img

Siku ya Vijana Kimataifa na umuhimu uchaguzi wa mwaka huu,on August 13, 2020 at 1:52 pm

August 29, 2020

NA FREDERICK FUSSI JANA Agosti 12 mwaka huu, vijana wote ulimwenguni na Tanzania kwa ujumla waliadhimisha Siku ya Vijana Kimataifa. Siku hiyo iliyopewa kauli mbiu ya “Ushirikishwaji wa Vijana kwa ajili ya Juhudi za Ulimwengu” ambayo ni tafsiri yangu isiyo rasmi ya maneno ya lugha ya kingereza yasemayo“Youth Engagement for Global Action” . Hapa nchini kwetu
The post Siku ya Vijana Kimataifa na umuhimu uchaguzi wa mwaka huu appeared first on Gazeti la Rai.,

NA FREDERICK FUSSI


JANA Agosti 12 mwaka huu, vijana wote ulimwenguni na Tanzania kwa ujumla waliadhimisha Siku ya Vijana Kimataifa. Siku hiyo iliyopewa kauli mbiu ya “Ushirikishwaji wa Vijana kwa ajili ya Juhudi za Ulimwengu” ambayo ni tafsiri yangu isiyo rasmi ya maneno ya lugha ya kingereza yasemayo“Youth Engagement for Global Action” . Hapa nchini kwetu tunaweza kuamua kusema kuwa “Ushirikishwaji wa Vijana kwa ajili ya Juhudi za Tanzania”. Kwa hiyo basi ningependa leo tujadili juu ya umuhimu wa siku hii ya kumbukumbu kwa vijana kuangalia kwa namna gani vijana wa Tanzania wanashiriki na kushirikishwa katika juhudi za maendeleo nchini hususan mwaka huu wa uchaguzi.

Hapa nchini vijana wanatambuliwa kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Vijana inayotamka bayana kuwa vijana ni kati ya umri wa miaka 15 na 35. Huu ni umri ambao vijana rika wa miaka 15 na 17 wanakuwa ndio kwanza wapo katika vidato vya mwisho vya elimu ya sekondari. Ushiriki wa vijana wa rika hilo upo hasa kwenye ngazi za maamuzi ya kaya ama familia.

Je familia zetu hapa nchini zinashirikisha vijana rika hawa kufanya maamuzi muhimu ya kifamilia yanayoathiri kesho na hatma zao. Je wanashiriki kuamua wasome shule za umma kule kwenye utoaji wa elimu bila malipo au wanashirikishwa na wazazi wao kuamua wakasome shule za binafsi?

Swali hili majibu yake ni mengi na inategemea na uwezo wa kifedha wa wazazi. Endapo wazazi hawana uwezo wa kumudu gharama za shule za binafsi maamuzi huwa ni kusoma shule za umma, la wazazi wana uwezo kifedha basi watoto wanaweza kusoma shule binafsi. Suala la kipato cha kaya ama familia kwa maana ya wazazi wote wawili baba na mama linaweza kuathiri ushirikishwaji hafifu au kamilifu wa vijana rika kati ya umri wa miaka 15 na 17.

Jukumu la kutoa fedha za kuendesha familia mara nyingi huwa ni la baba wa familia na endapo mama pia akiwa na vyanzo vya mapato anaweza au asiweze kuchangia fedha hizo.

Uwiano wa madaraka ya familia kuamua vijana rika wanaweza kushirikishwa au lah, pia linaweza kuathiriwa na kipato duni cha mama wa familia.

Hili linaweza kuathiri machaguo ya watoto wa kike hasa kuamua wakasome shule zipi na endapo baba wa familia angewezaje kugharamia masuala ya watoto wa kike hasa ugharamiaji wa gharama za manunuzi ya taulo za kike, jambo ambalo ni jukumu la wazazi kugharamia.

Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ni muhimu kuwa na mjadala wa viongozi tutakaowachagua endapo wanaweza kutolea majibu maswali haya ya ushiriki wa vijana katika maamuzi ngazi ya familia na endapo kama Taifa tunahitaji mwongozo wa kuhakikisha ushirikishwaji unaanzia ngazi ya familia, kwenye jamii na hatimaye katika vyombo vya maamuzi ngani ya halmshauri za wilaya, Miji, Manispaa na hatimaye ngazi za Kitaifa na Kimataifa.

Sio sahihi kupuuza ushiriki wa vijana rika katika maamuzi ngazi ya familia na kushadadia ushirikishwaji na ushiriki wa vijana kwenye ngazi za maamuzi katika jamii na Taifa kwa ujumla. Hivyo ushirikishwaji na ushiriki sharti uanzie kwenye ngazi ya familia. Wazazi hasa wababa wawe tayari kugatua madaraka yao kwa wake zao na watoto wao wa kike na wa kiume. Tutakapomudu kuvunja udikteta wa kutoshirikisha vijana wetu katika maamuzi kwenye ngazi za familia hali kadhalika tunaweza kushindwa kuvunja udikteka kwenye ngazi za maamuzi kwenye jamii zetu.

Sauti za vijana na watoto zitakapopoa nafasi ya kusikika na kuheshimiwa katika ngazi ya familia bila shaka mafanikio ya vijana na watoto kusikilizwa, kushiriki na kushirikishwa kwenye ngazi ya jamii yatakuwa ni makubwa mno.

Endapo familia zetu zitajenga utamaduni wa kushirikishwa watoto na vijana kwenye maamuzi ya familia, vijana watajifunza masuala ya uongozi kuanzia ngazi ya familia. Tunapopata viongozi wasio waadilifu, wala rushwa, wababe, wasiojali wenzao kwenye vyombo vya maamuzi na wale wanaotumia vibaya rasilimali za nchi kujinufaisha zenyewe ni kwa sababu hatujaamua kuwaandaa kutokea ngazi ya familia.

Tukibaini matatizo katika uongozi wetu hasa ngazi ya Serikali za mitaa, udiwani na ubunge na hata ngazi za juu kabisa basi matatizo hayo chanzo chake ni ushirikishwaji hafifu wa vijana na watoto kwenye familia zetu.

Tunapoamua kuwapambania vijana washirikishwe kwenye ngazi za maamuzi ya mabaraza ya madiwani, Bungeni na hata kwenye baraza la mawaziri kwa mfano, ni mapambano katika uwanja usio sahihi. Mapambano hasa yanapaswa kuanzia ngazi ya familia.

Vijana wenye rika kati ya miaka 18 mpaka 21 ni wale wanaotarajiwa kuwa wamemaliza kidato cha nne, hivyo kwa mujibu wa mfumo wa elimu yetu ama wataendelea kidato cha tano na sita au wataachwa.

Ushirikishwaji wa kundi hilo la vijana ni ama kufanya maamuzi kuingia kwenye ajira isiyo rasmi au kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi. Je mafunzo ya sekondari ni toshelevu kiasi cha kuwafanya vijana waweze kumudu kujiajiri ndani ya sekta isiyo rasmi ya ajira.

Hawa ndio wapiga kura wa leo, kwa sababu umri wa kupiga kura ni kuanzia miaka 18 lakini pia hawa pia wana sifa za kuweza kuwa wawakilishi wa wenzao ama kwenye baraza la madiwani au ndani ya Bunge.

Umri wa kuwa mbunge angalau uwe na miaka 21. Je hawa ndio kundi la ndugu wajumbe ambao waliopata umaarufu siku chache zilizopita baada ya kuwasulubu wagombea wasomi kwenye ngazi za kura za maoni katika michakato ya ndani ya vyama vya siasa? Unapokuwa na kundi kubwa la vijana ambao hawakupata elimu kubwa, wakaingia kwenye ajira isiyo rasmi, mapato yao ni duni au hawapati ujira kabisa unakuwa unatengeneza umasikini kupitia mfumo wako wa elimu.

Matokeo ya kura za maoni ya kundi la vijana au wazee au watu wazima ambao katika ujana wao wa miaka 18 na 21 hawakupata elimu bora kulinganisha na ile ya wenzao wasomi, yamedhihirisha maana halisi ya uwakilishi. Kuwa ndugu wajumbe waliamua kuwapeleka bungeni wagombea wenye sifa kama zao kwa sababu inaaminika kuwa wajumbe wengi elimu yao sio kubwa kama vile ile ya wagombea wengi.

Somo la wasomi kukataliwa na wajumbe “wenye elimu” duni litufundishe kuwa ndani ya mwaka huu wa uchaguzi 2020 tuna wajibu wa kutafakari dhana ya ushirikishwaji wa watoto na vijana kwenye maamuzi kuanzia ngazi ya familia.

Tusipoweza kuwashirikisha vijana na watoto kwenye familia tutapataje ujasiri wa kuwashirikisha kwenye ngazi za kitaifa? Hivyo nitoe rai kwa wadau wote wa masuala ya vijana, Serikali, asasi za kiraia, wasomi wa vyuo vikuu, wasiosoma na watu wa kada zote kuchukua hatua sasa. Hatua tutakazochukua ni kulingana na nafasi ya kila kundi kwenye jamii. Tusipochukua hatua leo, wajumbe wataendelea kututia adabu siku zijazo.

The post Siku ya Vijana Kimataifa na umuhimu uchaguzi wa mwaka huu appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *