img

Ilani za vyama na vipaumbele vya maendeleo ya watu,on September 10, 2020 at 9:10 am

September 10, 2020

NA FREDERICK FUSSI JUMA lililopita tulipata fursa ya kuangazia na kuchambua ilani za vyama vitatu vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka huu  ambavyo ni CCM, Chadema na ACT-Wazalendo. Katika utangulizi tulitoa maana ya neno ilani kuwa ni tangazo ambalo lipo bayana juu ya masuala ya kimaendeleo ambayo endapo chama kitachaguliwa,
The post Ilani za vyama na vipaumbele vya maendeleo ya watu appeared first on Gazeti la Rai.,

NA FREDERICK FUSSI

JUMA lililopita tulipata fursa ya kuangazia na kuchambua ilani za vyama vitatu vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka huu  ambavyo ni CCM, Chadema na ACT-Wazalendo.

Katika utangulizi tulitoa maana ya neno ilani kuwa ni tangazo ambalo lipo bayana juu ya masuala ya kimaendeleo ambayo endapo chama kitachaguliwa, kushinda uchaguzi na kuunda Serikali basi watatumia ilani kutengeneza mipango ya maendeleo kwa ajili ya watu.

Katika uchambuzi wa leo tutaangazia maeneo ya ilani za vyama hivi ili kuona namna zilivyoainisha masuala ya maendeleo ya watu na wao endapo wakichaguliwa kuunda Serikali watafanya nini.

ILANI YA CCM JUU YA MAENDELEO YA WATU

Sura ya pili yote ya ilani ya CCM inazungumzia maendeleo ya watu katika sura iliyopewa kichwa cha habari kuwa “mapinduzi ya uchumi kwa maendeleo ya watu” Sura hii ya pili pekee imesheheni kurasa 115. Sura inaanzia ukurasa wa 9 hadi 124, huku maelezo ya uchambuzi wao kuhusu maendeleo ya watu ukiwa umewekwa katika aya zenye nambari, jambo ambalo linawezesha usomaji wa rejea na wenye mtiririko unaoeleweka. Katika aya ya 12, CCM wanasema kuwa wanaendelea kutambua umuhimu wa kujenga uchumi wa kitaifa ili kuhakikisha kwamba Watanzania ndio wanufaika wakuu wa uchumi na maliasili za nchi.

Katika muktadha huo, CCM kwenye ilani yake ili iweze kujenga uchumi wa kunufaisha Watanzania wao wadai kuwa watajikita katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda  na uchumi fungamanishi, jumuishi na shindani unaotumia sayansi na teknolojia za kisasa na ambao unahimili utandawazi na unaoweza kutumia kikamilifu fursa zake kwa kuuza zaidi bidhaa za viwandani na bidhaa nyingine nje ya nchi.

Kwa mantiki hii CCM wanaamini kuwa ili kuleta maendeleo kwa watu hakuna budi kuendeleza viwanda, kukuza uzalishaji wa kisasa kabisa, kuongeza ajira na hatimaye kuuza bidhaa kwenye maskoko na ushindani ndani nje ya nchi. Katika aya ya 14 CCM inasema kuwa inathamini na kutambua mchangowa sekta binafsi katika kujenga uchumi wa kitaifa na wenye ushindani, huku wakionelea kuwa ni vema sekta binafsi ikajikita kwenye uzalishaji wa bidhaa za viwandani hususani katika sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii na sekta nyingine zote.

CCM imetoa ahadi kubwa sana kwa sekta binafsi ambazo kama itachaguliwa imekusudia kutekeleza ahadi hiyo ya kampeni na ilani ya uchaguzi. Wao wamesema kuwa na nitanukuu kuwa “CCM itaendelea kusimamia serikali zake kuhakikisha sekta binafsi inalindwa na kuendelezwa na kwamba haki ya kila mtu, kikundi, ushirika na kampuni ya kuendesha shughuli za uchumi na biashara kwa uhuru na kwa mujibu wa sheria zinalindwa wakati wote.” Masuala mawili ambayo CCM itasimamia kwenye sekta binafsi kama ilivyoahidi ni uhuru wa watu kufanya shughuli za kiuchumi na biashara lakini pia kwa kufuata sheria”

Katika aya ya 17 kipengele cha (x), CCM imeiahidi sekta binafsi na Watanzania wafanyabiashara kuwa itajikita kwenye kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve Business Environment) kwa kutatua changamoto zinazokabili uwekezaji na ufanyaji biashara.

Ili kufanikisha haya yote kutokea CCM kwenye ilani yao wanadhani kuwa ipo misingi mikubwa mitano, ambayo itaweza kusimamisha nguzo za ujuzi wa mapinduzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.

Misingi hiyo imetajwa kwenye aya ya 14 kuwa ni uwepo wa amani na usalama, utawala wa sheria na utulivu wa kisiasa, mwenendo tulivu wa uchumi mpana (macroeconomic stability); ubora wa miundombinu na huduma wezeshi kama vile uchukuzi, nishati na mawasiliano; urahisi, ufanisi na uhakika wa sheria, kanuni, taratibu na utendaji wa sekta ya umma katika kuwezesha shughuli za uchumi na biashara za sekta binafsi na uwepo wa rasilimali watu ya kutosha yenye elimu, ujuzi na maarifa stahiki hususan katika nyanja za sayansi na teknolojia.

Ilani hiyo pia kwenye aya yake ya 15 inadai kuwa kuna sekta za uchumi na biashara ambazo endapo sekta binafsi itashindwa kuwekeza basi Serikali ya CCM itaweza “kujihusisha moja kwa moja kwenye shughuli za uchumi na biashara za kimkakati na zile ambazo sekta binafsi haijaweza kujihusisha nazo kwa ufanisi au haivutiwi kuwekeza.”

Ni katika sura hii hii ya pili ambapo Ilani ya CCM imechambua viashiria mbalimbali vya uchumi kwa kuelezea hali ya uchumi wa nchi ilivyo. Viashiria vya uchumi vilivyobainishwa ni ukuaji wa pato la Taifa kwa asilimia 6.9 kati ya mwaka 2016 na 2019, pato la wastani kwa kila mtu kutoka milioni 1.9  (Dola za Marekani 992) mwaka 2015 mpaka kufikia Dola za Marekani 1,086 sawa na Sh milioni 2.4 mwaka 2018.  Hilo ni sawa na ongezeko la dola 94 kwa miaka mitatu yote tangu 2015 mpaka 2018 na ni sawa na ongezeko la dola 31.3 kwa mwaka.

Kwa fedha za Kitanzania ongezeko hilo la pato la wastani kwa kila mtu ni sawa na ongezeko la Sh 489,531 kwa miaka mitatu na Sh 163,177 kila mwaka. Wastani wa miaka ya kuishi kuongezeka kutoka miaka 61 mwaka 2015 mpaka miaka 65 mwaka 2020, usambazaji wa umeme vijijini kuongezea kutoka asilimia 16.4 mwaka 2015 mpaka asilimia 67.1 mwaka 2019. CCM kwenye ilani yao wanahitimisha kutaja viashiria vya uchumi kwa kuzungumzia hali ya umasikini wakisema kuwa umasikini wa mahitaji ya msingi umepungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 mpaka asilimia 26.4 mwaka 2017/18, pia wakisema kuwa umasikini wa chakula umepungua kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011/12 mpaka asilimia 8.0 mwaka 2017/18. Takwimu hizo za umasikini pamoja na kuvutia kwake bado sio takwimu za siku za hivi karibuni kama mwaka 2019 au 2020.

Aya ya 23 ya Ilani ya CCM inazungumzia masuala ya Kupambana na Umasikini na Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Katika aya hiyo CCM imesema kuwa tayari ilifanya miradi takribani kumi ya ujasiriamali kwa ajili ya vyama vya ushirikia kwenye kilimo, upatikanaji wa mikopo yenye riba naafuu kwa wajasiriamali wanawake zaidi ya 3000 nchi nzima kwenye mikoa 26 ya Tanzania bara, halmashauri 185 kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 93.3 katika Mfuko wa kuwawezesha Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu huku wanufaika wakiwa takribani vikundi vya wajasiriamali 32,553. Ni katika aya ya 26 CCM imetoa ahadi 14 kwa ajili kuendeleza miradi ya kuwezesha wananchi kiuchumi. Aya ya 27 wamezungumzia masuala watakayofana kwenye uchumi wa rasilimali za maji (Blue Economy) na  aya ya 28 ilani hiyo imezungumzia ahadi za kutumia fursa za kijiografia za nchi yetu kuchochea maendeleo. Katika aya ya 32 CCM wameachambua jinsi watakavyoongeza fursa za ajira milioni 7 kupitia ahadi 19 za fursa kwenye halmashauri, uwekezaji kwenye misitu, programu za kujitolea, atamizi za ubunifu, mifuko ya hifadhi ya jamii, SACCOSS na makampuni.

ILANI YA ACT-WAZALENDO JUU YA MAENDELEO YA WATU

Kwenye ilani ya ACT-Wazalendo wao sura yote ya nne imezungumzia mada ya uchumi wa watu wakimaanisha maendeleo ya watu ni uchumi wao. ACT-Wazalendo katika sura hii ambayo wao wanaiita sura ya uchumi wa watu, ina maeneo 12 ambayo ilani yao imetamka bayana endapo watashinda uchaguzi na kuunda Serikali basi wataweza kufanyia maendeleo gani wananchi. Sehemu ya kwanza ni biashara yenye tija na endelevu, ajira ikiwa sehemu ya pili, ya tatu ni masuala ya michezo, sanaa na burudani, huku suala la nne likiwa ni kilimo, mifugo na uvuvi. Jambo la tano wanalosema watafanya ni kujenga utajiri wa jamii kupitia ushirika wa kisasa, jamo la sita ni ardhi kwa maendeleo ya watanzania, saba ni kujenga miundombinu wezeshi, nane ni viwanda vya zana za usindikaji na tisa ni utajiri kwenye maliasili na kumi ni miradi ya kimkakati na kumi na moja ni kulinda mazingira na kumi na mbili wamezungumzia masuala ya sera za kodi. Hayo ndio masuala yote kwa ujumla ambayo ACT-Wazalendo imeya-ainisha kwenye ilani yake kuwa ndio yanaunda uchumi wa watu ndani ya takrabani kurasa 14, kati ya ukurasa wa 28 mpaka ukurasa wa 42 wa ilani yao ya uchaguzi.

Kuhusu bishara zenye tija endelevu ACT-Wazalendo imetoa ahadi 11 kwa wafanyabiashara. Wanasema kuwa wao wataondoa urasimu kwenye uanzishwaji na uendeshaji wa biashara, kutambua na kurasimisha biashara zilizo nje ya mfumo rasmi, mazingira mazui ya kisera ya kufanya biashara, udhamini na mikopo kwa biashara chipukizi, kuwalinda wafanyabishara wa ndani, diplomasia na mahusiano ya kimkakati na kuhamasisha uwekezaji wa ndani viwandani. Ahadi nyinginezo kwa wafanyabishara ni kuwauzia Watanzania hisa hadi asilimia 51 ya makampuni yanayomilikiwa na Serikali na kupitia mifumo yote ya kodi ili wafanyabishara wasilipe kodi kabla ya kuanza biashara.

Kuhusu ajira wao ACT-Wazalendo wamebainisha watazitoa wapi ajira milioni 10 wanazosema watazalisha. Wao wanasema kuwa watazalisha ajira “zenye tija milioni kumi (10) ndani ya miaka mitano. Ajira million tano (5) kutoka kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo, ajira million 2 kutoka sekta rasmi na ajira milioni 3 kutoka sekta isiyo rasmi. Kwenye kipengele hicho cha ajira wametoa ahadi takribani saba. Kuhusu ahadi ya kujenga Utajiri wa Jamii kupitia Ushirika wa kisasa, wao wanatoa ahadi nne kuwa wataweka mazingira ya kisera na kuwekeza katika ushirika utakaomilikiwa na wanaushirika kwa ajili ya maendeleo yao, wataweka mazingira ya kisera na kisheria kuunganishwa kwa wakulima, wavuvi na wafugaji na masoko makubwa ya nje ya nchi kupitia vyama vyao vya ushirika na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo. Pia wanasema kuwa wataondoa unyonyaji unaofanywa na madalali (middlemen) kwenye soko la mazao, na kuwa pale ambapo madalali ni lazima kwa sababu za kihistoria, kiuchumi na kimazingira, Serikali itahalalisha udalali wa asili kwa kuurasimisha.

ILANI YA CHADEMA JUU YA MAENDELEO YA WATU

Wao Chadema wanasema kuwa ilani yao ni ilani ya uhuru, haki na maendeleo ya watu. Chadema wameahidi kuwa wakichaguliwa kwenye uchaguzi huu na kuunda Serikali chama cha kitaisimamia Serikali “kujenga uchumi shirikishi wenye kulenga maendeleo ya watu na kama maendeleo ya vitu basi yawe yale yenye kuimarisha uwezo wa wananchi walio wengi kujiletea maendeleo wenyewe bila kufanywa watumwa wa vitu au watwana wa watu wengine”. Hii maana yake ni kuwa ukiisoma ilani ya Chadema msingi wake ni kwenye masuala ya uhuru, haki na mendeleo ya watu. Ilani hii haina sura maalum inayozungumzia maendeleo ya watu isipokuwa maendeleo ya watu yamezungumziwa angalau kwenye kila sura ya ilani hiyo.

Sura ya nne inazungumzia kujenga na kumiliki uchumi imara na shirikishi,  sura ya tano imezungumzia elimu bora kwa maendeleo ya endelevu, sura ya sita imezungumzia masuala ya afya, hifadhi na huduma za jamii, sura ya saba imezungumzia ardhi, maji, mipango miji, nyumba na maendeleo ya makazi na sura ya nane imezungumzia masuala ya kujenga kilimo, uvuvi na ufugaji. Sura ya 13 imezungumzia masuala ya viwanda.

Ukirejea sura ya 6 kipengele cha 6.4 kinazungumzia masuala ya fursa za ajira na ujira bora kwa vijana. Kwenye kipengele hicho tofauti na ilivyokuwa ilani ya ACT-Wazalendo na ile ya CCM zilizosema bayana kiasi cha ajira watakachozalisha, wao Chadema ilani yao kwenye kipengele hicho haikutaja bayana itazalisha ajira kiasi gani isipokuwa ilani yao imezungumzia ahadi 8 ambazo Serikali yao itaweza kufanya endapo chama hicho kitashinda uchaguzi; itatoa na kuimarisha elimu ya ufundi na stadi za kazi mashuleni, ili hatimaye mwanafunzi atakapohitimu masomo yake anakuwa na uwezo wa kujiajiri kwenye fani ya ufundi na uongezaji wa thamani kwa mazao ya
kilimo badala ya kusubiria ajira rasmi kutoka serikalini. Pia wanasema kuwa watahakikisha kunakuwepo na mashamba yenye miundombinu ya umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha
mboga mboga ili vijana waweze kujihusisha na kilimo. Wanaongeza kuwa wataweza kujenga viwanda vya kuchakata mazao katika kila Mkoa na hata wilaya, viwanda hivi vitasaidia kuongeza fursa za ajira na kuongezea thamani mazao ya wakulima. Pia wamesema kuwa kupitia upya mfumo wa ujira ili kuhakikisha kuwa waajiriwa wanapata ujira unaokidhi mahitaji ya maisha kama vile nyumba, chakula na mavazi.

Pia wamesema kima cha chini cha mshahara lazima kimwezeshe mfanyakazi kuweka akiba isiyopungua asilimia 5 ya ujira wake, hili litaenda sambamba na Kuweka uwiano mzuri wa mishahara kati ya kima cha chini na juu na kupunguza kusigana baina ya mishahara. Kuhusu kodi ya mapato kwa wafanyakazi wamesema kuwa wataweza kupunguza tozo kwenye mshahara (PAYE) na kuwa si zaidi ya asilimia 8. Aidha serikali yao itahakikisha kuwa makato anayokatwa mfanyakazi kama vile kulipia madeni ya Bodi ya Mikopo,Bima ya Afya, mifuko ya hifadhi ya jamii na mengineyo hayatazidi asilimia 30% ya mapato ghafi ya mfanyakazi. Wamesema pia endapo wakichaguliwa Chadema itaweka utaratibu kwa kila Halmashauri nchini kuwa na kanzi data ya vijana kuweza kujiandikisha juu ya taaluma zao na hivyo kuwa na senta moja ya utambuzi wa vijana ambao hawana ajira na pindi fursa itakapopatikana kulingana na uwezo na au taaluma ya kijana husika wataweza kujulikana na kuajiriwa, na hii itaondoa upendeleo na kujuana katika kutoa ajira kwani wataajiriwa kulingana na sifa na yupi alitangulia kujiandikisha.

Mwisho kwenye eneo la ajria kwa vijana wamesema kuwa Chadema itaweka utaratibu wa kisheria kwa ajili ya taasisi zote za fedha zitakazokuwa zinatoa mikopo kwa masharti nafuu kwa vijana kupatiwa motisha na serikali kama vile kupunguziwa baadhi ya kodi au ushuru kwa lengo la kuziwezesha kuwa na mitaji mikubwa ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika na mikopo husika.

The post Ilani za vyama na vipaumbele vya maendeleo ya watu appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *