoni mwa wanasiasa watakaowania urais 2022, huku wakisisitiza Uhuru atakuwa katika nafasi muhimu kwenye maamuzi ya nchi baada ya mwaka 2022 hata kama hatakuwa rais.

Murathe alianza kampeni dhidi ya Ruto ambayo awali ilionekana kama mkakati wake binafsi, lakini sasa mkakati huo unaonekana kuhusisha watu wengi zaidi wenye nguvu dhidi ya Naibu Rais ambaye amedai mfumo umepanga kuona anashindwa kufaulu.

Makamu Mwenyekiti huyo wa Jubilee ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Gatanga anayejua kujieleza tena kwenye majukwaa ya kisiasa, amejitosa kama mtu muhimu katika kitendawili cha nani atakayemrithi Uhuru huku Rais akiamua kucheza karata zake kwa uangalifu.

Kinachoshangaza ni kwamba mawazo ya Murathe hayatofautiani na ya Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli, ambaye anatabiri Uhuru ataendelea kuwepo baada ya mwaka 2022 lakini sio kwenye nafasi ya urais.

“Atakuwa katika majukumu mengine. Nipo karibu na Raila na Gideon (Moi – kiongozi wa KANU). Kama ilivyo kwa Uhuru, hata Raila na Gideon wanaitakia mema nchi hii. Wanataka kuacha kumbukumbu njema kwa Wakenya,”alisema Katibu Mkuu huyo wa COTU.

Huku wandani wa Ruto na mawaziri katika serikali ya Uhuru wakionekana kulumbana hadharani, Naibu Rais amekuwa akisisitiza uhusiano wake na Rais upo imara akigusia kwamba kutoonekana kwake katika serikali ya Uhuru kwa muhula wake wa pili ni makubaliano baina yao wawili.

The post Jubilee yapandisha joto la siasa Kenya appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *