img

Sauti ya Askofu Mameo kuhusu amani ya kinabii,on September 3, 2020 at 7:35 am

September 3, 2020

NA VICTOR MAKINDA KUSIKIA sauti ni jambo moja na kufanyia kazi kile ulichokisikia ni jambo jingine. Kusikia tu hakutoshi, msingi ni nini unasikia na hatua gani unachukua baada ya kusikia. Waarabu wana msemo usemao ‘Kila kichwa kina hekima’. Naam, vipo vichwa vyenye hekima nyingi. Binadamu tumejaliwa karama tofauti tofauti. Karama ya kila mmoja ina mchango 
The post Sauti ya Askofu Mameo kuhusu amani ya kinabii appeared first on Gazeti la Rai.,

NA VICTOR MAKINDA

KUSIKIA sauti ni jambo moja na kufanyia kazi kile ulichokisikia ni jambo jingine. Kusikia tu hakutoshi, msingi ni nini unasikia na hatua gani unachukua baada ya kusikia. Waarabu wana msemo usemao ‘Kila kichwa kina hekima’. Naam, vipo vichwa vyenye hekima nyingi.

Binadamu tumejaliwa karama tofauti tofauti. Karama ya kila mmoja ina mchango  kwa maisha ya mwingine. Naam, Biblia inasema ‘kila mmoja ni kiungo kwa mwingine’. Ili kuwa kiungo kwa mwingine unapaswa kuenenda na kutenda kwa kuzingatia masilahi ya wengine na kutokuwa kikwazo katika ustawi wa maisha ya wengine.

Makanyo, maono na maonyo ni masuala muhumu ya kuzingatiwa katika ustawi wa jamii staarabu. Ukweli ulivyo wapo  miongoni mwetu katika jamii zetu wenye uwezo mkubwa wa kuona viashiria vya hatari.

Hawa huweza kuona mapema jambo litakalotokea liwe baya au zuri na huwa hawaishii tu kuona bali hutamka hadharani ili kuwaacha watu wakiwa wanajua nini kitakachotokea. Hufanya hivyo kwa mintaarafu ya ama kuonya  ili  tahadhari  ichukuliwe au kujiandaa kwa ujio wa jambo au tukio jipya.

Watu walio na karama hizo zamani zile walikuwa wanaitwa manabii.   Ukweli ulivyo manabii wangalipo hata sasa kwa kuwa karama za kuwa na maono ya mambo yajayo iwe ni mazuri au mabaya bado zipo miongoni mwetu.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo, amenena sauti ninayodiriki kuiita ni ya kinabii. Naam, Askofu Mameo Jumapili ya wiki iliyopita, akihutubia katika ibada ya ufunguzi wa nyumba ya Mchungaji Usharika wa Lungo, Turiani Morogoro, ameona na kuonya juu ya uwezekano wa vurugu kutokea hapa nchini, ikiwa wanasiasa watafanya siasa za matusi na kuendekeza rushwa katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

“Wito wangu kwa wanasiasa wote nchini, hiki ni kipindi cha kampeni za uchaguzi. Ni kipindi muafaka cha kunadi sera za vyama vyao. Ni kipindi ambacho wanasiasa wanapaswa kueleza nini watawafanyia Watanzania.

“Sio kipindi cha kutukanana na kuchochea vurugu.  Wanasiasa waseme nini wanataka kuwafanyia watu kwa ajili ya kuwakwamua watu hao katika lindi la umasikini. Matusi, kejeli na vurugu ni mambo yanayopaswa kuepukwa kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha amani ya Taifa letu,”alisema Askofu Mameo.

Askofu Mameo aliongeza kusema kuwa matusi na kejeli kwa watawala na wagombea wa vyama vingine kamwe haiwezi kuwa sera. Nchi yetu imekuwa ni kisiwa cha amani kwa miaka nenda rudi hivyo tunapaswa kuitunza amani hiyo kwa kufanya siasa za kistaarabu kwa kuepuka matusi.

“Ikiwa tutafanya siasa za matusi basi ni dhahiri kuwa  tunaweza kuingia katika vurugu ambazo zitaliteteresha Taifa letu na kuitikisa amani yetu. Kuna baadhi ya vyama vya siasa vimeonesha viashiria vya kutaka kuwachochoea wananchi kufanya vurugu, hatua hiyo inatakiwa kukemewa kwa nguvu zote kwani ikiwa Taifa likaingia katika sintofahamu watakaothirika zaidi ni akina mama na watoto huku wanasiasa hao wakitimkia kujificha nje ya nchi,”alisema.

Askofu Mameo aliwaonya wanasiasa kuitunza amani ya Tanzania kwa kutowadanganya na kuwarubuni wafuasi wao kufanya vurugu.

“Nchi yetu nzuri yenye sifa nzuri isiharibiwe kwa kauli na matendo ya wanasiasa wenye uchu wa madaraka ambao wako tayari kuingia Ikulu kwa kuogelea juu ya damu za watu. Ni vema kuhakikisha kuwa wanasiasa wanahubiri amani na sio uchochezi ambapo ikiwa tutaingia kwenye machafuko wanasiasa hao ndio huwa wa kwanza kukimbilia ughaibuni huku wakituacha wananchi wakawaida tukiuana. Tusikubali kugombanishwa kwa ajili ya siasa za vyama. Vyama vitapita Tanzania itabaki,”alisema Askofu Mameo kwa uchungu katika ibada hiyo huku akiahidi kuendelea kuliombea amani Taifa Tanzania.

Msomaji, wewe unaweza kuwa shahidi wa kile kinachoendelea nchini kwa sasa. Ni katika uwanja wa siasa na kampeni za uchaguzi zinazoendelea. Ukweli ulivyo tumeanza kushuhudia kauli ambazo zinaashiria kuwa huenda wapo waliojiandaa kwa ajili ya kuwachochea Watanzania kufanya vurugu.

Kwenye uwanja wa siasa kuna kushindwa au kushindwa. Yote hayo ni matokeo ya uchaguzi. Hivyo sio sahihi mgombea kuanza kuhamasisha wafuasi wake kujiandaa kudai ushindi hata kabla ya matokeo ya uchaguzi? Kwanini waaanze maandalizi ya kudai ushindi ilhali uchaguzi bado na matokeo ya uchaguzi yanaweza kuwa kushinda  au kushinda.?

Binafsi nikiamini kuwa nyuma yangu kuna mamilioni ya Watanzania wapenda amani, tunaipinga kauli ya yoyote ya kuchochea kuvunja amani yetu.

Askofu Mameo sauti yake ya kinabii iligusia na kusisitiza juu ya rushwa katika nyakati za uchaguzi. Alisema kuwa ni wazi wapo wanasiasa ambao wanaopokea na kutoa rushwa kushawishi wapiga kura ili wawachague hatua ambayo ni mbaya na inaweza kuzorotesha amani ya nchi.

“Rushwa ni adui wa haki. Haki ya wenye haki huondoshwa kwa kutoa rushwa. Rushwa hupofusha macho, huziba masikio na hufifisha ufahamu na uwezo wa kufikiri. Mtu aliyekula rushwa hukosa wasaa wa kutafakari nani atamfaaa naye huangalia nani kampa nini ili amchague. Tutapata viongozi wabovu kwa kuendekeza rushwa. Tutakosa haki zetu kwa kuendekeza rushwa,”alisema Askofu Mameo.

Aliongeza kusema kuwa rushwa huzaa manung’uniko na hali ya kutowajibika. Huzaa viongozi wasio wajibika kwa wananchi na hivyo kero za wananchi hubaki pale pale.

“Ufukara hautakwisha kwa kuwa viongozi hawatakuwa wakiwajibika kwa wananchi kuondoa changamoto zinazowakabili. Mwishowe ni rahisi kwa wananchi masikini kukata tamaa. Mwananchi akikataa tamaa ni rahisi kufanya vurugu kwani hana cha kupoteza.

Aliwaasa wanasiasa kuepuka rushwa katika nyakati hizi za uchaguzi na wananchi wasikubali kupokea rushwa kwani ikiwa watapokea rushwa hawatakuwa na uwezo wa kumuwajibisha kiongozi aliyewapa rushwa.

Ukweli ulivyo unaungana na sauti ya kinabii ya Askofu Mameo na kutoa pongezi kubwa kwake kwa kuyaona hayo yote katika uwanja huu wa siasa hususani katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.

Ni muhimu kwa wanasiasa, viongozi na wananchi kwa ujumla kusikia sauti hii ya maono na makanyo ili kuepuka matokeo yatakayotokana na kupuuzia sauti hiyo ya kinabii ya Askofu Mameo.

Rushwa imelalamikiwa mahali pengi nchini katika nyakati hizi za uchaguzi. Wito kwa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAkukuru) na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuwa macho katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.

Ni wazi kuwa wapo wanasiasa waliodhamiria vurugu. Hawa wanapaswa kukemewa na kuchukuliwa hatua kali za haraka za kisheria ili wasiichafue amani ya nchin yetu.

Watanzania wana imani kubwa kwa Rais wao Dk. John Magufuli kuwa ni kiongozi shupavu na imara ambaye atapambana kuilinda nchi hii ili isitumbukie mikononi mwa majahiri ambao wanataka kuutumia uchaguzi huu kusababisha machafuko hapa nchini.

Huu ni wakati wa uchaguzi, uchaguzi usiwe kikwazo cha kuivuruga amani yetu. Vyama vitapita lakini Tanzania itabaki kama asemavyo Askofu Jacob Mameo. Tuilinde amani yetu.

The post Sauti ya Askofu Mameo kuhusu amani ya kinabii appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *