img

Sijaiona agenda ya upinzani kuelekea Oktoba 28 mwaka huu,on August 13, 2020 at 1:37 pm

August 29, 2020

NA DEOGRATIAS MUTUNGI NIANZE kwa kusema bila agenda inayoeleweka upinzani utaendelea kusikia neno dola kama msamiati au kitendawili kisichoteguliwa kwa miaka mingi ijayo. Mafanikio ya upinzani kushika dola yapo mikononi mwao na wao wanalijua hilo,  mchawi wa upinzani ni upinzani wenyewe na tafiti zinaonyesha hivyo, siuchukii upinzani kwa maana kuwa naujua umuhimu wa siasa za
The post Sijaiona agenda ya upinzani kuelekea Oktoba 28 mwaka huu appeared first on Gazeti la Rai.,

NA DEOGRATIAS MUTUNGI


NIANZE kwa kusema bila agenda inayoeleweka upinzani utaendelea kusikia neno dola kama msamiati au kitendawili kisichoteguliwa kwa miaka mingi ijayo.

Mafanikio ya upinzani kushika dola yapo mikononi mwao na wao wanalijua hilo,  mchawi wa upinzani ni upinzani wenyewe na tafiti zinaonyesha hivyo, siuchukii upinzani kwa maana kuwa naujua umuhimu wa siasa za upinzani ndani ya mifumo yetu ya kisiasa katika kufikia maendeleo ya kweli, Kwa ufupi upinzani ni kichocheo cha maendeleo kwenye mifumo ya siasa za mfumo wa vyama vingi bila shaka ukweli huu haupingiki.

Kuendesha siasa za upinzani sio dhambi ingawa sijui kama upinzani unalijua hilo, maana wao hujitenga na kujionyesha ni watoto wa mama wa kambo wanaobaguliwa, upinzani usijione ni yatima kisiasa bali usimame hadharani na kuzitambulisha agenda zao kwa lugha nyepesi na inayoeleweka, upinzani ufahamu kuwa siasa zenye mfumo wa vyama vingi zinaundwa na tabaka la ushindani katika mambo ya msingi, aidha zinahitaji uvumilivu wa hali ya juu sana kufikia malengo yaliyokusudiwa kisiasa na si ubabaishaji hasa kwa nyakati za kizazi cha sasa cha kudadisi na elimu ya kutosha.

Aidha nikiri kuwa maendeleo ya sasa hapa nchini yana mchango mkubwa wa upinzani kwa namna moja au nyingine kwa maana upinzani umekuwa ukipaza sauti chanya kwa kuhoji na kukemea pale inapobidi.

Kwa muhtasari huo hoja yangu inapojengwa  si kuubeza upinzani wala kuukebehi bali ni kuhoji nini agenda ya vyama vya upinzani wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu hapo Oktoba 28 mwaka huu, ni haki kikatiba na kidemokrasia kwa wapiga kura kuuliza na kuhoji maswali kadhaa juu ya dhana ya agenda kwa vyama vya upinzani, kupitia siasa za upinzani tunahitaji kuisikia agenda inasemaje na inasimamia nini ili tuweze kupima na kulinganisha na agenda za CCM, kabla ya kufanya maamuzi ya kutumia sanduku la kura.

Sijaisikia agenda iliyotambulishwa na upinzani hadi sasa yenye maudhui ya kutuvusha Watanzania kwenye hatua ya uchumi wa kati kwenda mbele na kipato kwa mwananchi wa kawaida kinachoakisi maendeleo ya kweli, kinachosikika kwa sasa ni lawama za kuonewa na mamlaka za kiserikali ikiwa ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kisiasa huu ni udhaifu na anguko la kushika dola badala ya hoja zinajengwa lawama za kutaka huruma ya wapiga kura.

Kanuni ya kushika dola ni kuitangaza agenda ya chama husika ikiwa ni pamoja na ilani yake ili kuwafanya wapiga kura  wasisimke kisiasa na kujenga tumaini la kweli juu ya agenda hizo na kutoa fursa ya kushika dola, bila hivyo ni sawa na kumpigia gitaa ngedere ili acheze sendema kamwe bwana ngedere hatocheza sendema kama unavyotaka akuchezee, mpeni ndizi bwana ngedere ndipo atakapo kuchangamkia na kukuchezea sendema, hata mpiga kura anahitaji agenda bora ili akupe fursa ya kushika dola.

Kisiasa agenda ni msingi na mtaji mkubwa wa kufikia malengo ya kushika dola na lengo kuu la chama chochote cha kisiasa ulimwenguni ni kushika dola lakini kabla ya kufikiria kushika dola ni lazima vyama vitafakari juu ya agenda zao kisiasa zina mashiko kiasi gani? Je, zinashawishi na kunogesha hitaji la watu kwa wakati huo au ni agenda ilimradi ni agenda tu, ukirejea kwenye vyama vyetu vya upinzani hapa nchini vina ombwe la uwepo wa agenda inayoeleweka na kushawishi Watanzania licha ya kuwa na wanasiasa wasomi na wakongwe kwenye siasa za ndani na nje pengine mukwamo huu unatokana na siasa za umimi kwanza badala ya wao kwanza.

Ni wajibu wa vyama vya upinzani kujiuliza na kubuni agenda mama zenye mtiririko wa kuchomoza suluhisho la matatizo badala ya agenda za masilahi binafsi zenye kutaka kujinufaisha kimakundi kuliko watu walio wengi, kinachoonekana kwa sasa ndani ya vyama vya upinzani ni uwepo wa agenda za kusadikika badala ya agenda zenye dira na maudhui ya kiukombozi kwenye nukta ya falsafa ya maendeleo ya watu na vitu.

Upinzani umejikita kwenye kujenga agenda za kimatukio zaidi badala ya agenda endelevu na shindani kwa Chama Cha Mapinduzi ndipo kosa linapoanzia hapo, ili upambane na mifumo ya CCM kama chama kikongwe chenye mtaji wa itikadi, watu, falsafa na utambulisho wa sera za kujikomboa kwa watu wake lazima upinzani ujenge agenda kinzani zenye weledi na mbinu za usasa vinginevyo CCM itaendelea kushika dola na kujiimarisha kisiasa kwa miongo mingi ijayo.

Ipo wazi kuwa kisiasa agenda ni moyo na ramani muhimu ya kushika dola, agenda ni utambulisho muhimu wa chama chochote kile cha kisiasa kinachojitambua, agenda yenye nguvu huonyesha umaridadi wa chama cha kisiasa, mathalani unaweza usiwe mwanachama wa chama chochote cha kisiasa lakini agenda husika ikagusa kile unachokihitaji katika dhana ya maendeleo na hivyo ukaamua kuwapa ridhaa ya uongozi wenye agenda inayovutia zaidi.

Kwa ufupi agenda ushawishi na kujenga imani kwa wapiga kura, kwa mantiki hiyo agenda ni fursa na mwelekeo wa chama kushika dola.

Kisiasa maudhui ya agenda kushika dola ni kama pande mbili za sarafu huwezi kuzitenganisha kamwe, tunao wanasiasa wengi vijana kwa wazee wanaohubiri siasa za kushika dola na demokrasia ya kweli bila kuitambulisha agenda yao ni ipi?

Kisiasa huu ndio utapeli na uhuni kwa baadhi ya vyama vyetu na wanasiasa wake,  wanasiasa wetu wanajenga hoja za kushika dola sambamba na ombwe la ukosefu wa demokrasia bila kuitambulisha mantiki yao ya kiagenda ni nini katika kusudio la kuwatumia watu wawatume kuwatumikia kupitia hiyo dola.

Ni dhahiri kuwa siasa ni sayansi inayohitaji mikakati mbadala na yenye mipango inayoeleweka kimfumo, sayansi ya siasa na mifumo yake ni pamoja na agenda, agenda za upinzani ni kumjadili mtu badala ya mipango na mikakati ya vyama vyao, mathalani kwa kipindi hiki tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, agenda za baadhi ya vyama vikuu vya upinzani ni Dk. John Magufuli kwa Tanzania bara na Dk. Hussein Mwinyi kwa Zanzibar, huu ni utovu wa nidhamu kisiasa badala ya agenda mbadala zinajengwa hoja za kuwajadili watu.

Kisiasa huu ni uchovu ndani ya ulingo wa mapambano na badala yake tusitegemee kuona maajabu ya upinzani katika ushindani wa kushika dola, kwenda Ikulu si jambo jepesi kunahitaji mbinu na sayansi ya siasa  yenye agenda pana ndani yake iliyojitambulisha vyema kwa watu na si kujadili watu au mtu, siasa za kuwajadili watu kama agenda ya vyama huo ni umbea na unafiki usiokuwa na afya kwa maendeleo ya watu.

Wakati tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, tunahitaji vyama vya upinzani kuzitambulisha agenda zao kisiasa ambazo zitawapa fursa wapiga kura kuwapima kama wanafaa kupewa nafasi ya kushika dola, kwenda Ikulu kunahitaji uwezo na utambulisho ulio imara kiagenda, Ikulu si sehemu ya majaribio ya mfumo kuona kama unafaa au la hasha!

Tunahitaji upinzani imara unaoweza kuitambulisha agenda mama yenye dira ya kutuvusha kutoka hatua nyembamba kwenda hatua ya anga za mbali kimaendeleo, bila hivyo ni ngumu sana kwa wapinzani kuinusa dola kwa pua za kawaida kwa maana kuwa hoja ya vyama vya upinzani kushika dola inaongelewa na kuhubiriwa tu kienyeji kienyeji tu bila umakini wa aina yoyote ile.

HYPERLINK “mailto:dmutungid@yahoo.com” dmutungid@yahoo.com

0717-718619

The post Sijaiona agenda ya upinzani kuelekea Oktoba 28 mwaka huu appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *