img

Hivi ndivyo vipaumbele vitakavyovibeba vyama Oktoba 28,on September 3, 2020 at 8:01 am

September 3, 2020

NA FREDERICK FUSSI NENO ilani si geni hapa nchini hasa kwenye shughuli za uchaguzi. Neno hili maana yake ni tangazo ambalo lipo bayana kuelezea kinagaubaga juu ya matamanio ya chama cha siasa kuhusu maendeleo ya watu. Ilani huelezea chama cha siasa endapo kikichaguliwa pamoja na wagombea wake watafanya nini kuhusu kuwaletea wananchi maendeleo na kuhakikisha
The post Hivi ndivyo vipaumbele vitakavyovibeba vyama Oktoba 28 appeared first on Gazeti la Rai.,

NA FREDERICK FUSSI

NENO ilani si geni hapa nchini hasa kwenye shughuli za uchaguzi. Neno hili maana yake ni tangazo ambalo lipo bayana kuelezea kinagaubaga juu ya matamanio ya chama cha siasa kuhusu maendeleo ya watu.

Ilani huelezea chama cha siasa endapo kikichaguliwa pamoja na wagombea wake watafanya nini kuhusu kuwaletea wananchi maendeleo na kuhakikisha ustawi wao.

Endapo chama cha siasa kikishinda uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kitalazimika kubadili ilani ambalo ni tangazo kuwa mpango wa miaka mitano wa maendeleo kwa sababu ndio muda wa kikatiba wa Serikali kuwepo madarakani.

Mpango huo wa maendeleo hugawanywa katika mipango ya kila mwaka ambayo huwasilishwa bungeni na Serikali, ili kutungiwa sheria ya matumizi na sheria ya fedha kwa mwaka wa fedha husika.

Kwa hiyo Ilani za uchaguzi ni muhimu katika michakato ya ushiriki wa wananchi katika kuchagua viongozi na vyama vyao vya siasa. Hapa nchini hatuna utaratibu wa wagombea binafsi, kama tungekuwa nao pia wao wangelazimika kusema ilani zao ni zipi katika uchaguzi mkuu.

Katika pitapita zangu nimefanikiwa kupata nakala tatu za ilani za uchaguzi za vyama vya siasa vya CCM, chadema na ACT-Wazalendo. Hivyo basi nimeona ni muhimu nikasaidia kufanya uchambuzi wa ilani hizo ili kujua kinagaubaga cha matangazo ya matamanio ya vyama hivyo.

Ilani hizo zitanadiwa na vyama husika ndani ya siku 63 za kampeni kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Oktoba 28 mwaka huu. Bila shaka uchambuzi wangu utasaidia wasomaji wa safu hii kuyaelewa vizuri matamanio ya vyama na wagombea wao katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Hapa nchini tunachagua wagombea wanaotokana na vyama vya siasa. Hivyo ukichagua mgombea wa chama cha siasa pia unakuwa umechagua na ilani ya uchaguzi ya chama chao.

Kuhusu ukubwa wa ilani za vyama vya siasa. Ilani ya CCM ina jumla ya kurasa 308, Chadema ilani yao ina kurasa 104 wakati ACT-Wazalendo ina kurasa 62. Hii maana yake ni kuwa wasomaji wa hizi ilani watatumia muda mfupi zaidi kusoma na kuelewa ilani ya ACT-Wazalendo, ikifuatiwa na Chadema na muda mrefu zaidi utatumiwa kusoma na kuielewa ilani ya CCM kwa sababu inaongoza kwa kuwa na kurasa nyingi zaidi.

Ilani ya CCM ina kusara nyingi kwa sababu imeripoti kazi ambazo zimefanywa na Serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015-2020) wakati ilani za Chadema na ACT-Wazalendo hazina ripoti kama hizo za utendaji wa kazi zao kwa sababu hawakushinda wala kuunda Serikali.

Katika aya ya 6 ya sehemu ya kwanza ya Ilani ya CCM imezungumzia mafanikio ya Serikali ya CCM kati ya mwaka 2015 na 2020, wakati huo huo ilani ya ACT-Wazalendo katika sehemu ya kwanza mara baada ya utangulizi wao, wamefanya uchambuzi ya hali ya nchi katika kipindi hicho hicho cha miaka mitano iliyopita.

Wakati Chadema wao mara baada ya maneno ya utangulizi wametoa orodha ya vipaumbele vyao na mambo watakayofanya ndani ya siku 100 za kwanza baada ya serikali yao kuchaguliwa kuunda dola.

Katika aya za utangulizi wa kila ilani ya kila chama ambazo zinachambuliwa hapa vyama vinazungumzia misingi ambayo ilani zao imesimamia. Kila chama cha siasa kinakuwa na imani yake kuhusu misingi ya ujenzi wa maendeleo.

Vyama vyote vimezungumzia msingi wa uhuru kwa mitizamo yao. Kwa mtazamo wa CCM wao imani yao kuhusu uhuru wamesema kuwa na nitanukuu “CCM itahakikisha kuwa Tanzania inaendelea kulinda Uhuru wake, kudumisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kuimarisha Muungano wetu wenye mfumo wa serikali mbili pamoja na tunu nyingine za Taifa ikiwemo falsafa ya Mwenge wa Uhuru ili kuendelea kujenga Taifa imara linalojitegemea kiuchumi na kisiasa, lenye ustawi wa watu wake na linaloenzi na kuthamini mila nzuri, desturi na utamaduni wetu”, mwisho wa nukuu.

Wakati CCM ikiamini kuhusu mtazamo huo, Chadema wao mtazamo wao kuhusu uhuru wanasema kuwa; na nitanukuu wao wataongoza nchi kwa “kudumisha na kuendeleza uhuru wa mawazo, uhuru wa kutoa na kupata habari na kujumuika na wengine kama nyenzo ya kutoa nafasi kwa ubunifu kushamiri ambao ni nyenzo ya kuboresha elimu na na hatimaye ukuaji wa uchumi kwa ujumla”.

ACT-Wazalendo wao kwenye utangulizi wao pia wametoa mtazamo wao kuhusu uhuru kama msingi wa ilani yao, nitanukuu, wao walisema kuwa wanaamini “uchaguzi huu ni uchaguzi wa kuchagua, “Uhuru wa kweli kwa kila mtu dhidi ya utumwa”

Kuhusu vipaumbele vya kila chama, CCM kwa upande wao wamewasilisha vipaumbele sita vya miaka mitano, wakati Chadema wao wameorodhesha vipaumbele 20.

ACT-Wazalendo wao wametaja vipaumbele 12. Vyama vyote vimeorodhesha vipaumbele vyao kwa namna ambayo sio rahisi kwa wapiga kura kuzikumbuka kwa haraka. Kazi kubwa waliyonayo vyama vya siasa ni kuwasiliana na wapiga kura katika kuzichambua ilani zao na kuwasilisha matamanio yao kwa lugha rahisi inayoeleweka kwa wepesi zaidi, kwenye eneo hilo Chauma ambayo imemsimamisha Hashim Rungwe kwenye uchaguzi wa Rais wamefanikiwa sana kuwasiliana na wapiga kura wao.

Chauma wao ilani yao inasisitiza lishe bora kwa wananchi, huku mgombea wao wa urais akinadi sera zao kwa kusisitiza kula wali na nyama. Kwa upande wa CCM vipaumbele vyao sita ni pamoja na; kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa letu, kukuza uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi, kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi; kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini na kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi.

kabisa kipaumbele chao ni kutengeneza ajira zisizopungua 8,000,000 (milioni nane) katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana.

CCM wao kwenye kila kipaumbele wameelezea shabaha zao ni zipi. Kwa mfano kwenye eneo la kwanza la utu, usawa, uongozi, umoja, amani na mshikamano wameorodhesha shabaha takribani sita.

Shabaha hizo ni pamoja na kudumisha na kuimarisha umoja, udugu, mshikamano, amani, utulivu, ulinzi na usalama; kuimarisha Muungano wa Serikali mbili, kuenzi Uhuru wa nchi yetu na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na kutumia tunu nyingine za kitaifa ikiwemo falsafa ya Mwenge wa Uhuru katika kujenga moyo wa uzalendo na uwajibikaji; kuimarisha demokrasia, utawala bora na haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, pamoja na udhalilishaji wa aina zote; Kuimarisha Serikali za Mitaa ili ziweze kutimiza wajibu wao kwa wananchi katika maeneo husika; kuchukua hatua madhubuti za kujenga mazingira wezeshi kwa asasi za kiraia, kidini na vyombo vya habari kustawi ili kuchangia katika maendeleo ya Taifa na kuimarisha huduma na kulinda haki kwa makundi maalum wakiwemo wanawake, vijana, wazee, watoto na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wa Chadema vipaumbele vyao 20 ni pamoja na kugatua madaraka ya uongozi na utawala kwa lengo la kuusogeza karibu na wananchi; kubadili mfumo wa uongozi na utawala ili kuongeza na kuzingatia misingi ya uadilifu, ufanisi, uzalendo na uwajibikaji; kwa kushirikiana na sekta binafsi kujenga uchumi imara wa kidigitali na shirikishi; kuongeza mishahara na kuwapandisha madaraja watumishi wa umma; kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje; kurejesha mchakato wa Katiba Mpya kuanzia ilipoishia Rasimu ya Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji Warioba; kurejesha uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza na kutoa maoni; kutoa elimu bora na bure kwa ngazi zote; kuanzisha utaratibu wa afya bure kwa akinamama wajawazito, watu wenye ulemavu, watoto na wazee; kuwajengea uwezo wanawake kusimamia na kumiliki uchumi; kwa kushirikiana na sekta binafsi kuongeza wigo wa ajira na kipato chenye tija kwa vijana; kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi, salama na ya uhakika kwa wote; kuwezesha Wananchi kumiliki ardhi kwa matumizi endelevu; kushirikiana na sekta binafsi kuboresha miundombinu ya barabara, masoko, nishati na viwanda vya kusindika mazao vijijini; kutumia rasilimali ya maji iliyopo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na mifugo; kushirikiana na sekta binafsi kuboresha miundombinu ya barabara, reli, usafiri wa anga na majini; kushirikiana na sekta binafsi kuboresha sekta ya utalii na maliasili; Kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha uwepo wa nishati nafuu na ya uhakika; kuboresha sekta ya madini na kuwezesha wachimbaji wadogo wanashiriki na kumiliki uchumi wa madini; kushirikisha sekta binafsi katika kuimarisha sekta ya sanaa, utamaduni na michezo na kuifanya iwe ya kibiashara.

Katika kufanikisha ilani yao Chadema wanadai kuwa ilani yao haijajikita kwenye ahadi hewa, huku wakijinasibu kuwa wao wanaamini katika “Uhuru, Haki na Maendeleo ya Watu”. Wakati CCM wakionesha shabaha ya kila kipaumbele, Chadema wao wameonesha dhahiri watafanya mambo makubwa 16 katika siku 100 za kwanza baada ya chama chao kuchaguliwa na wananchi kuunda Serikali.

Mambo hayo kwa ufupi ni pamoja na kupeleka muswada bungeni ili kutunga sheria ya maridhiano ya kuondoa hofu ya kutolipiza visasi, kuunganisha nguvu za wananchi wote bila ubaguzi wa vyama katika kuongoza Taifa.

Jambo la pili ndani ya siku zao 100 ni pamoja na kupeleka muswada bungeni wa kutunga sheria ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kuhusu kutoa elimu bure kwanzia shule za awali mpaka sekondari.

Jambo lingine ni kupunguza kiwango cha marejesho ya mikopo ya elimu ya juu hadi kufikia asilimia 3 ya mshahara kwa mnufaika na kutanua wigo wa muda wa marejesho hadi kufikia miaka 25 tangu mnufaika apate ajira, pia wanadhamiria kufuta riba na tozo zote zitokanazo na adhabu ya kuchelewesha marejesho ya mkopo wa elimu ya juu.

Ndani ya siku hizo hizo 100 za kwanza endapo wakichaguliwa kuunda Serikali, Chadema wanasema kuwa serikali yao itashirikiana na sekta binafsi kuweka utaratibu wa kutoa huduma za afya ya msingi kwa wananchi bila malipo; pia watarejesha mchakato wa Katiba Mpya kuanzia ilipoishia Rasimu ya Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji Warioba; jambo lingine ni pamoja na kutekeleza matakwa ya Katiba kuhusu Tume ya Pamoja ya Fedha ya Muungano ili kila nchi Mshirika wa Muungano ipate mgao wake wa fedha kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Wanaendelea kudai kuwa wao na Serikali watakayoiunda watarejesha uhuru wa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kuruhusu vyombo hivyo kurusha moja kwa moja vikao vya Kamati za Bunge, Mikutano ya Bunge na Mwenendo wa Uendeshaji wa Mashauri Mahakamani.

Katika kipindi hicho hicho cha siku 100 za kwanza bado wao wanadai kuwa wataweza kupeleka miswada ya Sheria bungeni kwa madhumuni ya kuzifuta sheria zote kandamizi na zinazokiuka misingi ya haki za binadamu; wanaendelea kusema kuwa wataanzisha utaratibu wa mazungumzo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar kwa lengo la kufikia muafaka juu ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, uvuvi wa bahari kuu na usajili wa meli; pia wanadhamiria kuwa wataandaa mazingira rafiki na wezeshi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali kama vile ugonjwa, kukosa ada, mimba n.k. kurejea kwenye mfumo rasmi wa elimu na kumalizia masomo yao.

Katika hatua hizo za siku 100 za kwanza bado wanadai kuwa wanaweza kupeleka bajeti ya nyongeza bungeni katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya kuongeza mishahara ya watumishi wote wa umma, kulipa malimbikizo; sambamba na kuwapandisha madaraja watumishi wenye sifa na kulipa mishahara inayoendana na madaraja yao.

Katika hatua nyingine wanadai kuwa wataanzisha bima maalumu ya afya kwa watumishi wote wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wawapo kazini na baada ya kustaafu vikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zima moto na Uokoaji.

Pia wanasisitiza kuwa siku zao 100 za kwanza ni za kufanya vitu kama vile kurejesha maduka yasiyotozwa kodi (Duty free shops) katika vyombo vya ulinzi na usalama vikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Uokoaji; kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya sheria ya hifadhi ya jamii ili kurekebisha kikokotoo cha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wastaafu ili kiendane na mahitaji ya wastaafu; wanadai kuwa wao wanaweza kuruhusu wafanyakazi na watumishi waliochangia katika mifuko ya jamii kuchukua mafao yao wakati wowote (fao la kujitoa); wanasema kuwa bado wataweza ndani ya siku hizo kuweka utaratibu na kuwatafutia masoko wakulima, wavuvi na wafugaji ya kuuza mazao yao ndani na nje ya nchi bila kizuizi na mwisho wanasema kuwa ndani ya siku hizo wataweza kurejesha utaratibu wa awali wa ukusanyaji wa kodi,ushuru na tozo mbalimbali kwa mamlaka ya serikali za mitaa.

Kwa upande wa ACT-Wazalendo wao vipaumbele vyao 12 ni pamoja na  Ujenzi wa Demokrasia na Utoaji Haki za Watu; kwa na Ufanisi na Ubora wa Huduma za Jamii; kushughulikia Uchumi wa Watu; kufanikisha Uhuru kwa kila mtu; kutoa Elimu Bora ya kivumbuzi bila malipo; kwa na kilimo cha kimapinduzi na mazingira wezeshi ya biashara; kuwa na usawa na ustawi wa wanawake na vijana; vipaumbele vingine ni pamoja na kufanikisha Hifadhi ya Jamii kwa kila mtu/afya bora kwa wote; kuwa na ushirika wa kisasa kwa Maendeleo Jumuishi; kulinda haki za watu wenye ulemavu; kufanikisha miradi ya maji safi, salama na gharama nafuu na mwisho kabisa wao ACT-Wazalendo wanadhamiria kuzalisha ajira mpya milioni 10.

Angalau kwa kila kipaumbele ilani ya ACT-Wazalendo imechanganua shabaha zake ni zipi, kwa mfano ili kufanikisha ufanisi wa utoaji wa huduma za kijamii, kwenye sekta ya elimu wao wamewasilisha shabaha tano kwenye elimu ya msingi, shabaha tatu kwenye elimu ya sekondari, shahaba saba kwenye elimu ya ufundi, na shabaha takribani 15 kwenye elimu ya juu.

Mfano wa shabaha zao wanazotaka kufanikisha endapo chama chao kitashinda uchaguzi na kuunda Serikali kwenye elimu ya msingi pekee wanadhamiria kujenga vyumba vya madarasa 24,000 kila mwaka ili kutosheleza ongezeko kubwa la watoto mashuleni, kupanua uwezo wa vyuo vya walimu kudahili ili kuzalisha walimu 20,000 kila mwaka ili kukidhi hitaji la ongezeko la wanafunzi, kufanya mabadiliko makubwa ya mtaala, kuwa na zana za kutosha za kujifunzia na kuwepo kwa masilahi bora ya walimu na mazingira wezeshi ya kufanyia kazi.

Hivi ndivyo vipaumbele vinavyonadiwa na kila chama kati ya vyama hivi vitatu ambavyo gazeti hili limefanikiwa kupata nakala zake za ilani ya uchaguzi mkuu.

Juma lijalo tutaendelea kuchambua na kulinganisha sera za kila chama kulingana na sekta mbalimbali walizozingumzia kwenye ilani zao za uchaguzi.

The post Hivi ndivyo vipaumbele vitakavyovibeba vyama Oktoba 28 appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *