img

Wagombea waseme watakachoifanyia nchi,on September 3, 2020 at 6:56 am

September 3, 2020

NA ALOYCE NDELEIO  WAKATI kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu zikiwa zinaendelea yapo mambo mengi ambayo yamejitokeza na hivyo kujenga taswira ya kwamba Tanzania ya leo si ile ya jana wala juzi. Dhana hiyo inajionesha kuwa katika misingi wa kuiangalia mioyo iwapo ina uzalendo katika kuongoza, pamoja na kutetea masilahi ya
The post Wagombea waseme watakachoifanyia nchi appeared first on Gazeti la Rai.,

NA ALOYCE NDELEIO 

WAKATI kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu zikiwa zinaendelea yapo mambo mengi ambayo yamejitokeza na hivyo kujenga taswira ya kwamba Tanzania ya leo si ile ya jana wala juzi.

Dhana hiyo inajionesha kuwa katika misingi wa kuiangalia mioyo iwapo ina uzalendo katika kuongoza, pamoja na kutetea masilahi ya umma au imo katika kuangalia migongano ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Hali hiyo inatokana na kigezo kwamba kumekuwepo mizani ya kuangalia iwapo viongozi kwa sasa wanataka kutumikiwa au kutumikia na katika mazingira hayo ni dhahiri lipo swali ambalo mvuja jasho huwa anajiuliza, “Nitaifanyia nini nchi yangu?”

Wakati akiwa anajiuliza hivyo wengine wanaegemea kwenye kinyume chake na kuwa ni nitafanyaje niweze kuneemeka, kujitajirisha na kuonja pepo ambalo ni, “Nchi yangu itanifanyia nini?”

Mazingira ya Tanzania ya juzi, ilikuwa inajionesha dhahiri kuwa maana ya chama cha siasa ilikuwa ni kujenga na kuimarisha sera kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya jamii ya kiuchumi na kisiasa na hata kiutamaduni.

Kinyume cha hali hiyo leo hii chama cha siasa au kujiingiza kwenye siasa na kwa kutumia chama kumekuwa ni kutumia chama kama jiwe la kuvukia mto kufuata madaraka iwe kwa njia zinazokubalika au zisizokubalika na kwa maana hiyo dhana kuwa wavuja jasho watakuwa wamepata mtetezi inatoweka na kuwa na badala yake kuwa jasho lao kuvunwa.

Katika kudhihirisha hali hiyo na kuona kukengeuka kulikokuwa kunajitokeza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage  Nyerere, alikwishaliona hili mapema kwa upande  CCM akionesha dhahiri ni nani wenye chama.

Alisema kwamba, CCM kimekuwa chama cha viongozi badala ya kuwa chama cha wanachama kwa maana kuwa wenye chama hawakuwa tena wakulima na wafanyakazi.

Kutokana na kuchukizwa na hali hiyo alisema kwa ghadhabu,  “Chama mimi si mama yangu.  Kwangu mimi chama ni sera…chama kile  (CCM) kikiziacha shabaha zile na mimi natoka… mimi sio mwenzenu tena.  Leo nawaeleza ukweli tu.”

Haiyumkini kwamba pindi chama kinapotekwa na matajiri taswira inayojitokeza ni kwamba utajiri unanunua demokrasia  na moja kwa moja haki  za wavuja jasho zinanunuliwa.

Kwa maana hiyo pindi ambavyo watu wamekuwa wakijikomba na kuwa wakereketwa, wafurukutwa sio kwamba wanasukumwa na uzalendo bali wanavutwa na harufu ya mnuso ulio mbele yao ambao ni keki ya taifa kwamba waweze kuifikia kwa urahisi, waanze kuvuna jasho.

Lakini wakati kampeni zikiwa zinaendelea zipo hoja nyingi zitakazowasilishwa kwenye mikutano ya hadhara na nyingi zitakuwa ni chanya na hata hivyo hasi hazitakosekana.

Pamoja na hali hiyo, inakuwa ni fursa kwa wanaohudhuria kampeni hizo kutafakari na kufanya rejea kwani kila mmoja anaweza kuwa na mchango wake ambao atakuwa ameutoa kwa nchi kupitia maneno, mawazo na hata matendo na hivyo inakuwa ni busara kuyaangalia na kuyafanyia tafakuri ya kina.

Inakuwa ni fursa ya kuangalia na kumengenyua kwani jambo lililodhahiri ni kwamba katika uchaguzi Rais atapimwa uwezo wake wa kuongoza kwa jinsi anavyokabiliana na maovu yanayotishia kuliangamiza taifa na kama atajionesha katika kujinadi kwamba anayo taswira ya kufumbia macho, basi hafai kuwa mpangaji namba moja ya nchi hii.

Mwalimu Nyerere alikuwa na kauli nzuri ya ushauri wa kuongoza ambapo alisema, “Serikali ya wala rushwa ( hapa alitumia neno la Kiingereza corrupt), inawafanyia kazi wenye mali.  Tunataka kiongozi ambaye atasema rushwa kwangu ni mwiko na watoa rushwa watajua hivyo…Ikulu hapawezi kuwa pango la walanguzi.”

Ni wazi kampeni ni jukwaa la kuomba ajira na baada ya uchaguzi wanaoshinda wanakuwa wameingia mkataba ambao ni kati ya wanaoongoza na wanaoongozwa na jambo linalofuata kuutii mkataba kwa kujenga uwiano kati ya pande hizo mbili.

Kinachotarajiwa ni kuona kuwa kitakachopatikana kinawaridhisha wote na kutoa taswira ya jinsi wanaoongoza wanavyotakiwa kuongoza na wanaoongozwa wanavyotaka kuongozwa.

Kwa bahati nzuri haijawahi kutokea kwamba wale waliochaguliwa kufikia hatua ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani baada ya wapiga kura  kutoridhishwa na uongozi wao.

Hata hivyo wapo viongozi wanaochepuka kutoka kwenye reli kwa kusakamana kwa kejeli na mipasho kwa kutumia nguvu kubwa isiyo na tija jambo ambalo linaweza kuungwa mkono na wafurukutwa ambao  wengine  huingia katika ushabiki kwa ajili ya kuchumia tumbo kuliko hoja zenye mashiko.

Kwa kuwa wengi hupambisha moto upambe wao na kujinasibu ambako kunaondosha ladha ya yale muhimu kunasababisha baadhi ya hoja kugeuka kuwa ni kioja.

Baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuwa ni vioja yanakuwa ni yale ya kulazimisha ama kwa kauli za vitisho kwenye hadhara ambayo yanakuwa mbali na dhana halisi ya demokrasia na badala yake kuleta harufu ya udikteta mamboleo.

Baba wa taifa aliwahi kutoa kauli nyingine akisema, “Lazima tutumie demokrasia kuhitilafiana mawazo na lazima tuseme tunahitilafiana kwa nini.”

Katika changamoto za kuhitilafiana wengi wanashindwa kuonesha uvumilivu.  Hapa ndipo zinapotokea kauli za kejeli zisizo na mashiko dhidi ya hoja zenye mashiko na zenye rejea za msingi na hususani zilizoandikwa na wasomi wote wa ndani na nje.

Changamoto hizo ndizo zinazonesha dhahiri na ni kwa namna gani baadhi ya wapambe, mashabiki na hata wafia vyama wanavyoweza kuonesha kwamba badala ya kujikita katika mwelekeo wa nini cha kuifanyia nchi wanachepuka.

Katika mchepuko huo huwa wanasombwa na wimbo mzuri wa mpiga filimbi wa Hamelini na kuwasahau wenye nyumba ambao ni wananchi.

The post Wagombea waseme watakachoifanyia nchi appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *