img

Kampeni ni mizani ya kupima wagombea,on September 3, 2020 at 7:29 am

September 3, 2020

NA MWANDISHI WETU “KAZI ya vyama vyetu vya siasa ni ngumu zaidi sasa kuliko ilivyokuwa pale tulipokuwa tunapigania uhuru. Pale tuliita mikutano ya umma; tulipiga kelele kutaka Uhuru; tuliwatukana wakoloni ambao, lazima niongoze, walistahili sana kutukanwa! Lakini sasa tunajenga nchi. “Tunapokuwa na mikutano ya umma hatuwezi kuitukana serikali kwa sababu sisi ni serikali na watu ndio serikali.
The post Kampeni ni mizani ya kupima wagombea appeared first on Gazeti la Rai.,

NA MWANDISHI WETU

“KAZI ya vyama vyetu vya siasa ni ngumu zaidi sasa kuliko ilivyokuwa pale tulipokuwa tunapigania uhuru. Pale tuliita mikutano ya umma; tulipiga kelele kutaka Uhuru; tuliwatukana wakoloni ambao, lazima niongoze, walistahili sana kutukanwa! Lakini sasa tunajenga nchi.

“Tunapokuwa na mikutano ya umma hatuwezi kuitukana serikali kwa sababu sisi ni serikali na watu ndio serikali. Kazi yetu sasa ni kuelimisha, kueleza na kujenga. Ni wajibu wetu kuwaongoza watu katika kazi ya kutoa mashauri ya kusaidia maendeleo.”

Hiyo ni kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere miaka 54 iliyopita, lakini ikibaki kuwa na uhai endelevu, licha ya kwamba siasa za hivi sasa Tanzania zinatofautiana na ambazo zilikuwa zinafanywa takribani miaka 25 iliyopita, kutokana na mabadiliko yaliyochagizwa na kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi.

Hata hivyo kauli hiyo haikulenga kwenye chama kimoja cha siasa licha ya kwamba ilitolewa enzi za chama kimoja cha siasa.

Kuwepo kwa vyama vingi kuliwezesha kuibuka kwa wanasiasa ambao awali walikuwa wamefunikwa na kivuli cha ‘chama kimoja, itikadi moja’.

Hali hiyo imewezesha waliojitokeza na kuchaguliwa kuviongoza vyama hivyo kwamba wapo upande upi katika kuutumikia umma au wapo kwa ajili ya kikundi au tabaka la watu.

Wakati Tanzania ikiwa inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani ambao utatanguliwa na kampeni za kujinadi kwa wapiga kura.

Hapo ndipo kauli hiyo ya Baba wa Taifa inapenyeza kwani itakuwa ndio kigezo sahihi cha kuangalia na kusikiliza utashi wa wanaoomba iwapo unakidhi yaliyoelezwa katika kauli hiyo.

Jambo la msingi ambalo limekuwa likielezwa katika kuhusisha vyama vingi, imekuwa ni kuweka mbele masilahi ya taifa kwanza na kuachana na masuala ya kichama na kiitikadi kutokana na kigezo muhimu kwamba maendeleo hayana chama.

Jambo hilo ni jema na sawia ili kupata mafanikio, dira inatakiwa kulenga masilahi kwa wote. Kwa upande mwingine ni kwamba  pale linapojitokeza suala la itikadi ni sawa na kuligawa taifa katika matabaka ya watu.

Pindi likianza suala la itikadi ni dhahiri kuwa haitakuwa rahisi kuepuka masuala mengine ambayo yatakuwa ni ya kibaguzi dhidi ya kundi moja na jingine.

Hata hivyo jambo linaloweza kujitokeza ni kwamba wanaoegemea kwenye itikadi za kichama watakuwa hawasemei watu bali watakuwa wanapigia mbiu masilahi ya chama husika na papo hapo matarajio yakiwa ni masilahi ya kiitikadi pia.

Pindi kampeni zikielekeza katika udhanifu wa namna hiyo, ni dhahiri kuwa kundi la aina hiyo linakoma kuwa ni mwakilishi wa watu na kwamba halitaweza kuzingatia maono ya watu na hata uwepo wa vyama kwa mtazamo huo hautakuwa ni wa kuwasemea watu bali kulisema kundi la watu na hivyo kujenga matabaka la watu.

Katika mazingira ya aina hiyo hoja ya msingi ni kwamba mizani itaegemea upande gani wakati wa kujinadi kwa wapiga kura?

Je, vyama vipo kwa ajili ya watu au kwa masilahi ya kundi la watu kwa maana kwamba vyama vipo kwa ajili ya kundi kubwa la watu ambao ni walala hoi au vipo kwa ajili ya kikundi cha watu ambao tayari wameshaonja pepo?

Kauli hiyo ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa katika mkutano wa chama cha Uganda People’s Congress Juni 7, 1968 mjini Kampala, ‘Lazima Chama Kiwasemee Watu”  Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alisema  “Kazi ya chama cha siasa kilicho imara ni kuwa kama daraja la kuwaunganisha watu na serikali waliyoichagua, na kuiunganisha serikali na watu inayotaka kuwahudumia.”

Ni dhahiri katika kampeni ambazo zitakuwa za ushindani kutoka kwa vyama vya siasa 17, mizani itakuwa inapima iwapo kinachonadiwa kinawaunganisha watu au kinawaparaganyisha.

Kwa kutumia mizani hiyo wapiga kura wanaweza kuhoji iwapo maoni yao yamekuwa yanatekelezwa au yanaachwa yateterekee ‘kusikojulikana’ kwa maana kwamba kama waliwasilisha kero na hakuna ufumbuzi uliofanywa basi hata wanaoomba kura watakuwa wanalenga kuwaparaganya watu.

Mwalimu Nyerere aliendelea kusema, “Ni wajibu wa chama kuwasaidia watu kuelewa serikali yao inafanya nini na kwanini; ni wajibu wake kusaidia watu kushirikiana na serikali yao kwa juhudi ya pamoja ili kuuondosha umaskini ambao umetuelemea.

“Na ni wajibu wa chama pia kuhakikisha kwamba serikali inaendelea kuyajua sana maoni yao, shida na matakwa ya watu. Ni wajibu wake kusemea watu. Pia ni wajibu wake kuwaelimisha watu na kuwasaidia kuona shughuli za Serikali zina maana gani kuhusu usalama wao wenyewe wa siku zijazo na fursa zao wenyewe za siku zijazo.”

Kimsingi kinachotafutwa pindi watu wanapotoa maoni au malalamiko yao ni kutaka kuijenga leo, kesho na siku zijazo na kujiona kuwa wako kwenye usalama na wanaweza kuzitumia fursa zinazokuwepo kwa masilahi ya taifa lao.

Kwa maana hiyo ni kwamba kama vyama vikiegemea kwenye itikadi vinajiondoa kwenye kuwasemea watu na hivyo kujiondoa kwenye mioyo ya watu na kuwa chama kilicho na fikra za kubagua na hata kujaa unafiki nd miongoni mwa viongozi wake.

Kwa maana hiyo Mwalimu Nyerere alibainisha, “Chama chenye mizizi yake katika mioyo ya watu tu, chenye wafanyakazi wenye ari vijijini na kwenye miji nchini kote – chama cha namna hiyo tu ndicho kinachoweza kuiambia serikali ni nini matilaba ya watu, na kama matilaba hayo yanatekelezwa kwa njia ya kuridhisha.

 “Kuweko chama kama hicho ndiko kunakoweza kuhakikisha kwamba Serikali na watu wanashirikiana kutekeleza matilaba ya watu.”

Kwa maana hiyo ni dhahiri kuwa ufanisi wa vyama unatokana na uongozi safi jambo ambalo limekuwa likihubiriwa kila mara kama moja ya nguzo muhimu ya maendeleo. Kimsingi viongozi hao wanatakiwa kuwajali wanajamii wote bila kuwagawa kimatabaka.

 “Marais, mawaziri, wabunge na kadhalika, majina yao yanaweza yakaandikwa magazetini, wanaweza kuonekana kwenye kionambali (televisheni). Lakini wakiwa ni viongozi safi, watakuwa ni safi hasa kwa sababu wanaungwa mkono na chama chenye nguvu, ambacho kinajua na kuelewa mahitaji ya watu na maoni ya watu.

 “Ikiwa viongozi kama hao hawavitumii vyeo vyao ipasavyo, au hawana fungamano na watu, basi aghalabu itakuwa ni kwa sababu chama kinashindwa kuwasemea watu na kuwa jicho la watu,”alisema.

Hata hivyo alionya, “Mfanyakazi wa chama ndiye mtu muhimu…yaani kama anafanya kazi pamoja na watu, na kama  watu wanamkinai na kuwa na imani naye kama mmoja wao, ambaye wanamwendea wakati wa shida, au wanapokuwa na mawazo, au wanapokuwa hawaelewi kitu fulani.

 “Kama mna shaka na ukweli wa maneno haya, tazameni kote Afrika – kusema kweli, tazameni dunia nzima – mwone nini kimetendeka katika zile nchi  ambako vyama vya siasa vimeshindwa kuwa, au vimekoma  kuwa, vitendaji na viwakilishi vya watu….”

Hoja inayoibuka ni kwamba katika masuala nyeti kama la kuhakikisha kuwa rasilimali zilizopo, au mikakati iliyo na dira ya kuharakisha maendeleo inapokuwa ni kwa masilahi ya jumla ya wananchi na kuungwa mkono na vyama basi unakuwa ni mrengo chanya.

Hali ya aina hiyo katika mizani ya kampeni inaweza kuwa ni njia ya kujipatia kura kwa moyo safi wa wapiga kura.

Kama ikiwa ni kinyume na kuwa katika mrengo wa kiitikadi basi vyama vitakuwa vinajinasibu kuwa vimekoma au kushindwa kuwa viwakilishi vya watu.

Kama hali ikiwa ni hivyo basi vitakuwa ni viwakilishi vya walioonja pepo na vikiwa vinaendelea kuwanyonga wavuja jasho na kitakachofuata ni kukwamisha mikakati ya maendeleo.

The post Kampeni ni mizani ya kupima wagombea appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *