img

Wananchi zingatieni ilani za vyama kuelekea uchaguzi 2020,on September 10, 2020 at 8:57 am

September 10, 2020

NA ANNA HENGA IMEKUWA ni kawaida kila mwaka wa uchaguzi vyama vya siasa hapa nchini hutoa hadharani Ilani zao za uchaguzi mkuu ili kuweka bayana nia zao pamoja na mipango madhubuti watakayotumia kujenga nchi. Hadi kufikia sasa kampeni zimeshafunguliwa rasmi na tumeona maelfu ya wananchi wakijitokeza katika mikutano ya ufunguzi wa kampeni za vyama mbalimbali
The post Wananchi zingatieni ilani za vyama kuelekea uchaguzi 2020 appeared first on Gazeti la Rai.,

NA ANNA HENGA

IMEKUWA ni kawaida kila mwaka wa uchaguzi vyama vya siasa hapa nchini hutoa hadharani Ilani zao za uchaguzi mkuu ili kuweka bayana nia zao pamoja na mipango madhubuti watakayotumia kujenga nchi.

Hadi kufikia sasa kampeni zimeshafunguliwa rasmi na tumeona maelfu ya wananchi wakijitokeza katika mikutano ya ufunguzi wa kampeni za vyama mbalimbali vya kisiasa kuelekea siku ya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Uchaguzi huu utafanyika kwa usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kushuhudiwa na wadau wengine wa uchaguzi na wapenda demokrasia kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo wananchi wenyewe.

Tayari vyama vya siasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi huu vimejipanga ili kuweza kuhakikisha ilani za vyama vyao zilizojaa mipango na mbinu za kuboresha maisha zinawafikia wananchi kwa wakati.

Ilani za vyama vikuu vya upinzani pamoja na ile ya chama tawala, zimekuwa na umaarufu mkubwa miongoni mwa wananchi kwa kuwa wengi wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kuona mipango ya kila chama katika kuleta mabadiliko chanya hapa nchini.

Nikiwa kama mdau wa demokrasia, utawala wa sheria pamoja na haki za binadamu, napenda kuwasihi wananchi kutumia muda wao mwingi kusoma na kuzielewa ilani hizi ili waweze kufanya maamuzi bora ya kuchagua viongozi bora kwa faida ya Taifa la Tanzania.

’Kuna msemo usio rasmi unaotumiwa na baadhi ya watu unaosema kwamba Watanzania hawapendi kusoma na ukitaka kuwaficha Watanzania jambo fulani basi liweke katika maandishi’.

Watanzania tusikubaliane na msemo huu bali tujiwekee utaratibu mzuri wa kusoma ili kupitia kusoma machapisho kama vile hizi ilani za vyama vya siasa, basi tuweze kupata uelewa wa mipango na nia za vyama mbalimbali vya siasa ya kuleta maendeleo endelevu nchini.

Vyama vya siasa vinavyoendelea na kuchuana katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani vimeelezea malengo yake kwa taifa na namna ambavyo watafanya mageuzi katika sekta mbalimbali na hatimaye kuweza kuleta maendeleo na kuwanufaisha Watanzania kiujumla.

Nikiwa kama mdau mkubwa wa demokrasia na utawala bora, nitachambua na kulinganisha ilani za uchaguzi za vyama vitatu jinsi walivyojipanga kuinua kilimo hapa nchini iwapo watashinda uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.

Nitaanza na Ilani ya CCM ambacho ndio chama tawala pamoja na ilani za vyama vikuu vya upinzani ambavyo ni Chadema na ACT-Wazalendo kuhusu kilimo na ufugaji kwa kuwa kwa miaka mingi ndio imekuwa shughuli kuu ya uzalishaji hapa nchini.

ILANI YA CCM KUHUSU KILIMO

Pamoja na mipango mingine mingi ya maendeleo ambayo CCM imeeleza katika ilani yao, Chama Cha Mapinduzi katika kipindi cha miaka mitano ijayo kimepanga nanukuu;

Kuelekeza serikali kuendelea kuleta mabadiliko makubwa na ya kisayansi katika ufugaji kwa kuhimiza ufugaji wa kisasa wenye kuzingatia kinga, tiba na utafiti wa mifugo ili kuzalisha ajira nyingi zaidi hasa kwa vijana na kuinua mchango wa sekta katika Pato la Taifa na kuleta ustawi wa wananchi.

Aidha, Serikali itatakiwa kushughulikia kwa nguvu zaidi migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Ili kufikia azma hiyo, CCM itaelekeza Serikali kujikita katika kuboresha maeneo ya kimatokeo kama ifuatavyo;

Kwanza; Kuendeleza na kuimarisha huduma za Ugani katika ngazi za Kata na Vijiji kwa kuhakikisha kuwa kila mfugaji anafikiwa na huduma za Ugani na kwa wakati.

Kwa Kuongeza idadi ya maofisa ugani kwa kuajiri na kuhakikisha kuwa kila kata na kijiji kinafikiwa na ofisa ugani au mtoa huduma za ugani nchini Kujenga skimu mpya za umwagiliaji 208 nchini, kati ya hizo skimu ndogo ni 123, skimu za kati 63 na skimu kubwa 22. Ujenzi huu unatarajia kuongeza eneo la umwagiliaji kwa hekta 136,928. Aidha, sekta binafsi itahamasishwa kushiriki kwenye ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji itakayoongeza eneo la umwagiliaji kwa eka 150,000;

Vilevile; Kujenga na kuimarisha mabwawa ya uvunaji wa maji ya mvua 88 katika skimu za umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha mpunga na mazao mengine katika mikoa 25 ili kuongeza maeneo ya kilimo cha umwagiliaji nyingi zaidi;

Hii ni baadhi tu ya mipango niliyonukuu katika ilani ya CCM yapo mengi katika ilani yao nashauri kila mmoja wetu atafute nakala ya Ilani ya CCM na ajisomee ili aweze kuelewa vizuri na baadae kuchaga kiongozi bora.

ILANI YA CHADEMA KUHUSU KILIMO

Pamoja na mipango mingine mingi ya kuboresha sekta mabalimbali iliyopo katika ilani ya chama kikuu cha upinzani Tanzania Chadema;Nakuwekea hapa kwa uchache mipango yao ya namna wao watakavyoboresha sekta ya kilimo kama ambayo kwao wamekitambua kama ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania katika ilani yao; Wao nameahidi kama ifuatavyo;

Serikali ya Chadema kwa kushirikiana na sekta binafsi itahakikisha kuwa taasisi au mataifa ya nje yanayotaka kuwekeza katika kilimo nchini yanafanya hivyo kwa kuingia mikataba na vijiji na maeneo husika ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo husika wananufaika na uwekezaji mkubwa wa kilimo kiteknolojia na kimasoko.

Pia; Serikali ya Chadema itaweka msukumo wa kipekee kwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine na vyuo vingine vya kilimo ili viwe ni vituo vya utafiti kwa vitendo katika mazao, mifugo na chimbuko la mbegu bora. Lengo ni kuhakikisha kuwa nchi inajitosheleza katika mahitaji ya mbegu na kuliondolea taifa aibu ya kuagiza mbegu bora za kutoka nje ya nchi.

Vilevile; Serikali ya Chadema itahamasisha uanzishwaji wa kilimo cha mijini (urban farming) hasa katika mazao ya bustani za mboga na matunda. Lengo ni kuhakikisha kuwa katika miji yote mazao kama mboga na matunda yanapatikana kwa urahisi, katika mazingira safi na salama. Hii itakuwa ni pamoja na kuweka mfumo wa kuanzisha viwanda vidogovidogo vya kuhifadhia matunda na mboga.

Hiyo ndio baadhi ya mipango ya chama kikuu cha upinzani Chadema juu ya namna ya kuboresha sekta ya kilimo nchini. Nawasihi wananchi kujisomea kiundani ilani hizi ili kuweza kuchagua kiongozi bora atakayeweza kuendeleza kilimo hapa nchini Tanzania.

ILANI YA ACT-WAZALENDO KUHUSU KILIMO

Chama cha ACT-Wazalendo kimekuwa pia mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa ilani ya chama hicho, inaelezea kwa kina namna ambavyo chama hicho kitaboresha sekta ya kilimo kwa kipindi cha miaka mitano iwapo wataingia madarakani.

ACT-Wazalendo katika kuhakikisha kwamba wanapata mapinduzi makubwa ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini, Serikali ya ACT-Wazalendo itafanya yafuatayo;

Itatenga asilimia 20 ya bajeti ya maendeleo kwenye Sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi, mara mbili zaidi ya makubaliano yaliyozimiwa na Umoja wa Afrika (CAADAP).

Itapanua na kuboresha vyuo vya kilimo, na kuwekeza kiasi kisichopungua Sh bilioni 100 kwa mwaka katika utafiti, usambazaji wa mbegu bora za kilimo na kutengeneza mnyororo wa thamani kwa kila zao linalozalishwa hapa nchini.

Itafungamanisha sekta ya kilimo na sekta ya viwanda, kwa kuhakikisha kwamba viwanda vya ndani vinapata zaidi ya asilimia 80 ya mahitaji yao kutoka kwa wakulima na kwamba wakulima wanafaidi bei nzuri ya mazao yao na soko la uhakika.

Pia; Itatengeneza mahusiano ya karibu ya kikazi kati ya vyuo vya ufundi, vyuo vya kilimo, vyuo vya masoko na biashara na vyuo vya jamii ili kuhakisha utaalamu, taaluma na uvumbuzi unachagiza ukuaji wa sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo na kutengeneza ajira zenye tija zisizopungua milioni 5 kwenye mnyororo wa thamani ndani ya miaka 5.

Hii ndio baadhi ya mipango michache niliyonukuu katika ilani ya ACT Wazelendo kuhusu namna watavyoendeleza kilimo kuelekea uchaguzi mkuu 2020, ili kuweza kuwapatia baadhi ya wadau wa uchaguzi  fursa ya kuelewa mipango kadha wa kadha ya kuboresha kilimo inayoahidiwa na chama na ACT wazalendo.

Rai kwa wadau wote wa uchaguzi

kabla ya kuanza kutoa rai kwanza napenda kueleza sababu moja tu ambayo imenisukuma kufanya ulinganifu wa ilani za vyama hivyo vitatu; ni kwamba kila chama kinachotaka kuingia madarakani kina nia njema na dhabiti ya kutaka kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo kilimo nchini Tanzania.

Kila chama kina uelewa wa hali halisi ya maisha ya Watanzania kwa hiyo kazi imebaki kwa wananchi kuchagua ni chama kipi kiongoze miaka mitano ijayo.

Napenda kuendelea kusisitiza umma wa Tanzania kujiwekea mazoea ya kusoma hasa nyaraka mbalimbali za uchaguzi na kuzielewa katika wakati huu wa kampeni za vyama kuelekea siku ya kupiga kura ambayo ni Oktoba 28.

Nipende kutoa rai kwa wadau wote wa uchaguzi kuendelea kuitunza amani na kuheshimu misingi ya demokrasia hasa tunapoelekea katika uchaguzi mkuu ambao ndio msingi wa demokrasia na utawala bora.

Mwisho kabisa napenda kuwatia moyo Watanzania na kuwasihi kutumia haki yao ya kikatiba kumchagua kiongozi aliye bora na ambaye anaheshimu misingi ya utawala wa sheria na haki za binadamu, huu ndio wakati wetu sisi wananchi kujidai kwani ni wakati kama huu wa uchaguzi pekee ndio tunapata mamlaka makubwa ya kuamua na kuchagua serikali tunayoitaka.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

The post Wananchi zingatieni ilani za vyama kuelekea uchaguzi 2020 appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *