img

Uhifadhi wa misitu ya asili na maeneo ya kale unavyodumisha utamaduni, kukuza uchumi,on August 13, 2020 at 1:49 pm

August 29, 2020

NA VICTOR MAKINDA TANZANIA ni nchi iliyojaliwa mito mingi, mabonde mengi, milima, bahari, maziwa, mabwawa na misitu mingi ya asili ambayo ndani yake kuna utajiri mkubwa wa mali asili na mali kale. Sambamba na hayo Tanzania imejaliwa kuwa na makabila mengi yenye tamaduni tofauti tofauti. Tanzania ni nyumbani mwa makabila zaidi ya 120 yenye asili
The post Uhifadhi wa misitu ya asili na maeneo ya kale unavyodumisha utamaduni, kukuza uchumi appeared first on Gazeti la Rai.,

NA VICTOR MAKINDA


TANZANIA ni nchi iliyojaliwa mito mingi, mabonde mengi, milima, bahari, maziwa, mabwawa na misitu mingi ya asili ambayo ndani yake kuna utajiri mkubwa wa mali asili na mali kale.

Sambamba na hayo Tanzania imejaliwa kuwa na makabila mengi yenye tamaduni tofauti tofauti. Tanzania ni nyumbani mwa makabila zaidi ya 120 yenye asili na historia tofauti tofauti ambapo ikiwa tamaduni hizo zikatumiwa vizuri, zinaweza kuwa chanzo cha kipato na kukuza uchumi.

Kana kwamba hilo halitoshi Tanzania iliwahi kutawaliwa na mataifa tofauti ya kigeni kutoka Bara la Ulaya, ikiwa ni Wajerumani na Waingereza. Waarabu wanatajwa kama watu wa mwanzo kufika pwani ya Afrika ya Mashariki ikiwemo Tanganyika na Zanzibar ambapo waliendesha biashara ya utumwa na kuacha historia kubwa maeneo hayo. Bagamoyo, Kilwa na Zanzibar ni miongoni mwa maeneo hayo ambayo biashara hiyo haramu ilifanyika.

Babu zetu kwa nyakati na vipindi tofauti walipambana na tawala hizo na kuacha maeneo mengi ambayo yanaeleza historia ya mapambano hayo. Maeneo hayo yanapatikana ndani ya misitu ya asili na mengine nje ya misitu hiyo.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, inayahifadhi maeneo hayo na maeneo mengine mengi kwa ajili ya urithi na faida kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.

Hatua hiyo ya uhifadhi na usimamizi wa maliasili inatekelezwa na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo. Moja ya taasisi hizo ni Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (FFS).

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest Services Agency, TFS) ulianzishwa kisheria kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali (GN 269) la tarehe 30/7/2010 na kuzinduliwa rasmi tarehe 18/7/2011. Kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu ni kwa mujibu wa Sheria ya Wakala “the Executive Agencies Act Cap. 245 (Revised Edition 2009)”, pamoja na Sera ya Misitu ya mwaka 1998, Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998, Sheria za Misitu na Nyuki Sura 323 na Sura 224 za mwaka 2002.”anaanza kueleza Suleiman Burenga, Ofisa Habari na Mahusiano wa TFS kanda ya Mashariki. Kanda inayohudumia mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Lengo Kuu la Kuanzishwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Wakala wa Huduma za Misitu umeundwa kwa madhumuni ya kuhakikisha uwepo wa usimamizi madhubuti na wenye ufanisi na tija wa rasilimali za misitu na nyuki, huku wakala ukijikita katika kuongeza ubora na thamani ya kifedha katika kutoa huduma kwa umma na kuendelea kukuza na kuboresha uwezo wa kutoa huduma kwa umma.

Majukumu ya wakala yameongezeka licha ya kutoshughulikia sera na sheria. Wakala umepanua wigo kibiashara na kuongeza maeneo ya uzalishaji miti na mazao ya nyuki ili kukidhi mahitaji halisi, shughuli za uwekezaji, kuboresha njia mbadala za mapato na uboreshaji wa hifadhi za misitu na nyuki kwa ujumla.

Dira ni kuwa kielelezo bora katika usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki wakati dhima ya wakala ni kuwa na usimamizi endelevu wa rasilimali za kitaifa za misitu na nyuki ili kuchangia mahitaji ya kijamii, kiuchumi, ki-ikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho”. Anaanza kueleza Suleman Burenga, Ofisa Habari na Mawasiliano TFS, kanda ya Mashaliki alipozungumza na Rai mjini Morogoro hivi karibuni.

Burenga anaongeza kuwa pamoja na mambo mengine mengi TFS ina jukumu la kuhifadhi maeneo ambayo yana historia ya kale au tunaweza kusema mambo kale. Anayataja maeneo hayo kuwa na utajiri mkubwa wa kihistoria akitolea mfano eneo la mji mkongwe na Kaole yanayopatikana mkoani Pwani.

Burenga anasisitiza kuwa ni muhimu maeneo hayo yakahifadhiwa kwa usimamizi na umakini uliotukuka kwa ajili ya kumbukumbu za kihistoria huku yakileta tija kwa jamii kiutamaduni na kiuchumi.

“Kila Taifa lina historia yake. Kila kabila lina historia yake hali kadhalika koo na hata mtu mmoja mmoja. Ni muhimu sana kutunza maeneo ya kihistoria ya mambo kale kwa kuwa yanatupa mwanga na picha halisi ni wapi tumetoka, wapi tulipo na wapi tunakwenda.

Hivyo TFS sambamba na jukumu letu zito la kutunza na kusimamia misitu ya asili, pia tunatekeleza jukumu hili muhimu la kutunza mambo kale kwa umakini mkubwa. Zipo faida nyingi za kuhifadhi maeneo ya misitu na maeneo ya asili lakini kubwa ni kusaidia jamii inayozunguka maeneo hayo kiuchumi na kiutamaduni,”anaeleza Burenga.

Kauli ya Burenga inaungwa mkono na Wilfred Pima, Ofisa Misitu na shamba la miti la Ukaguru mkoani Morogoro lililo chini ya TFS. Pima anaeleza kuwa katika misitu wa mazingira ya asili ya Ukaguru kuna utajiri mkubwa wa kiikolojia na kihistoria.

Anataja uwepo wa msitu mnene wenye aina nyingi za mimea na miti ambapo ndio chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa wilaya ya Gairo mkoani Morogoro. Pima anasema kuwa misitu ya asili ya Ukaguru ni moyo na mapafu ya wakazi wa wilaya hiyo.

“Maporomoko ya maji ya Mfufumo yanayo patikana ndani ya msitu wa asili wa Milima ya Ukaguru ni kivutio kikubwa cha utalii.  Msitu huo una milima yenye mawe katika baadhi ya maeneo ambapo kuna mapango makubwa ambayo yalikuwa yanatumiwa kwa ajili ya kufanya ibada na toba hapo zamani na mababu zetu.

Mapango hayo yanayojulikana kwa jina la Chigalegale kwa lugha ya Kikaguru, neno lenye maana ya kusujudu. Historia inaeleza kuwa hapo ndipo palikuwa eneo mahususi kwa yeyote aliyekuwa na shida kufika na kuomba shida zake ndani ya mapango hayo.” anaeleza Pima.

Pima anaongeza kusema kuwa katika hifadhi hiyo ya asili yenye utajiri wa kihistoria kuna aina nyingi za vipepeo, mandhari nzuri ya misitu pamoja na hali ya hewa nzuri.

Analitaja eneo hilo kuwa ni eneo zuri la kutalii ambapo mtalii atajifunza mengi ya kihistoria sambamba na kufurahia hali ya hewa nzuri itakayouburidisha mwili na moyo wa mtalii.

Anasema upo mkakati mkubwa wa kuyatangaza maeneo hayo ili yaweze kutembelewa na watu wengi hususani watalii wa ndani ili waweze kujifunza na kuchangia pato la Taifa.

Siyawezi Hungo ni Mhifadhi wa Mambo ya kale Bagamoyo, mkoani Pwani, ambako maeneo ya kihistoria ya Mji Mkongwe na Kaole yapo chini ya TFS. Anaunga mkono kauli ya Wilfred Pima, kuwa uhifadhi wa mambo ya kale una tija kubwa kwa Taifa kiutamaduni na kiuchumi.

Siyawezi anasema kuwa mji wa Bagamoyo ni kitovu cha historia ya mambo ya kale huku ukiwa umebeba utajiri mkubwa wa historia ya biashara ya utumwa, utamaduni wa watu wa pwani na dini za kiislamu na kikristu.

“Mji wa Bagamoyo umesheni historia adhimu na adimu. Tuna dhamana ya kuutunza mji huo kwa mintaarafu ya kutunza historia ambapo ulimwengu mzima unatamani kuijua.

Ukweli ni kwamba unapozungumzia biashara ya utumwa huwezi kuacha kuitaja Bagamoyo. Unapotaja majengo ya kale huwezi kukosa kuitaja Bagamoyo. Bagamoyo ni miongoni mwa miji ya kwanza kabisa kupokea wageni kutoka Mashariki ya mbali, Kati na Bara la Ulaya. Hapa pana chemichemi ya historia ya miaka zaidi ya 1000 iliyopita.

Siyaweza anasema kuwa tofauti na maeneo mengine yenye historia ya asili, Bagamoyo inapata watalii wengi wa ndani kuliko wa nje huku akitaja uchakavu wa majengo ya kale kuwa ni moja ya changamoto zinazokabili uhifadhi wa eneo hilo.

“Mji wa Bagamoyo uliosheheni mambo kale una majengo mengi ya miaka mingi iliyopita. Maeneo kama Kaole na mji mkongwe ni hazina ya Taifa na ulimwengu kwa ujumla. Kwa sasa baadhi ya majengo yamechakaa na yanahitaji ukarabati hususani yale yanayomilikiwa na watu binafsi ambayo watu hao waliyarithi kutoka kwa mababu zao.

Tatizo ni watu hao hawataki kuyakarabati au hawana uwezo wa kufanya hivyo. Hii kwa mtazamo wangu ni changamoto kwani majengo hayo yanaweza kubomoka na kuharibu historia nzuri ya mji huo wa kale kabisa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki wenye utajiri wa kihistoria na wenye tija kubwa kiutamaduni na kiuchumi,”anaeleza Siyawezi.

Naye Ofisa Misitu, Hifadhi ya Misitu ya  Asili ya Uluguru ambaye pia anakaimu nafasi ya Ofisa Utalii, Zarina Shaweji anaitaja Hifadhi ya Milima ya Uluguru kama eneo linalotoa mchango mkubwa kiutamaduni na kiuchumi hapa nchini.

Zarina anasema kuwa Hifadhi ya Misitu ya Asili ya Uluguru ni eneo linalokaliwa na utajiri mwingi wa rasilimali mbalimbali pamoja na maeneo ya kihistoria.

Anaongeza kusema pamoja na mambo mengine mengi ya kihistoria kwenye msitu, humo kuna njia ya asili ya kale ya Wajerumani ambapo kilele cha njia hiyo kinampa fursa mtalii kuuona mji wote wa Morogoro kwa uzuri kabisa.

“Licha ya hifadhi hii ya asili ya Uluguru kuwa na utajiri wa historia ya kabila la Waluguru, katika hifadhi hii ya asili kuna aina nyingi za vinyonga wenye pembe. Wapo vinyonga wenye pembe 3,2 na moja ambapo kinyonga mwenye pembe 2 ni kinyoga anayepatikana milima ya Uluguru pekee na huwezi kumpata maeneo mengine duniani. Lakini pia kuna aina ya ndege maarufu katika Hifadhi hii ya asili ya msitu wa wa Uluguru. Msitu huo  ni nyumbani kwa ndege aina ya  Nkurumbizi ndege anayepatikana hifadhini hapo tu na hapatikanai maeneo mengine Duniani. Sambamba na hilo yapo maporomoko maarufu ya  maji yanayojulikana kama maporomoko ya maji ya Hululu,”anasema Zarina.

Zarina  anaongeza kusema kuwa ndani ya Hifadhi ya Asili ya  Msitu wa Uluguru ndipo panapo patikania uwanda oevu wa Lukwangule ambako ndipo chanzo cha mto Ruvu mto ambao ni moyo wa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na maeno mengi ya Mkoa wa Pwani.  Itaendelea Alhamisi ijayo….

The post Uhifadhi wa misitu ya asili na maeneo ya kale unavyodumisha utamaduni, kukuza uchumi appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *