img

Vyombo vya usalama ni rafiki wa wapiga kura,on September 10, 2020 at 8:51 am

September 10, 2020

NA JAVIUS KAIJAGE HAPO zamani za kale ilikuwa ni kwamba raia kumwona au kukutana na askari ni kama kukutana na simba, chui au kitu chochote cha kuogofya. Kwa sisi ambao tulibahatika kukulia katika mazingira ya vijijini, nakumbuka siku moja nikiwa mtoto mdogo sana pale kijijini kwetu alijitokeza kijana mmoja aliyekuwa ametoka kwenye mafunzo ya Jeshi
The post Vyombo vya usalama ni rafiki wa wapiga kura appeared first on Gazeti la Rai.,

NA JAVIUS KAIJAGE

HAPO zamani za kale ilikuwa ni kwamba raia kumwona au kukutana na askari ni kama kukutana na simba, chui au kitu chochote cha kuogofya.

Kwa sisi ambao tulibahatika kukulia katika mazingira ya vijijini, nakumbuka siku moja nikiwa mtoto mdogo sana pale kijijini kwetu alijitokeza kijana mmoja aliyekuwa ametoka kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akiwa amevaa kombati, hakika siku hiyo ilikuwa ya vihoja maana watu wengi baada ya kumwona baadhi yao waliamua kutimukia porini.

Kukimbilia porini ilikuwa ni kumhofu yule askari kwani wananchi hao waliamini kuwa kuna tatizo hivyo alikuja kwa ajili ya kuwakamata.

Huyo akiwa ni mhitimu wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, aliogopwa sana lakini pia polisi wetu katika mazingira tofauti wamekuwa wakiogopwa na wananchi wanapokuwa wamekwenda maeneo tofauti kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kila siku.

Akijitokeza Polisi utasikia watu mbalimbali hao ni Polisi sijui wamekuja kufanya nini kwetu muda huu! Hofu hofu hofu! Polisi hao, polisi hao.

Hata hivyo siku hizi mambo yamebadilika kwani wananchi walio wengi wameishaanza kutambua umuhimu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama katika maisha yao na hivyo kuvichukulia kama marafiki na ndiyo maana sehemu mbalimbali wananchi wanataka kujengewa vituo vya Polisi.

Kimsingi vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama, majukumu yao makuu ni kwa ajili ya kusimamia Ulinzi na Usalama ili amani iendelee kuwepo na wala si vinginevyo.

Katika kipindi hiki tuko kwenye kampeni za kisiasa na tunaelekea kufanya uchaguzi mkuu mwishoni mwa Oktoba mwaka huu wa 2020 ambapo uwepo wa ulinzi na usalama ni suala nyeti ambalo haliwezi kuepukika.

Ndiyo jukumu la Ulinzi na Usalama, ni la kila mwananchi lakini wapo wahusika waliopewa majukumu rasmi kwa ajili ya kusimamia shughuli hizo kwani hao ndio wamepewa mafunzo maalumu ya kufanya hivyo.

Shughuli za kisiasa ikiwemo kufanya kampeni, kupiga kura na hatimaye kutangaza mshindi/washindi ni mchakato ambao hauwezi kukwepa mkono wa vyombo vya Ulinzi na Usalama hususan Jeshi letu la Polisi.

Kwa mujibu wa jarida la Utawala wa umma, Fedha na Sheria linaloangazia wajibu wa Usalama katika uchaguzi wenye kuaminika na demokrasia endelevu nchini Nigeria, mwandishi wa jarida hilo ndugu Osezua Ehiyamen anasema: ‘‘ Uchaguzi hauwezi kuchukuliwa wenye kuaminika, huru na haki mpaka pawepo wakala wa demokrasia kama vile usalama, vyombo vya habari na taasisi za kiraia.

Mwandishi katika jarida hilo anaendelea kusema kuwa historia ya maendeleo ya kidemokrasia inaonyesha kwa kiwango cha juu kuwa taifa la kidemokrasia haliwezi kuendesha chaguzi zilizo huru na haki bila ya maafisa wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, watendaji wa vyombo vya habari na taasisi za kiraia kutimiza wajibu wao.

Aidha jarida linafafanua kuwa ni kweli nchi haiwezi kushuhudia uchaguzi ulio wa uaminifu, kudumisha demokrasia isipokuwa tu vyombo vya Ulinzi na Usalama vimewajibika kabla na baada ya uchaguzi.

Kwa upande wa jarida la Wajibu wa Jeshi la Polisi katika Chaguzi za Kidemokrasia lilitolewa na Jeshi la Polisi mwaka 2015 linafafanua kuwa: ‘‘Ofisa wa Polisi ni mtumishi wa kutekeleza sheria na kulingana na Ibara ya 1 ya Kanuni ya Tabia Njema ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Watumishi wa utekelezaji wa sheria.’’

‘‘Watumishi wa utekelezaji wa sheria wakati wowote ule ni watekelezaji jukumu walilopewa kwa mujibu wa sheria, kuitumikia jamii na kuwalinda watu wote dhidi ya vitendo visivyokuwa vya kisheria, kwa kiwango kikubwa cha uwajibikaji kutokana na taaluma zao.

Katika jamii ya kidemokrasia, Jeshi la Polisi na jamii wanafanya kazi pamoja ili kuwa na usalama, maisha yenye heshima na yenye hadhi ya juu kwa wananchi wote bila kujali umri wao, jinsia, uwezo wao au hali yao ya ulemavu, asili yao ya kijamii au uwezo wa kiuchumi, mawazo yao ya kisiasa, asili yao ya kikabila au dini zao wala bila kujali utambulisho mwingine wowote ule wa kijamii.

Jeshi la Polisi lina jukumu muhimu sana la kuhakikisha amani, utulivu na usalama nchini katika kipindi cha kampeni za uchaguzi, katika kipindi cha uchaguzi na pia baada ya uchaguzi.

Baada ya kuangalia mapitio haya mawili ya majarida inabainika jinsi gani vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyo na wajibu mkubwa linapokuja suala la kulinda na kutetea demokrasia hususan kampeni za uchaguzi na uchaguzi kwa ujumla.

Katika mazoezi ya pamoja ya vyombo vya Ulinzi na Usalama yaliyofanyika Mkoa wa Mwanza Jumamosi ya Agosti 5 mwaka huu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, ACP Muliro Jumanne Muliro aliwaambia washiriki kuwa vyombo vya Usalama vitahakikisha vinasimamia amani katika kipindi chote cha kampeni na uchaguzi mkuu kwa ujumla.

Ni dhahiri ya kwamba utimamu na utayari wa walinzi wetu wa amani katika kutekeleza majukumu yao kwa haki bila upendeleleo huku wakiheshimu taratibu, kanuni na sheria ndivyo vitapelekea  kampeni na uchaguzi vimalizike kwa usalama.

Ni ukweli usiopingika kwamba vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vipo kwa ajili yetu na kwa matarajio yetu sisi wananchi na wala visichukuliwe kama maadui wa demokrasia.

Vyombo vyetu ya kiusalama kuwepo kwake katika mikusanyiko ya kampeni za uchaguzi na katika uchaguzi si kutafuta shari, kukamata watu bila sababu bali ni kusimamia ulinzi ili mambo yote yaweze kufanyika kwa amani kwa mujibu wa sheria zinazoongoza matukio husika.

Ni kweli baadhi ya wananchi katika mikutano ya kampeni wanaweza kujiuliza kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama ni vya nini wakati wao wenyewe wanajua wajibu na wanaweza kujisimamia?

Sina shaka ya kwamba Watanzania wanatambua umuhimu wa amani na hivyo wako tayari kujisimamia lakini ikumbukwe kuwa saikolojia ya wanadamu ni ya ajabu kwani ndani ya wastaarabu wapo pia wasiopenda ustaarabu huo.

Ni katika kampeni za kisiasa utashangaa mtu anaendeshwa na mihemko ya upenzi uliopitiliza na hatimaye kuchafua hali ya hewa kwa kuanza kurusha mawe ovyo.

Ni katika mikutano ya kampeni panaweza kujitokeza watu wanaotumia lugha za matusi kudhalilisha wengine.

Ni katika vituo vya kupiga kura, mihemko ya kisiasa kutokana na mapenzi yaliyopitiliza watu fulani wanaweza kushinikiza kutangazwa kwa mgombea ambaye siyo halali kwa maana hajashinda katika uchaguzi huo.

Wapiga kura wengine wanaweza kutumiwa na mihemko ya kisiasa kuwalazimisha wenzao wasio katika upande wao  kuwapigia kura ambao si chaguo lao.

Ni katika vituo vya kupigia kura zinaweza kufanyika njama za kuiba kura, ili kumpa ushindi ambaye si mshindi halali na hivyo kuhatarisha mustakabali wa demokrasia.

Si tu katika mikutano ya kampeni za uchaguzi na kwenye vituo vya kupiga kura panaweza kutokea vurugu zinazotokana na ushabiki wa vyama au wagombea, bali pia katika mikusanyiko hiyo hata vibaka wanaweza kujitokeza.

Si jambo la kushangaza katika mikutano ya kampeni za uchaguzi na uchaguzi wenyewe kuwepo kwa wezi wa mali za watu hususan simu, mikoba na fedha.

Katika mazingira ya namna hii vyombo vya Ulinzi na Usalama vinahitajika kwa kiwango kikubwa katika kusimamia demokrasia ya kweli.

Yote katika yote vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vimesheheni maofisa/askari  walioelimika huku wakitambua thamani ya demokrasia, hivyo wapiga kura na wananchi wote kwa ujumla wasiwe na mashaka dhidi yake kwani nina uhakika vimejipanga kutenda haki.

Email:  HYPERLINK “mailto:javiusikaijage@yahoo.com” javiusikaijage@yahoo.com, Simu: 0756521119

The post Vyombo vya usalama ni rafiki wa wapiga kura appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *