img

Biden na hofu ya Rais Trump kuiba kura,on September 3, 2020 at 6:50 am

September 3, 2020

NA HASSAN DAUDI JOTO la Uchaguzi Mkuu wa Marekani linazidi kupanda ikiwa ni takribani miezi miwili tu imebaki. Ni Novemba 3 mwaka huu siku iliyoshikilia hatima ya Rais Donald Trump; aidha aingie awamu yake ya pili au asogee kando na kumpisha mpinzani wake mkubwa, Joe Biden. Kama ni utani, basi hii unaweza kuiita ‘vita ya
The post Biden na hofu ya Rais Trump kuiba kura appeared first on Gazeti la Rai.,

NA HASSAN DAUDI

JOTO la Uchaguzi Mkuu wa Marekani linazidi kupanda ikiwa ni takribani miezi miwili tu imebaki.

Ni Novemba 3 mwaka huu siku iliyoshikilia hatima ya Rais Donald Trump; aidha aingie awamu yake ya pili au asogee kando na kumpisha mpinzani wake mkubwa, Joe Biden.

Kama ni utani, basi hii unaweza kuiita ‘vita ya vikongwe’ kutokana na sababu inayoelezwa katika aya inayofuata.

Endapo Rais Trump ataendelea, basi atakuwa rais mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kuiongoza Marekani kwani ataapishwa akiwa na miaka 74.

Pia, ikiwa Biden atashinda, basi ataingia Ikulu akiwa na umri wa miaka 78 na kuweka historia ya kuwa rais mzee zaidi wa Marekani.

Hii ni mara ya tatu kwa Biden kutaka urais, akiwa amewahi kufanya hivyo mwaka 1988 na 2008.

Mchuano ni mkali kati ya wawili hao, ambapo Rais Trump wa Republican anakabiliana na Biden, makamu wa rais wa zamani anayeipeperusha bendera ya chama kingine kikubwa cha siasa Democrat.

Awamu ya kwanza madarakani ya Rais Trump inapambwa na ukosolewaji mkubwa wa namna serikali yake ilivyoyaenda mambo.

Acha wengi kutofurahishwa na sera walizoziita za kibaguzi dhidi ya makundi mbalimbali, mathalan Waislam na raia wenye asili ya Afrika.

Rais Trump alinyooshewa vidole alipopuuzia janga la Corona, licha ya kwamba limeua raia wake zaidi ya 100,000, sahau kuhusu wengine milioni 40 waliopoteza ajira zao.

Duru za siasa zinaamini Rais Trump alizembea na kulipa uzito wa wastani tatizo hilo, hasa kwa uamuzi wake wa kupuuzia hatua ya kuvaa barakoa (mask).

Wakati kwake Corona ikiwa si ishu kubwa, Rais Trump hakujua anapoteza ushawishi kwa watu wenye umri mkubwa, ambao kimsingi ndiyo kindakindaki wa chama chake, Republican.

Ifahamike kwamba wataalamu wa afya wanalitaja kundi hilo kuwa ndilo lililo hatarini zaidi kupata maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Pia, kauli za kebehi dhidi ya umri wa mpinzani wake (miaka 77), vilichagiza kumfanya Rais Trump aendelee kupoteza mvuto mbele ya kundi hilo.

Biden, ambaye hii ni mara yake ya tatu kuifukuzia Ikulu aliutumia mwanya huo kuendelea kujizolea ushawishi.

Mwanzoni mwa mwaka huu, alikuwa mstari wa mbele kuhamasisha raia wa Marekani kuchukua tahadhari zote, ikiwamo kubaki nyumbani na kuvaa barakoa.

“Vaeni barakoa. Msijifikirie nyinyi tu, fikirieni na familia zenu. Fikirieni pia kuhusu majirani zenu. Fikirieni wenzenu. Ni suala la kulinda usalama wa watu wengine,”anasema Biden.

Ikiwa inafaa kuongeza, timu ya kampeni ya Biden imejipanga kwa kiasi kikubwa, tofauti na ile ya mpinzani wa Rais Trump katika uchaguzi uliopita, Hillary Clinton.

Jopo lake limejikita zaidi katika mitandao ya kijamii, pia likihakikisha linapunguza tofauti kubwa iliyokuwapo kati ya wazungu, watu weusi na wenye asili zingine, wakiwamo kutoka Latin.

Msisitizo wa Biden katika kampeni zake ni kufanya mabadiliko makubwa katika serikali atakayoachiwa na Rais Trump.

Sifa kubwa ya Biden ni utayari wake wa kufanya kazi na chama pinzani, wengine wakimfahamu kuwa ni mwanasiasa asiyemudu kuongea sana.

Hata hivyo, kuelekea Novemba 3 mwaka huu, changamoto ya wazi ni uwezekano wa kuwapo kwa uchaguzi huru na wa haki.

Tayari baadhi ya wachambuzi wa siasa wameibua minong’ono, wakihofia huenda kukawapo na vitendo vitakavyoathiri matokeo ya uchaguzi huo.

Wengi wao hawaoneshi imani yao kwa serikali iliyoko madarakani, wakimtaja Rais Trump kuwa ni mvurugaji wa mambo.

Licha ya kwamba bado kuna miezi miwili, Rais Trump ameanza kutilia shaka matokeo ya uchaguzi kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa imekuwa ni kawaida yake kuibua madai ya kutokuwa na imani na matokeo ya uchaguzi hata kabla ya kupiga kura.

Bado haijasahaulika alichokifanya katika Uchaguzi Mkuu uliopita (2016), aliposema hatakubaliana na matokeo endapo mwanamama Hillary Clinton angetangazwa kuwa mshindi.

Safari hii, moja kati ya aliyopinga ni kitendo cha raia kupiga kura kupitia njia ya posta.

“Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa kiboko kwa matokeo yasiyo sahihi na wenye ujanjaujanja mwingine,” aliandika katika ‘posti’ yake ya mtandao wa Twitter.

Vilevile, Rais Trump ameonesha wazi kutokubaliana na hatua ya uchaguzi kusogezwa hadi Novemba 3, licha ya kwamba hilo limetokana na janga la Corona.

“Itakuwa ni aibu kubwa kwa Marekani. Kuchelewesha uchaguzi hadi watu waweze kupiga kura kwa usalama (baada ya Corona)???” aliandika Rais Trump.

Lakini sasa, wapinzani wake wa Chama cha Democrat, sambamba na wanaharakati wa Marekani wanayatazama madai hayo kwa jicho la tatu na kubaini jambo.

Kwamba kelele zake hazina mashiko, bali zinatokana na hofu ya kupoteza nafasi ya kurudi Ikulu mbele ya Biden.

Aidha, zimelenga kumpa uhalali wa kupinga matokeo hapo baadaye, endapo Biden atatangazwa kuwa rais mpya wa Marekani.

Akihojiwa na kituo cha televisheni miezi michache iliyopita, Rais Trump aliulizwa kama atakubaliana na matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu. “Nitaangalia. Hapana, siwezi kuitikisa tu,” alijibu.

Wakati huo huo, wakosoaji wake kutoka upande wa pili, Democrat, hawaoni uwezekano wa uchaguzi wa haki na huru, wakikumbushia skendo ya ushindi wa Rais Trump mwaka 2016.

Itabaki kwenye kumbukumbu za wengi kuwa Urusi ilitajwa kushiriki kwa kiasi kikubwa kumpatia ushindi Rais Trump.

Mazingira yale yamemuibua mpinzani wake, Biden, aliyesema anahisi Rais Trump atashinda kwa figisu za aina ile.

“Ni wasiwasi wangu mkubwa, hiyo ndiyo hofu pekee niliyobaki nayo. Huyu rais ataiba tena matokeo ya uchaguzi huu,” anasema Biden.

Aidha, wachambuzi wanahofia kuchelewa kwa mchakato wa uchaguzi kulikotokana na janga la Corona kunaweza kusababisha hata matokeo ya uchaguzi yasitangazwe usiku wa siku ya upigaji kura.

Hiyo itatokana na muda mwingi utakaotumika katika mchakato wa kuhesabu kura zilizopigwa kwa baruapepe na zile zitokanazo na njia ya posta.

Katika hilo, mkurugenzi wa masomo ya uchaguzi wa Chuo cha Sheria cha Virginia, Rebecca Green, anasema:

“Hili ni janga linalokuja taratibu. Nafuatilia kwa makini na inanitia hofu.”

Athari za Corona katika Uchaguzi huo zilionekana wazi katika majimbo ya Wisconsin na Georgia.

Vifaa vya upigaji kura vilichelewa kufika katika maeneo hayo ambayo watu wake walikuwa nyumbani kukwepa maambukizi ya Corona, hivyo kusababisha foleni kubwa.

Huku zoezi la kuhesabu kura likitarajiwa kuchukua muda mrefu hadi matokeo yatakapotangazwa, wachambuzi wanahisi kunaweza kuwapo kwa hoja ya kutotendewa haki miongoni mwa wagombea.

Democrat pia wameibua madai mengine, wakisema wana wasiwasi mfumo wa upigaji kura kwa baruapepe unaweza ‘kuchezewa’ kwa lengo la kuwakwamisha wananchi kutekeleza haki yao hiyo ya kikatiba.

Hofu ya aina hiyo inawakumbusha wajuzi wa siasa za Marekani kile kilichotokea kati ya wagombea Rutherford Hayes na Samuel Tilden katika Uchaguzi wa mwaka 1876, ambapo mshindi wa kiti cha urais alitangazwa siku mbili kabla ya kuapishwa.

Mbali ya hilo, wengine wanakumbusha utata wa matokeo katika Uchaguzi wa mwaka 2008, ukisababisha kura kuhesabiwa mara mbili katika Jimbo la Florida.

Pia, kile kilichotokea mwaka 2000, ambapo ni Mahakama Kuu ndiyo iliyoamua matokeo ya kiti cha urais, hakijasahaulika katika siasa za Marekani.

Vilevile, sarakasi za matokeo ya uchaguzi zilijirudia mwaka juzi na kushuhudiwa katika majimbo ya Florida na Georgia.

Kilichotokea Georgia ni wataalamu wa uchaguzi kubaini makosa katika kumbukumbu za usajili wa wapigaji kura.

Macho ya wachambuzi yameelekezwa Georgia, North Carolina na Texas, yakifahamika kuwa ni majimbo ambayo raia wake wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya unyanyasaji kila kinapofika kipindi cha uchaguzi.

“Tunaona maofisa wakipita maeneo mbalimbali wakitumia ugonjwa (Corona) kama tishio la watu kutokwenda kupiga kura,” anasema Kristen Clarke, rais wa Kamati ya Wanasheria wa Haki za Kiraia.

Hilo linampa hofu hata rais aliyetoka madarakani kumpisha Trump, Barack Obama, aliyesema chama chake, Democrat, kinahofia serikali iliyoko madarakani inatumia Corona kutisha raia wasiende kupiga kura.

Ifahamike kuwa Biden ndiye aliyekuwa makamu wa rais wa Obama kwa awamu zote mbili madarakani.

Kutokana na ukaribu wao, haikushangaza kumsikia Obama akimpiga kijembe Rais Trump kwa kusema raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika atakuwa amekosea kumnyima kura Biden.

Tafiti nazo haziko mbali kama ambavyo zimekuwa zikijitokeza kutoa taswira ya matokeo kila kinapofika kipindi cha uchaguzi.

Moja kati ya tafiti hizo, imeonesha asilimia kubwa (53%) ya waliojiandikisha watampigia kura Biden.

Lakini sasa, asilimia tano ya waliosema watampigia kura Biden, pia walisisitiza kuwa wanaweza ‘kupindua meza’, yaani kubadili uamuzi na kumpa Rais Trump aendelee kwa awamu yake ya pili madarakani.

Kati ya asilimia 47 waliojipambanua kuwa ni wafuasi wa Rais Trump na kusema watampigia kura, asilimia nne walisema uamuzi unaweza kubadilika ifikapo Novemba 3.

Utafiti huo pia unaonesha kuwa Biden ni kipenzi cha Wamarekani wenye asili ya Afrika, Asia na Hispania, pia akiwa na ushawishi mkubwa kwa wanawake.

Rais Trump yeye bado anatamba na wazee (ingawa ushawishi umepungua) na kundi la raia wasio na elimu, kama iliyokuwa katika Uchaguzi wa mwaka 2016.

Ukija kwa wazungu, kwa maana ya Wamarekani wenye ngozi nyeupe, asilimia kubwa (54%) wanamkubali Rais Trump.

Ikimaanisha kwamba, ni asilimia 45 tu waliosema wanamuunga mkono Biden katika kinyang’anyiro cha urais.

Ukija kwenye kundi la wasomi, Biden ana mvuto zaidi vyuo vikuu (asilimia 68), ukilinganisha na Rais Trump anayependwa vyuo vya kati, sekondari na chini ya hapo (asilimia 53).

Utafiti pia ulibaini kuwa sehemu kubwa ya waliopiga kura katika Uchaguzi uliopita na Rais Trump akamshinda Clinton, watashiriki tena safari hii.

Zaidi ya kushiriki, utafiti uligundua kwamba wengi wao wamebaki kwenye vyama walivyovipigia kura mwaka 2016.

Mathalan, kati ya walioulizwa, asilimia 94 walisema walimpigia kura Rais Trump na watafanya hivyo tena dhidi ya Biden ifikapo Novemba 3 mwaka huu.

Ni asilimia tano tu waliosema wamebadili upepo, wakimaanisha safari hii watapeleka kura yao kwa mpinzani, Biden.

Ukija upande wa pili, asilimia 96 ya waliojitokeza mwaka 2016 na kumpigia kura Clinton wamesema watampigia Biden. Ni asilimia nne tu waliosema watahamia upande mwingine kwa kumpigia kura Rais Trump.

Sambamba na hilo, raia ambao mwaka 216 hawakumpigia Rais Trump wala Clinton nao safari hii wametupa karata yao kwa Biden, wakiwa ni asilimia 55. dhidi ya 39 za walimgeukia Rais Trump.

Hata hivyo, ingawa tafiti si za kupuuza, ukweli ni kwamba hazitoshi kuhitimisha matokeo ya uchaguzi ujao.

Ndiyo, bado ni ngumu kutumia utafiti huo kutaja atakayeibuka kidedea kati ya Rais Trump na Biden.

Iko hivi; katika Uchaguzi wa mwaka 2016, ziliibuka tafiti nyingi za aina hii zikimtaja Clinton kuwa ndiye angemgaragaza Rais Trump.

Kufikia Agosti, Clinton alitajwa na tafiti kuwa na ushindi wa asilimia 55 na mwenzake huyo angeambulia asilimia 42.

Hata wafuasi wa Rais Trump, ni asilimia 74 tu walioamini angeshinda uchaguzi ule.

Je, nini kilichotokea zaidi mfanyabiashara huyo kuingia Ikulu na sasa anaisaka awamu yake ya pili akiwa rais wa Marekani?

Hivyo basi, Novemba 3 itatoa majibu sahihi juu ya hatima ya Rais Trump na Biden.

Ni aidha aendelee au akabidhi kijiti kwa mwanasheria huyo anayetokea familia ya Kikatoliki.

The post Biden na hofu ya Rais Trump kuiba kura appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *