img

Pambalu: Mama alininyima chakula kisa nimejiunga na Chadema,on September 3, 2020 at 7:02 am

September 3, 2020

Na CLARA MATIMO “MWAKA 2011 ni mwaka ambao sitausahu kabisa maishani mwangu, mama yangu mzazi alininyima chakula alipogundua nimejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati huo yeye alikuwa  ni Katibu wa UWT, mwanachama kindakindaki wa Chama Cha Mapinduzi”. Ndivyo anavyoanza kueleza changamoto alizokutana nazo katika siasa kwenye ngazi ya familia yake,  mgombea ubunge Jimbo
The post Pambalu: Mama alininyima chakula kisa nimejiunga na Chadema appeared first on Gazeti la Rai.,

Na CLARA MATIMO

“MWAKA 2011 ni mwaka ambao sitausahu kabisa maishani mwangu, mama yangu mzazi alininyima chakula alipogundua nimejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati huo yeye alikuwa  ni Katibu wa UWT, mwanachama kindakindaki wa Chama Cha Mapinduzi”.

Ndivyo anavyoanza kueleza changamoto alizokutana nazo katika siasa kwenye ngazi ya familia yake,  mgombea ubunge Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza kwa tiketi ya Chadema, Mwalimu John Pambalu , mwenye Shahada ya Ualimu katika masomo ya Historia na Jiografia.

Anasema wakati huo alikuwa na umri wa miaka 21 akiwa mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Ihungo iliyopo Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera ambapo alikuwa amerudi kwa likizo fupi.

Pambalu anabainisha kwamba wazazi wake wote wawili baba yake mzee Justine Pambalu na mkewe Hyasinta Wanchelele walikuwa ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao walikuwa wakikipenda sana chama chao.

“Mama yangu mzazi Hyasinta wakati huo alikuwa ni Katibu wa UWT Kata ya Butimba, baba alikuwa hana cheo chochote ndani ya CCM alikuwa akigombea mara nyingi nafasi ya ujumbe wa Serikali ya Mtaa anashindwa huku akilalamika kwamba anahujumiwa ingawa sijui alikuwa anahujumiwa vipi,”anaeleza.

Anasema ingawa wazazi wake walikuwa ni wanachama wa CCM yeye alivutiwa na  Chadema hasa kupitia Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe kila alipokuwa akihutubia mikutano mbalimbali pia alikuwa akivutiwa na wabunge wa upinzani walivyokuwa wakiibua hoja zenye tija kwa wananchi na taifa bungeni.

Anaeleza Aprili 16 mwaka 2010 alijiunga rasmi na Chadema, kwa kuwa wazazi wake walikuwa ni wanachama wa CCM hakutaka waone kadi yake hivyo akaificha lakini kwa  bahati mbaya ikabumbuluka.

“Wakati nasoma kidato cha nne Shule ya Sekondari Butimba, nilikuwa Mwenyekiti wa litrujia wa Tanzania Young Catholic Studeny (TYCS) hivyo nilikuwa na kadi ya TYCS nilipoondoka kwenda shule kidato cha tano Ihungo sekondari nilichukua kadi yangu ya Chadema nikaweka ndani ya kadi ya TYCS nikaitunza chumbani kwa mama.

“Nilipokuja likizo fupi nyumbani mwaka 2011 nikiwa naamini mama hajaona kadi yangu ya Chadema, usiku alipomaliza kupika akaweka chakula mezani, kabla hatujaanza kula akaniuliza wewe ni chama gani?

“Nikajua hapa siri yangu imefichuka nikamjibu Chadema, akaniambia sasa leo hautakula nenda huko Chadema ukale, ikabidi nikae pembeni lakini walipokula kidogo baba akasema siasa zenu pelekeni huko muache mwanangu ale.

“Nilisogea nikala lakini kwa kweli mwanzoni mama hakuwa upande wangu kabisa kwa sababu alikuwa anaipenda sana CCM, baba yangu aliniuliza kwa nini unapenda kujiunga upinzani nilipomweleza kwamba  nimegundua wana hoja nzuri zenye tija kwa wananchi alinielewa na alikuwa wa kwanza kuniunga mkono,”anaeleza Pambalu.

Anafafanua kwamba mama yake alimuunga mkono rasmi Agosti mwaka 2015 siku aliyokuwa akizindua kampeni za kugombea udiwani Kata ya Butimba kupitia Chadema.

“Ile huruma ya mama ilizidi mapenzi ya chama ikabidi mama yangu ajiunge na mimi kwenye chama changu ili kunisapoti alisema mimi ni mwana wa CCM, lakini damu ni nzito kuliko maji inabidi nimuunge mkono mwanangu ninawajibu wa kuhakikisha anafikia ndoto zake.

“Walimwita mama kwenye vikao vya  CCM wakamwambia tunaona una mtihani kwenye familia yako tunahitaji utuombee kura lakini una mgombea wa upinzani kwenye familia yako ambaye ni mwanao unasemaje akawajibu kwa kweli kwa sasa lazima nichague kimoja kati ya chama na mwanangu na imebidi niwe upande wa mtoto wangu akawapa vifaa vyao vyote akajiunga rasmi Chadema akanisaidia kampeni nikashinda udiwani,”anaeleza.

Kwa mujibu wa Pambalu akiwa Diwani wa Kata ya Butimba ndiye aliyekuwa diwani mdogo kuliko madiwani wote wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambapo alikuwa na umri wa miaka 25 mwaka 2015.

Anasema mwanasiasa anayemvutia zaidi kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, John Mnyika kwa sababu ni kiongozi mwenye maadili, pia ni mcha Mungu amebaini hilo kwa kuwa kila mara asubuhi huwa anampigia simu na kumwambia asisahau kujiombea, kuliombea taifa, viongozi na Watanzania wote.

KWANINI AMEAMUA KUGOMBEA UBUNGE

Pambalu anasema sababu iliyomfanya agombee nafasi hiyo ni kupata fursa ya kuwasemea watu ambao wanaonewa huku akibainisha ingawa amewahudumia wananchi kwa kipindi cha miaka mitano katika ngazi ya udiwani amegundua uwakilishi wake una mipaka hivyo ameona agombee ubunge ili apate uwanja mpana wa kuwasemea.

“Wananchi wamekuwa wakinituma kuwasemea changamoto mbalimbali ili zipatiwe ufumbuzi na Serikali lakini uwakilishi wangu haukuzaa matunda kwa sababu kelele zote nilizokuwa napiga ili kuwasaidia zilikuwa zinaishia ndani ya jengo la Halmashauri ya Jiji la Mwanza, maana ni masuala ya kisera na vipaumbele vya Serikali vya kibajeti vya kila mwaka.

“Nikagundua uwakilishi wangu una mipaka nikaona nigombee ubunge ili nikapambane kuiondoa hiyo mipaka maana nimetambua wanapotunga bajeti za nchi wanapokosekana watu wanaoweza kusimama kwa niaba ya wananchi sio kwa niaba ya Serikali wanaoumia ni wananchi, kwa hiyo ili niweze kusaidia kwenye hayo maeneo ni lazima niende kule ambako kunatoa mwelekeo wa Serikali na halmashauri ambazo ziko chini ya Serikali,”anasema.

Anasema sababu nyingine iliyomfanya agombee ubunge ni kuwasaidia vijana,  maana wengi wanahitimu vyuo vikuu bila kujua nini watafanya baada ya kuhitimu ikiwa hawataajiriwa kwa sababu sera za kifedha zinawabagua.

“Nilitembelea benki ya Maendeleo ya Wakulima, wanakopesha kuanzia Sh milioni 20 lakini wanataka uwe na dhamana ya shamba lenye thamani ya Sh milioni 20 ambalo ni la kwako sasa kijana kupata mtaji kwa dizaini hiyo haiwezekani.

“Ninaingia bungeni ili kikundi cha vijana chenyewe kitafsiriwe kuwa ndiyo dhamana ya vijana ambao hawajaanza kuwa na dhamana yoyote wakopeshwe, natamani kuona halmashauri ya Jiji la Mwanza inaongozwa na upinzani ili tukatoe mikopo ya vijana na akina mama pasipo kuwa na upendeleo wowote kama ilivyo kauli mbiu yangu ‘Nyamagana mpya, fikra mpya’ .

MFANIKIO KATIKA UDIWANI

Anasema anajivunia zaidi  kuona wakazi wa Kata ya Butimba wote ambao walikuwa hawajapimiwa maeneo yao wamepimiwa  kupitia upimaji shirikishi, sasa wanaweza kukopa katika taasisi mbalimbali za fedha kwa manufaa ya kuinua uchumi wao.

Vilevile amefanikiwa kupunguza utoro shule ya Msingi Mazoezi B ambapo alikutanisha kamati ya shule, walimu na wazazi  wakatengeneza mkakati wa pamoja utoro ukaisha,  shule ya msingi amani ilikuwa ya pili kutoka  mwisho kiwilaya lakini hadi mwaka jana imeshika nafasi ya 60.

“Shule ya Msingi Tambuka Reli ilikuwa miwoshoni lakini mwaka jana ilipata pongezi kutoka halmashauri kati ya shule ambazo zilikuwa kwenye hatari mbaya sasa zimepiga hatua.

“Shule ya Sekondari iliyokuwa inafanya vibaya ilikuwa ni Butimba Day ambayo nayo tumepongezwa kutokana na matokeo  ya mwaka jana kwa kweli nilivyozikuta na nilivyoziacha zinatia moyo pia tumefanya uwekezaji wa miundombinu  ya madarasa, jengo la utawala na matundu ya vyoo zaidi ya Sh milioni 170 shule ya Sekondari Nyegezi na maabara Sh milioni 26 shule ya Sekondari Nyamagana.

Anaeleza mafanikio mengine kuwa ni ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Msingi Amani Sh milioni 18, nyumba ya mwalimu  na ukarabati wa majengo Shule ya Msingi Tambukareli pamoja na kukarabati majengo zaidi ya Sh milioni 25.

“Ninajivunia sana pia sekta ya michezo mwaka 2016 nilidhamini mashindano ya mpira wa miguu yaliyojumuisha vijana wa Kata ya Butimba na kata jirani  lengo likiwa ni kuibua vipaji vya vijana ambapo timu ya Kata ya Butimba Fathom Sports Club  iliibuka kidedea kwenye mashindano ya ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa,”anaeleza

Kwa upande wa afya anasema wanamalizia ujenzi wa jengo la mama na mtoto Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana kwa ufadhili wa Shirika la Agakhan, ujenzi wa jengo la elimu ya uzazi kwa vijana kwa ufadhili wa Taasisi ya kiwohede.

Huduma ya maji imewafikia wakazi wa Mtaa wa Londo Kata ya Butimba, mabomba Mtaa wa Tambukareli ingawa changamoto ni upatikanaji wa maji.

Miundombinu ya barabara wameweka mitalo  na wamerekebisha katika Mtaa wa Kambarage, kona ya shule Mtaa wa Tambukareli, Shule ya Msingi Kanyerere na darajani ingawa anakili bado changamoto ya barabara ni kero kubwa kwa sababu mvua ikinyesha huharibika.

CHANGAMOTO ALIZOKUTANA NAZO

Kwa mujibu wa Pambalu changamoto alizokutana nazo ni mapokeo ya baadhi ya watu katika jamii alipochaguliwa kuwa diwani ambapo walidai kwamba atawezaje kuongoza wakati anaumri mdogo.

“Nimepata udiwani nikiwa nina umri wa miaka 25 nilikuwa naishi nyumbani kwa wazazi, sijaowa baadhi ya wanajamii wakawa wananichukulia kama msera lakini nilivyoanza kutimiza majukumu yangu kwa ufasaha ndipo waliponielewa.

“Pia tangu niwe diwani chama chetu kimepita katika misukosuko mikubwa sana mara nyingi polisi wamenizuia kila nilipokuwa natimiza majukumu yangu ya chama.

“Mwaka huu nikiwa wilayani Sengerema mkoani Mwanza na Jimbo la Kilombero  mkoani Morogoro kwenye Oparesheni Tume Huru walinizuia ukizingatia mimi ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema Taifa (Bavicha).

Pambalu anasema kitu anachokipenda katika maisha yake ni siasa zenye demokrasia ya kweli na anachukia sana dhuluma ya namna yoyote ile.

NYADHIFA KATIKA CHAMA

Mwaka 2012 hadi 2014 alikuwa Katibu wa Chadema Tawi la Amani Butimba, mwaka 2014/ 2015 Mwenezi wa chama Kata ya Butimba, mwaka 2015/2020 diwani  kata hiyo, mwaka 2014/2017 Mwenyekiti Bavicha Wilaya ya Nyamagana, 2017 Desemba alichaguliwa kuwa makamu Bavicha Tanzania Bara, 2019 hadi sasa ni Mwenyekiti Bavicha Taifa.

ELIMU NA MAISHA

Mgombea huyo mwenye umri wa miaka 30 alizaliwa Oktoba 17 mwaka 1990 katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, amesoma Shule ya Msingi Mazoezi iliyopo Kata ya Butimba wilayani humo kuanzia mwaka 1999 hadi 2005, baada ya kuhitimu elimu yamsingi mwaka 2006 hadi 2009 alijiunga Shule ya Sekondari ya kutwa  Butimba  ambapo alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne  na mwaka 2010 hadi 2012 alikuwa akisoma kidato cha tano na  sita katika shule ya sekondari  ya wavulana Ihungo iliyopo Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera, alipohitimu  mwaka 2012 alijiunga chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino cha jijini Mwanza (Saut) akahitimu Shahada ya Ualimu katika masomo ya Historia na Jiografia mwaka 2015.

Ni mtoto wa tatu kati ya sita kwenye familia yao, amefunga ndoa na Getruda Malugu katika Kanisa Katoliki Parokia ya Butimba  Agosti 12  mwaka 2017, hajabahatika kupata mtoto ingawa anatamani kuwa baba wa watoto watatu.

The post Pambalu: Mama alininyima chakula kisa nimejiunga na Chadema appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *