img

Utitiri wa wanaoutaka ubunge, udiwani 2020 kunani?,on August 13, 2020 at 1:43 pm

August 29, 2020

NA ANNA HENGA KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inampa kila raia wa Tanzania haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi katika ibara ya 21(i). Kwa miaka mingi hapa nchini kupitia viongozi na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa demokrasia pamoja na asasi za kiraia wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali
The post Utitiri wa wanaoutaka ubunge, udiwani 2020 kunani? appeared first on Gazeti la Rai.,

NA ANNA HENGA


KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inampa kila raia wa Tanzania haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi katika ibara ya 21(i).

Kwa miaka mingi hapa nchini kupitia viongozi na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa demokrasia pamoja na asasi za kiraia wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kulinda demokrasia na utawala bora hapa nchini Tanzania.

Mojawapo ya shughuli wanazofanya wadau wa demokrasia kwa ushirikiano na asasi za kiraia ni pamoja na kutoa elimu ya mpiga kura, kutoa elimu ya uraia pamoja na kuwajengea uwezo wananchi katika ngazi mbalimbalili kuhusu umuhimu wa ushiriki wao katika masuala ya utawala wa nchi.

Tanzania ilirudi katika mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1992 na tangu wakati wa Rais Mstaafu Ally Hassan Mwinyi hadi awamu ya kwanza ya Rais John Magufuli, Watanzania wamekuwa wakishiriki kuchagua na kuchaguliwa kuwa viongozi katika chaguzi za Rais, Wabunge na Madiwani.

Kwa miaka yote hiyo haijawahi kutokea mafuriko hayo ya wagombea wengi ubunge hasa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo mwaka huu zaidi ya wagombea 8,000 wamejitokeza.

Kwa mfano katika jimbo moja watia nia ya kugombea nafasi za ubunge au udiwani wamekuwa zaidi ya 100 jambo ambalo halikuwahi kutokea tangu nchi hii ilipoingia tena katika mfumo wa vyama vingi. Kuelekea uchaguzi mkuu wa wagombea wengi waliojitokeza wamekuwa na sifa tofauti kama wasomi wa fani mbalimbali wakiwepo, madaktari, wahandisi, wanahabari, mawakili, wanasiasa wakongwe na wafanyabiashara.

Haijawahi kutokea pia hata katika nafasi ya ubunge wa viti maalumu kiti kimoja kugombewa na wanachama zaidi ya 100 wenye sifa za aina mbalimbali. Hii ni kusema kwamba safari hii kila mtu ametamani kutia nia ya kuwa ubunge au udiwani tofauti na miaka iliyopita na hapa ndipo swali langu linapokuja kwamba je kunani?

Huenda hizi ndio sababu za wengi kutamani nafasi za uongozi mwaka huu.

Kama nilivyosema katika utangulizi hapo juu ibara ya 21(i) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inampa kila raia haki na uhuru wa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi. Kutokana na watu wengi wakiwemo wasomi kujitokeza kutia nia ya kuutaka uongozi, sababu zimetajwa nyingi za kuweza kujibu swali la ni nini chanzo cha hamasa hii ya ghafla, kwa watu wa kada mbalimbali kujitokeza kugombea na baadhi kuacha kazi zao walizokuwa wakifanya kwa miaka mingi.

Kwanza wachambuzi wa masuala ya kisiasa pamoja na wanaharakati ikiwemo wasomi wamekuwa wakitoa maoni tofauti juu ya mafuriko haya. Wapo wanaosema watu wamejitokeza kwa wingi kutokana na kukua kwa demokrasia na kudhibitiwa kwa rushwa. Vilevile wengine wamesema kuwa hii imetokana na mabadiliko ya kimkakati na kiuongozi yaliyofanywa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wengine wanasema watu wamejitokeza kwa wingi kwa sababu ni njia mojawapo ya kutafuta fursa za uteuzi kwani wanajua hawawezi kupitishwa kugombea katika maeneo yao.  Uchaguzi ni fursa kama fursa nyingine kama ilivyo misimu mbalimbali ya kilimo au biashara watu hujitokeza na kuchukua fursa.

Lakini wapo wanaosema ni hofu tu ambayo imetanda katika jamii kuwa, bila kuonekana unaunga mkono juhudi za serikali, basi biashara zako na kazi zako ziko hatarani.

Pia wapo wasomi waliokwenda mbali zaidi na kueleza udhaifu wa baadhi ya wabunge katika bunge lililopita umechangia kila mtu kujiona ana uwezo wa kuwa mbunge. Pia wapo walioingia kwenye kinyang’anyiro hicho wakiamini wakipata fursa watakwenda kuisaidia serikali ya awamu ya tano, kupambana na hoja za upinzani kwani mara kadhaa zimekuwa zikiteka mijadala ya bunge.

Hivyo kujitokeza wagombea wengi kuna taswira tofauti kama wanavyosema wachambuzi, wasomi na wanaharakati. Michakato ya kura za maoni ndani ya vyama inaendelea, hivyo viongozi wa vyama watakuwa na mtihani mkubwa kupata wagombea sahihi.

Kuna wagombea ambao walikuwa na nafasi kubwa serikalini, kama wakuu wa mikoa, makatibu wakuu, maofisa tawala mikoa na viongozi wa taasisi muhimu za serikali wakiwemo mawaziri pamoja na spika wa bunge nao walichukua fomu na kupigiwa kura na kushinda, hivyo wanasubiri maamuzi ya mwisho ya Kamati Kuu kwa upande wa chama tawala.

Kwa upande wa vyama vya upinzani kama Chadema pamoja na ACT-Wazalendo, tayari wameshasimamisha wagombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kila raia ana haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi; kama mdau wa haki za binadamu na utawala bora napenda kusisitiza kuwa wote waliojitokeza kutia nia ya kutaka kuwa wabunge au madiwani kupititia chama chochote wanalindwa na Katiba ya nchi ya mwaka 1977 ibara  ya 21 kifungu cha (1), ambacho kinaendeleza bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 5, ya 39 na ya 67 ya Katiba na ya Sheria za nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa.

Kwa hiyo jamii inatakiwa kutambua kuwa pamoja na kuwepo kwa sababu nyingi zilizoweza kuwafanya watu kujitokeza kutaka kuwania nafasi za uongozi bado katiba inawalinda.

Tukumbushane pia kuwa ibara hiyo inawapa haki ya kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria. Kilichozua mjadala ni dhamira zao, katika kutaka uongozi je, wanasukumwa na kutetea masilahi ya umma ama ni kwa maslah yao binafsi?

Naamini wapo ambao wana dhamira za dhati kabisa za kutaka kuwatumikia wananchi katika maeneo yao na pia wapo wachache ambao wao wanajua vilivyo shida za wananchi wao.

Uzuri ni kwamba wagombea wenye dhamira za dhati kumbukumbu zao zinasomeka kwenye mioyo ya watu, zimeacha alama ya uadilifu wao, utu wao na upendo wao kwa wananchi ambao sasa wanaomba kuwapa kura.

Nikiwa kama mdau mkubwa wa demokrasia na utawala bora, napenda kutumia fursa hii kutoa rai kwa serikali pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuendelea kushirikiana kwa usawa na wagombea wote kutoka vyama vyote bila ubaguzi wala upendeleo ili nchi iweze kufikia lengo la kukuza demokrasia na utawala bora.

Ninasisitiza haya kwa kuwa kwa sasa tumeanza kushuhudia malalamiko ya baadhi ya viongozi na wagombea kulalamika kuwa kuna vitisho vya kutaka kuuawa. Ni vyema Jeshi la Polisi likaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda raia na mali zake hasa katika wakati huu tunapoelekea kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu kwani uchaguzi sio uwanja wa vita.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

The post Utitiri wa wanaoutaka ubunge, udiwani 2020 kunani? appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *