img

Watia nia ubunge, wajumbe waliotumia rushwa waondolewe,on August 13, 2020 at 1:39 pm

August 29, 2020

NA DK. HELEN KIJO-BISIMBA BINAFSI huwa sifuatilii sana masuala ya uchaguzi ndani ya vyama. Mara nyingi huwa ninaona tu watu wanaosemekana kuwa ndiyo watapeperusha bendera za vyama vyao na ninawasubiri kwenye sanduku la kura. Mwaka huu imekuwa tofauti sana pale nilipoona kwenye mitandao ya kijamii watu waliokuwa wakisemekena ni watia nia wa Chama Cha Mapinduzi
The post Watia nia ubunge, wajumbe waliotumia rushwa waondolewe appeared first on Gazeti la Rai.,

NA DK. HELEN KIJO-BISIMBA


BINAFSI huwa sifuatilii sana masuala ya uchaguzi ndani ya vyama. Mara nyingi huwa ninaona tu watu wanaosemekana kuwa ndiyo watapeperusha bendera za vyama vyao na ninawasubiri kwenye sanduku la kura.

Mwaka huu imekuwa tofauti sana pale nilipoona kwenye mitandao ya kijamii watu waliokuwa wakisemekena ni watia nia wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakihojiwa na watu waliosemekana kuwa ni wajumbe wa vikao vya kuwapigia kura hao watia nia.

Kwanza mwaka huu katika ngazi ya majimbo ya ubunge watia nia walionekana kuwa wengi na idadi hiyo ni kutoka kwa watu wa kila aina, ndiyo maana hata ilikuwa ni rahisi sana kuwasikia na kuweza kuona vinavyoendelea katika vikao vya kupigiwa kura. Sikubahatika kuona kilichojiri katika vyama vingine kwa hiyo nilifuatilia zaidi niliyoyaona na kuyasikia ya chama tawala tu.

Jambo lililokuwa dhahiri ni kwamba kuna watu waliokuwa wamekwenda kutia nia wakawa wamepewa kama hakikisho kuwa wao ni watu wanaokubalika na ambao wana uwezo na hivyo wataweza kupigiwa kura bila taabu.

Wapo walioaminishwa kuwa kwa kufahamiana na wajumbe itawawezesha kupita bila shaka. Wapo walioenda bila kujua mambo huwa yako vipi katika mchakato huo nao walibaki na mshangao.

Ndio maana mwisho wa siku tulikutana na kauli kuwa ‘wajumbe si watu’. Wajumbe waliacha kuwa watu pale walipokuwa wamemmwagia mtu misifa yote na mtu huyo akaambulia kura moja kama si hola kabisa.

Nimejihoji sana kwanini watia nia wengi walikuwa wakilalamika sana kwani ninavyofahamu mimi katika uchaguzi wowote mjumbe au mpigakura ana haki ya kumchagua ampendaye na asifungwe  kumchagua anayemfahamu au hata ndugu yake.

Na waswahili husema asiyekubali kushindwa si mshindani. Hata hivyo kilichokuja kunifumbua macho ni pale niliposikia habari za watu waliotuhumiwa au kusemekana kuwa walijihusisha na rushwa katika hatua hiyo ya kutia nia.

Sikuelewa kabisa kuwa inawezekanaje mtu kudiriki kutoa rushwa katika kuwania uongozi. Nilipatwa na mshangao pale mmoja wa aliyetia nia nilipomsikia akisema yeye aliambiwa wazi kuwa kama hujawapooza wajumbe hata kidogo asitegemee kupata chochote.

Kwa kauli hiyo alisema hakuwa na fedha wala chochote cha kuwapooza, yeye alikwenda kutia nia akijua akipewa dhamana atapambana huko bungeni kuhakikisha watu wa jimbo lake wanapata manufaa. Mwisho wa siku alimpata mjumbe mmoja aliyempigia kura kwa hiyo akawa na kura yake moja.

Wapo waliosema kuwa walipewa hakikisho lakini inaelekea hawakuweza kukidhi matakwa ya wajumbe kwa kiasi cha mategemeo yao, hivyo walijikuta hawakupata kura au walipata chache sana.

Kwa uhakika kabisa kama ni kweli kuwa watia nia inabidi wawapooze wajumbe kwa maana ya rushwa na hao wajumbe waangalie dau la mtia nia, ndiyo wampe kura hapa tujue kabisa tuna tatizo kubwa kuliko tunavyoweza kufikiria.

Mtu anayetafuta kuwa kiongozi kwa ngazi ya ubunge au hata ngazi nyingine yoyote anatakiwa kuwa na sifa za kiongozi, mojawapo ikiwa ni kuwa na maadili ya hali ya juu. Kupewa dhamana ya uongozi halafu umeingia kwenye mchakato ukiwa na mikono michafu hutapata mahali pakuweza kuisafisha ili uweze kuifanya hiyo kazi kwa usafi.

Wajumbe nao ni viongozi walioaminiwa na chama chao ili waweze kukisaidia kuwachuja watu watakaoweza kupitishwa na chama ili wakiwakilishe chama hicho katika uchaguzi.

Iwapo wajumbe nao hawatawasikiliza watia nia kwa hoja zao na ubora walionao  wakaamua kusubiri kupoozwa na wakishapoa wakampa mtu kura kwa kuwa kawapooza nao pia hapaswi kabisa kuwepo katika huo mchakato kwani wanaaibisha na kufedhehesha mchakato mzima.

Nilipokuwa nawasikiliza watia nia waliorudi wakiwa wamesawijika nilijiuliza sana iwapo waliumia kwa vile wao waliwapooza wajumbe lakini kipoozeo chao hakikutosha au ni kwa vile hawakuwa na kipoozeo na wenzao waliopooza ndio wamepita?

Nilimsikia kiongozi mmoja wa chama husika akisema wakibainika waliotumia rushwa  kupitishwa na wajumbe watawakata au watawaondoa.

Nikajiuliza maswali hapa kuwa inavyoonekana zipo taarifa kuwa kulikuwa na rushwa. Iwapo hivyo ndivyo wale waliotia nia halafu ikaonekana walipitishwa kwa rushwa wakiondolewa wao wale wajumbe waliopokea rushwa nao watafanywaje?

Niliwaza kuwa iwapo kulikuwa na harufu yoyote hata ndogo ya rushwa kwenye huo mchakato kama kweli tunatafuta kuondoa rushwa nchi hii basi watia nia na wajumbe wote wangeondolewa na mchakato ukaanza upya kwani mtoa rushwa na mpokea rushwa ni sawa kabisa. Na wale waliokuwa wakiomba rushwa na hawakupewa nao wangewekwa wazi kwani hata hilo nalo si sahihi.

Tumebaki kucheka kuwa ‘wajumbe si watu’, ‘watia nia wamekomeshwa’, lakini hatujaangalia kwa undani tatizo kubwa linaloweza kuwa ndilo shida na kidonda ndugu katika taifa letu. Huu ni mchakato ndani ya chama kilichoko madarakani na huenda ndio hali ilivyo katika  jamii kwa ujumla. Sisi watanzania tumeaminishwa kuwa rushwa inapigwa vita, lakini hatuoni kwa vitendo rushwa ikipigwa vita. Watu wanaongea wakati vipo vyombo vimewekwa kisheria kupambana na kuzuia rushwa. Kwa vile watu wamekuwa wakiongea waziwazi ingeweza kuwa rahisi wakati wa mchakato kama huo vyombo husika vikafuatilia ili kuona kulikoni kati ya wajumbe na watia nia? Kwa hali ilivyo sasa waliopata kura chache wanaweza kusema ni kwa vile wenzao walitoa kitu kidogo na huenda wengine wakasemekana wamepita kwa rushwa na isiwe hivyo kwani fitina nazo zipo. Ilitakiwa ushahidi upatikane wakati huo wa mchakato. Wakikatwa hao waliopata kura nyingi kwa vile wanasemekana walitumia rushwa je iwapo waliokosa walikosa kwa vile dau lao lilikuwa dogo lakini nao walitoa rushwa hapo kutakuwa na tiba kweli? Na iwapo wapo watu wenye ushawishi na wasiotoa rushwa hata kama ni wachache kwa jinsi maneno yalivyozagaa nao huenda wakafikiriwa kuwa wametoa rushwa.

Ili kuusafisha huo mchakato ilibidi pale viongozi walipopokea taarifa kuwa kulikuwa na hali ya uwepo wa rushwa wangeufuta mchakato na kuanza upya kwa kutafuta mfumo mwingine wa kuwapata wagombea katika chama chao.

Ninakumbuka matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 1998 yalifutwa kote nchini kwa vile ilifahamika kuwa mtihani ulikuwa umevuja. Ilikuwa ni gharama kubwa sana lakini mamlaka ya wakati huo haikuwa tayari kuendelea na mchakato uliokuwa na dosari kama hiyo.

Ilibidi wanafunzi wale warudie tena kufanya mtihani nchi nzima. Na huu mchakato ambao umesemwa kiasi kikubwa hivi wajumbe wakipewa majina na watia nia wakizodolewa, ingebidi wahusika waangalie kulikoni na ikibidi wajitahidi kurekebisha au kusafisha.

Kusema kwamba watawafuta wanaodhaniwa kuhusika na rushwa, nadhani kuwasubiri katika vikao vya juu bila  ushahidi wa kutosha au ushahidi wa kimazingira au wa kusikiasikia itakuwa si haki. Kwa vile hata wajumbe nao watakuwa hawako safi kama waliwapitisha watu kwa rushwa. Haki huinua taifa na rushwa hupofusha macho.

0713 337240

The post Watia nia ubunge, wajumbe waliotumia rushwa waondolewe appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *