img

Tuangalie uongofu, tukatae upotovu,on September 10, 2020 at 7:12 am

September 10, 2020

NA ALOYCE NDELEIO IPO dhana iliyojengeka kwamba jamii imelemazwa na kusikiliza mambo lakini imejiweka kando kuyaangalia mambo yenyewe na hilo limekuwa likielezwa mara nyingi kupitia kujijengea utamaduni wa kusoma iwe ni vitabu, majarida na hata magazeti. Hilo linafafanuliwa kwamba kutokana na kupanuka kwa teknolojia na kuwepo kwa mitandao imekuwa rahisi kusambaza taarifa mbalimbali kwa urahisi na hivyo
The post Tuangalie uongofu, tukatae upotovu appeared first on Gazeti la Rai.,

NA ALOYCE NDELEIO

IPO dhana iliyojengeka kwamba jamii imelemazwa na kusikiliza mambo lakini imejiweka kando kuyaangalia mambo yenyewe na hilo limekuwa likielezwa mara nyingi kupitia kujijengea utamaduni wa kusoma iwe ni vitabu, majarida na hata magazeti.

Hilo linafafanuliwa kwamba kutokana na kupanuka kwa teknolojia na kuwepo kwa mitandao imekuwa rahisi kusambaza taarifa mbalimbali kwa urahisi na hivyo kuwafanya walio wengi kuzama kwenye mitandao.

Aidha hali hiyo imesababisha wengi kusahau kusoma vitabu na hata kujifikirisha zaidi kwa dhana kuwa kila kitu kinapatikana kwenye mitandao jambo ambalo si sahihi bali ni kupotoka.

Mfano huo si tu kwamba upo kwenye kudhoofu kwa tabia ya kujisomea bali upo pia kwenye nyanja nyingine zikiwemo za uchumi, utamaduni na siasa.

Katika uchumi inakuwa rahisi kwa wanajamii walio wengi kuzikubali bidhaa zinazozalishwa nje kuliko zinazozalishwa ndani ya nchi kutokana na dhana kuwa bidhaa hizo ni nzuri zaidi kuliko za ndani.

Dhana hiyo ilipounganishwa na mifumo ya biashara huria ndio kabisa jamii ikaingia kwenye upotovu na kuvisahau viwanda vya ndani ambavyo leo hii jamii inaanza upya masuala ya viwanda.

Ukweli unabakia kuwa kama si upotovu huo huenda hesabu zingekuwa kwenye awamu ya pili ya mapinduzi ya viwanda.

Katika nyanja ya utamaduni ndio kabisa jamii imeenda kinyume na kile alichokisema Mwanamapinduzi Frantz Fanon katika Kitabu  ‘A Dying Colonialism’ ambacho tafsiri yake ‘Ukoloni unaokufa’.

Anasema, “Jinsi watu wanavyovaa wao wenyewe, pamoja na tamaduni za kuvaa na uzuri wa desturi unaotumika unajumuisha mwonekano wa kipekee wa jamii yaani inaweza kusemwa aina moja ambayo  inakubalika… ni kupitia nguo zao ambazo jamii imefahamika kwazo mwanzoni, iwe ni kupitia kumbukumbu za  maandishi  au picha  au filamu.

“Hivyo yapo maendeleo bila tai, misuli au bila kuwepo kofia. Ukweli wa kinachomilikiwa katika kundi la jamii kwa  kawaida unafahamika kutokana na tamaduni za mavazi.”

Leo hii utambulisho huo wa mavazi umeegemea uvaaji ambao ni kadhia kuanzia kukosa staha hadi uvaaji ambao ni watu waliojitoa ufahamu, kwani haishangazi mtu kwenda duka la nguo la kununua nguo zilizochanika na kudai ni kwenda na wakati (fasheni).

Kwenye ulingo wa siasa huko ndiko kumekuwa na kusikiliza zaidi na kuangalia kumekosekana. Imekuwa ni rahisi kuona mambo yakienda shaghalabaghala na kuvishwa vilemba vya ukoka bila kutafakari lipi lililo chanya na lipi ni hasi.

Wakati kampeni zikiwa zinaendelea umekuwa ni msimu wa wavuja jasho kusabahiwa kwa heshima wakivishwa kilemba cha uheshimiwa, ndugu, rafiki, wapendwa na kila aina ya sifa.

Wapo wanaosikiliza na kuona kweli wamekuwa ni waheshimiwa na maswahiba wakubwa, kiasi kwamba wangekuwa ni watu wa kuangalia wangetambua kuwa wanapakwa mafuta kwa mgongo wa chupa na msimu wenyewe ni mfupi sana kwani ukiisha tu uheshimiwa unafikia ukomo na kurudi kwa wenyewe.

Kama wavuja jasho wangekuwa wanasikiliza na kuangalia wangemudu kuhoji uheshimwa wao kama ni endelevu au la.

Wavuja jasho wanaopenda kusikiliza na kuangalia wanaweza kurejea maudhi ya riwaya ya iliyoandikwa na mwandishi nguli wa Afrika Chinua Achebe ya ‘A Man of the People’ ambapo wahusika wakuu ni   Chifu Nanga  na kijana Odili.

Maudhui yanayomtambulisha ni kwamba  ni kiongozi aliyebobea katika rushwa na anayetumia madaraka yake kuwadhibiti wanaopinga dhuluma hizo na kuikandamiza mikakati yote ya kupinga dhuluma.

Kimsingi taswira iliyopo ni kwamba anawakilisha mahitaji na matakwa ya baadhi ya wanasiasa kwamba wanachokipa kipaumbele ni pamoja na uzinzi, magari ya kifahari, ardhi na kujilimbikizia mali.

Nanga anawakilisha wanasiasa wahafidhina ambao kimsingi hawataki mabadiliko kwa dhana kuwa wao ndio wanajua zaidi na hivyo kufikia hatua ya kuwananga wanasiasa vijana wanaokataa udhalili dhidi ya jamii na fedheha ya  rushwa.

Anabainishwa kuwa ni  ‘mtu wa watu’, lakini yupo kinyume  ni mtu anayetumia nafasi yake hiyo kujineemesha kwa kupora zaidi mali za watu.

Kijana Odili baada ya kuingia kwenye siasa kwa ajili ya kulipiza kisasi cha kuporwa mchumba wake na huyu Nanga na mapambano yanahitimishwa kwa ushindi ambao ulileta mabadiliko yaliyomng’oa Nanga. Hivyo ikabainika  sifa ya ‘mtu wa watu’ ni  fedheha kwani ni adui wa watu.

Ipo hali nyingine baadhi ya wanajamii hugeuzwa kuwa maadui wa watu  ilhali wakiwa ni watu wa watu. Tamthiliya ya ‘An Enemy of the People’ yaana adui wa watu iliyoandikwa na Henrick Ibsen mhusika mkuu Dk. Stockman, anabaini mfumo wa maji taka usio salama kwa jamii na ugunduzi wake uliungwa mkono na viongozi.

Hata hivyo baadaye meya wa mji husika alimwambia aondoe hoja yake kwa madai kuwa bwawa husika linafanyiwa ukarabati  kuuona ugunduzi wa Dk. Stockman kuwa haukuwa na tija.

Licha ya kwamba meya huyo alikuwa ni kaka yake, aliingia katika malumbano naye na alitegemea gazeti la Manispaa ya Mji wa Hovstad, lingeihabarisha jamii suala hilo kwa umakini.

Hakuna lililofanyika kutokana na hila zilizofanywa na meya kuhakikisha kwamba jamii ya Hovstad na Aslasken, inaipinga hoja ya ugunduzi huo na kwamba haukuwa na manufaa yoyote.

Hali hiyo ilimfanya Dk. Stockman kukabiliwa na kibarua kigumu cha kulaumu uongozi wa mji kutokana na hatua walizokuwa wanafanyiwa wakazi wa maeneo hayo.

Dk. Stockman na binti yake walikabiliwa na kipindi kigumu kwani meya alisema utafiti huo ulikuwa ni njama za kutafuta fedha na umaarufu na wajumbe wa Baraza la Manispaa walikubali.

Alipata ukinzani kwa sababu meya wa mji alikuwa ndiye mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na mmiliki wa hisa nyingi kwenye bwawa hilo, hivyo utafiti huo ulikuwa unaingilia masilahi yake.

Vyombo vya habari ambavyo ni sauti ya umma, vilizibwa mdomo ili kuuficha ukweli kwa manufaa ya tabaka tawala na kuinyima jamii haki. Vilishinikizwa na kumtosa mtu makini na kumfanya aonekane ni msaliti.

Meya aliinyima jamii ukweli kwa masilahi ya kundi lake, hivyo kuwa ndiye adui wa ukweli. Aliunda kundi la wanamtandao masilahi dhidi ya ukweli. Hilo lilithibitisha kuwa hakufurahishwa na ukweli huo.

Taswira inayotolewa na tamthilia hiyo si ngeni kwa Tanzania ya leo ni kiasi tu cha kurejea kwenye hoja zinazotolewa na baadhi ya wabunge zinadhihirisha kuwepo kwa mwangwi wa hali hiyo.

Miongoni mwa hoja zilizowasilishwa zikiwa hoja binafsi zimekuwa zinakumbana na  ukinzani mkali jambo ambalo limekuwa likiaminisha jamii kuwa wale wanaotoa hoja hizo ni ‘maadui wa watu’.

Pingamizi ambazo mara nyingi zimekuwa zikiwekwa kupinga baadhi ya hoja  zimekuwa hazitofautiani na ukweli wa ugunduzi uliofanywa na Dk. Stockman  ambaye alielezea ukweli lakini akaitwa ni mwongo.

Taswira zinazojitokeza kwenye tamthiliya na riwaya yenyewe ipo katika jamii hivi sasa. Haishangazi hivi sasa kuona kuwa wale wanaoeleza ukweli wakikwamishwa kwa kauli zisizo na mashiko, au kupitia propaganda hasi zinazolenga kukwamisha jamii.

Wavuja jasho wanaobebwa na mtindo wa kusikiliza wamekuwa wanasombwa na wimbi la kelele za kushangilia bila kujua kuwa wangeangalia wangebaini wanaowahubiria baadhi wamevaa vilemba vya kina Nanga na Meya.

Mazingira ya aina hiyo ndiyo yamekuwa yanadhihirisha kwamba jamii inaweza kukubali kuendeshwa kwa upotovu na kuwaacha walio na uongofu na baadaye wanapokuja kuubaini ukweli wanakuwa tayari wameshalia na kusaga meno.

Hali hiyo inamaanisha kwamba wakati mahudhurio katika kampeni za uchaguzi mkuu zikiwa zimeshamiri itakuwa sahihi kuweka katika mizania kwa kusikiliza na kuangalia uongofu wa Odili na Dk. Stockman na kuukataa upotovu wa kina Nanga na Meya.

The post Tuangalie uongofu, tukatae upotovu appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *