img

Naibu Rais Kenya awavaa wanaompinga Jubilee,on September 10, 2020 at 6:59 am

September 10, 2020

NA ISIJI DOMINIC TARATIBU siasa za majukwani zinaanza kurudi Kenya baada ya kusimama kwa muda mrefu kutokana na janga la virusi vya corona. Ni dhahiri katika majukwaa hayo ya siasa kinachotawala zaidi ni uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 na ripoti ya Building Bridges Initiative (BBI). Vitu hivi viwili vimegawa wanasiasa licha ya mirengo yao ya
The post Naibu Rais Kenya awavaa wanaompinga Jubilee appeared first on Gazeti la Rai.,

NA ISIJI DOMINIC

TARATIBU siasa za majukwani zinaanza kurudi Kenya baada ya kusimama kwa muda mrefu kutokana na janga la virusi vya corona.

Ni dhahiri katika majukwaa hayo ya siasa kinachotawala zaidi ni uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 na ripoti ya Building Bridges Initiative (BBI). Vitu hivi viwili vimegawa wanasiasa licha ya mirengo yao ya vyama vya siasa.

Huku zikiwa zimebaki miaka miwili kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini Kenya, kuna dalili ya kuibuka miungano mipya ya kisiasa hususan kutokana na kile kinachoonekana kuendelea ndani ya vyama vya siasa.

Sasa ni wazi kuwa hali si shwari katika muungano wa vyama vya upinzani, NASA, kufuatia tukio la Machi 9 mwaka 2018 lililomkutanisha Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Chama cha ODM, Raila Odinga.

NASA kimesambaratika hata kama viongozi wao wanasisitiza wako pamoja. Kama hiyo haitoshi, ndani ya vyama vinavyounda NASA navyo vimevurugana. Wiper hapajatulia Ford Kenya hakukaliki na Amani National Congress kunafukuta.

Hata pia katika chama tawala, Jubilee, kuna msuguano unaohatarisha uhai wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. Wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto wanataka makubaliano yaliyofikiwa kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2013 yaheshimiwe.

Wanadai kuwa makubaliano hayo yalikuwa Rais Uhuru atawale kwa miaka 10 kisha amuunge mkono naibu wake. Lakini kinachoonekana ni mvutano hususan baina ya wanachama wanaomuunga mkono Rais Uhuru na wale wanaomuunga mkono Naibu Rais Ruto.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, David Murathe, amekuwa akinukuliwa mara kwa mara akimpinga Ruto kuwania urais 2022 huku akimuunga mkono Raila. Aidha Murathe amekuwa akimtaka Ruto anayedai anatofautiana na Rais Uhuru pamoja na wale wote wanaomuunga mkono kuhama chama.

Katika kile kinachoonekana hana mpango wa kuhama chama tawala, Naibu Rais Ruto amewataka kundi la viongozi wa Jubilee ambao wanamshabikia viongozi wa vyama vingine vya kisiasa kujiuzulu nyadhifa zao na kuondoka.

Kutokana na kupigwa marufuku mikutano ya hadhara ya siasa, Ruto amekuwa akikutana na viongozi wa siasa na dini na alitamka maneno hayo hivi karibuni akiwa katika maeneo bunge ya Nyali na Mvita.

Alisema ni jambo la upuuzi kuwa baadhi ya viongozi wa chama cha Jubille wameamua kumuunga mkono mgombea mpinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

“Wale ambao wapo Jubilee na wameamua kuwa mgombea wao anatoka chama cha ODM ni bora wafungashe virago vyao na kuondoka; nini ambacho bado wanakifanya katika ofisi kuu ya chama chetu?” alihoji Ruto.

Naibu Rais alisema hajatetereka na nguvu hasi inayotokana na mawakala wa kisiasa ambao hawamtaki yeye kuwania urais.

“Tuko tayari na ngangari kwa mbio za urais 2022 na tunabebwa na rekodi nzuri ya maendeleo, masuala na sera ambayo yataifanya nchi yetu kuwa pahali pazuri kwa kila mtu,” alisema Ruto aliyeongozana kwenye mkutano huo na wabunge.

Mohamed Ali (Nyali), Benjamin Tayari (Kinango), Lydia Haika (Mwakilishi wa Wanawake, Taita Taveta), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Wangui Ngirici (Mwakilishi wa Wanawake, Kirinyaga) Gladys Sholei (Mwakilishi wa Wanawake, Uasin Gishu) na Kimani Ichungwa (Kikuyu).

Naibu Rais aliwataka viongozi wa Jubilee kusimama imara kufuatia vitisho vikali na kulazimishwa huku akisisitiza huo sio muda wao wa thamani na akaongeza kwamba Jubilee imedhamiria kuunganisha nchi zaidi.

Alisema hiyo itasaidia kuondoa chuki ya kikabili na mgawanyiko ambayo imerudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa miongo mingi.

Naibu Rais aliwataka viongozi kuepuka kurudia njia ya kizamani ya kufanya siasa akisema hali hiyo, ina hatari ya kuipotosha nchi na badala yake kuwataka viongozi kukumbatia siasa zinazolenga maendeleo.

Ziara ya Ruto mkoani Pwani ni sehemu ya kutaka kuungwa mkono katika azma yake ya kuwania urais 2022 na huku kukiwa na shauku ya Katiba kufanyiwa marekebisho kutokana na ripoti ya BBI, Mbunge wa Nyali, Ali, aliwashutumu wale wanaoshabikia marekebisho ya Katiba akisema hilo sio suala la msingi wakati huu Kenya inapambana na umasikini na ukosefu ya ajira iliyochangizwa na mlipuko wa virusi vya corona.

“Katiba yetu ina ubaya gani hadi ihitaji kufanyiwa marekebisho haraka? Shida zetu zimejikita katika ufisadi na hapo ndipo nguvu yetu inapaswa kuelekezwa,” aliongezea Hassan Omar aliyekuwa Seneta wa Mombasa.

Naye Mbunge wa Lunga Lunga, Mwashetani, alisema viongozi wa eneo la Pwani watakuja na chama chao cha siasa ambacho lengo lake kuu ni kuelezea changamoto zinazokumba watu wa eneo hilo.

“Ni chama kipya ambacho tutakitumia kutengeneza muungano thabiti na Naibu Rais wakati anasaka kuwa Rais wa tano wa nchi yetu,” alisema Mwashetani.

Naibu Rais Ruto ambaye amekuwa akisisitiza chama cha Jubilee bado kiko imara ametaka Serikali iwe na msimamo moja linapokuja suala la vita dhidi ya ufisadi na hii inatokana na Mamlaka ya Usambazaji Dawa Kenya (KEMSA), kushutumiwa kutoa zabuni pasipo kufuata taratibu.

Ruto alisema laiti mabosi wa KEMSA wangekuwa marafiki zake wangekuwa wameshakamatwa na kufunguliwa mashitaka.

“Wahusika wa sakata hilo wana bahati kubwa hawabebi nembo ya ‘marafiki wa Ruto’, la sivyo wangekuwa wameshawajibika kisiasa, kujiuzulu, kuandikisha taarifa, makampuni kuchunguzwa, wahusika kukamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema Naibu Rais.

Bado washirika wa Ruto wana kumbukumbu ya namna aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu alivyotolewa ofisini baada ya kuchunguzwa na kushtakiwa kwa ufisadi licha ya Ruto kumtetea hadharani na kupuuza shutuma zote za ufisadi.

Katika kile kinachoonekana kumjibu Ruto, mshirika wa karibu sana na Raila ambaye pia ni Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed, alimtaka Naibu Rais kuacha kuandika katika mtandao wake wa kijamii kuhusu ubadhirifu wa fedha za Covid-19 na badala yake awasilishe ushahidi kuhusu ufisadi kwa wapelelezi.

“Namshauri awasilishe ripoti kwa DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai) na EACC (Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi) au kituo chochote cha polisi,” alisema Junet ikiwa ni kumkingia kifua bosi wake katika chama cha ODM, Raila, ambaye Ruto anamshutumu kutetea ufisadi.

Lakini kwa Ruto, jukumu lake sasa akiwa Naibu Kiongozi wa Chama cha Jubilee ni kujiimarisha ili aweze kuwania urais kupitia chama tawala katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Makamu Mwenyekiti wa Jubilee, Murathe, anamtaka yeye na wenzake waondoke lakini sasa Naibu Rais ndiye anayemtaka Makamu Mwenyekiti huyo kutimka.

Nguvu aliyoipata Ruto ni kutokana na Murathe ambaye licha ya kuwepo ndani ya chama tawala, ameonyesha wazi kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Raila, kumrithi Rais Uhuru.

The post Naibu Rais Kenya awavaa wanaompinga Jubilee appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *