img

Maradhi ya kisiasa huuweka utu, utaifa sokoni,on August 13, 2020 at 1:20 pm

August 29, 2020

NA ALOYCE NDELEIO MIGOGORO kadhaa katika ulingo wa siasa chimbuko lake linakuwa halifahamiki, inapenyeza na kuingizwa katika ajenda za kutofautiana kiitikadi miongoni mwa vyama vya siasa, papo hapo uchumi unayumba na huishia kuwa si mgogoro tena bali ni ugonjwa. Katika kuchimbuachimbua chimbuko la hali hiyo fikra zinaanzia katika hatua za awali za nchi kujitawala baada ya uhuru
The post Maradhi ya kisiasa huuweka utu, utaifa sokoni appeared first on Gazeti la Rai.,

NA ALOYCE NDELEIO


MIGOGORO kadhaa katika ulingo wa siasa chimbuko lake linakuwa halifahamiki, inapenyeza na kuingizwa katika ajenda za kutofautiana kiitikadi miongoni mwa vyama vya siasa, papo hapo uchumi unayumba na huishia kuwa si mgogoro tena bali ni ugonjwa.

Katika kuchimbuachimbua chimbuko la hali hiyo fikra zinaanzia katika hatua za awali za nchi kujitawala baada ya uhuru ambapo dhima kuu ilikuwa ni kudai utu na uhuru wa kuziweka rasilimali za jamii za ardhi, kodi  na kujiondoa mikononi mwa tawala za nje.

Awamu ya pili baada ya uhuru kwa maana ya kipindi cha sasa mtazamo umekuwa ni kwenye kipimo cha uhuru wa mtu kwa kipimo cha fedha hivyo kwamba thamani ya mtu imekuwa ni pesa.

Matabaka ya watu yameibuka na yameongezeka na yamekuwa yanatumiwa  kufanya kazi za siasa.

Miaka 15 iliyopita wakati akichangia mada iliyohusu nafasi ya vyama vya siasa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, uliokuwa umeaandaliwa na Asasi ya Maendeleo Tanzania (TADIP) Mhadhiri  kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema hali ya aina hiyo ni ugonjwa wa kisiasa.

Bashiru Ally ambaye hivi sasa ni Katibu Mkuu wa CCM, alifahamisha kuwa hali hiyo inayozikabili nchi za Afrika si wizi wa kura  bali ni maradhi ya kufanya utu na utaifa wa nchi kuwa sokoni na kwa hali hiyo hakuna siasa mbadala.

Alihoji ni taifa gani Afrika leo hii linaweza  kudai kuwa utaifa wake uko salama? Aliongeza kuwa hali zilizokuwa zimejitokeza katika nchi za Zimbabwe na Kenya hazikueleweka chimbuko lililosababisha vurugu na hata kuziingiza katika chaguzi za kijuujuu.

Alibainisha kuwa tatizo lililozikumba nchi hizo lilikuwa limejikita katika suala la ardhi na kubainisha zaidi kuwa haiwezekani kuzungumzia suala la wizi wa kura miongoni mwa nchi nyingi za Afrika bila kuhusisha rasilimali.

Kuhusishwa kwa rasilimali kunamaanisha kukosekana kwa mgawanyo ulio sawa na hivyo kuibuka kwa migongano ya kimasilahi, kwamba wakubwa wenye tamaa ya kutawala wasipoelewana madhara yake yanakuwa ndiyo kama hayo.

Alifahamisha kuwa tatizo la nchi nyingi za Afrika si wizi wa kura kwani hata ndani ya vyama vya upinzani kuna wizi wa kura, jambo ambalo limekuwa likisababisha chaguzi nyingi kuhitaji usimamizi wa mataifa ya nje.

Mantiki ya hali hiyo ni kwamba ardhi imekuwa inatumika au inasababisha  migogoro na kuifanya Afrika kuwa bara la watu dhalili.

Awali ilitumika kauli mbiu ya “Binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja” leo hii jambo hili limetoweka, ukoloni mamboleo  unapewa fursa,  utandawazi unachanua na umewateka viongozi wengi na hivyo  kuendelea kulifanya bara hili kuwa la watu  dhalili.

Pamoja na hali hiyo aliarifu kwamba moja ya hoja inayotumika sana miongoni mwa  nchi za Afrika, ni fedha za kuendeshea uchaguzi kwamba hazipo na hivyo kulazimu kuomba fedha kutoka nchi zilizoendelea.

Katika hali ya aina hii ni kuuweka utu wa jamii sokoni kwani fedha za uchaguzi au kuendesha masuala ya kisiasa zinatakiwa zitoke ndani na zipatikane ndani ya nchi.

Aliweka wazi kwamba chaguzi za nchi nyingi zimebakia kuwa si safi na hivyo kuzifanya kuwa ni chaguzi za vijisenti na zinapokuwa katika hali kama hiyo ni lazima hazitakuwa huru wala za haki.

Jambo muhimu ni kujenga fikra tofauti  badala ya kutegemea  fikra zisizo  na mbadala.

Hata hivyo alifafanua kuwa ili kuondokana na hali hiyo, ipo haja ya kujenga mambo ya msingi kwani mfano rahisi ulikuwa kwenye kambi za upinzani ambazo alisema zilikuwa na udhaifu wa kujenga hoja.

Alivigeukia vyama tawala kwamba navyo vilikuwa na udhaifu wa usikivu na hivyo vimekuwa vinatawala bila usikivu.

Alifahamisha kuwa vyama tawala vimekuwa vinachelewa kuyafanyia maamuzi masuala mbalimbali yanayoigusa jamii kulingana na usikivu wa hisia za wananchi.

Anatoa mfano wa masuala nyeti kama kashfa za ufisadi za Richmond na EPA na hivi karibuni suala la “vijisenti” ni mambo ambayo tayari yameshajenga hisia ya aina fulani ndani ya jamii.

Hisia za aina hii tayari zimeshaunda taswira ya matabaka ya walionacho na wasionacho na hivyo jamii ya tabaka la wasionacho moja kwa moja wanaona walishaporwa  rasilimali nyingi ambazo zimeingia katika mifuko ya walafi wachache na wangetaka  kuona wakiwajibishwa.

Katika mandhari ya aina hii anasema kuwa usikivu unaotakiwa ni ule wa kuwa na utashi wa kufanya maamuzi hata katika mazingira magumu.

Anabainisha kuwa kama mamlaka iliyopo ikiwa sikivu ikiwa na maana ya kuwajibika kwa hisia chanya za wananchi na hali  ikarekebika ni dhahiri mikanganyiko  inayokuwa imejikita ndani ya jamii inakuwa  imepata ufumbuzi.

Mwalimu Bashiru alipokuwa anachangia mada hiyo hakuna kiongozi wa chama wala kisiasa bali alikuwa mwana taaluma wa Sayansi ya Siasa, lakini leo hii ni kiongozi wa kisiasa akiwa Katibu Mkuu wa chama tawala.

Haiyumkini anayaishi na kuyatenda yale aliyoyasema miaka 15 iliyopita kwa kushauri kuachana na kuomba fedha za kuendesha masuala ya siasa na badala yake fedha hizo zipatikane ndani ya nchi.

Inapoelezwa kuwa Serikali imesema kuwa uchaguzi wa mwaka huu 2020 kwamba utatumia fedha za ndani na si fedha za kuomba kutoka nje, hatua hiyo inaendana na kile alichokisema Mwalimu Bashiru kuwa ni jambo muhimu kujenga fikra tofauti  badala ya kutegemea fikra zisizo na mbadala.

Haiyumkini pia kwamba akiwa kiongozi wa chama atakuwa tayari ameshaweka mambo sawa kwa kile alichokisema kwamba vyama tawala mara nyingine vina udhaifu wa usikivu, hutawala bila usikivu na huchelewa kuyafanyia maamuzi masuala mbalimbali yanayoigusa jamii kulingana na usikivu wa  hisia za wananchi.

Pamoja na hali hiyo yote maradhi ya kisiasa yamekuwa yakichochewa pia na kirusi hatari cha rushwa inasadifu kusema kuwa kirusi hicho ndicho kinachopindisha haki kwani umma pindi unapouliza maswali sahihi na kukosa maamuzi sahihi kutoka kwa wanasiasa.

Kwa vyovyote vile mikakati ya chaguzi ikifanyika na kuhitimishwa kwa uhuru na haki basi inakuwa ni tiba ya maradhi ya  kisiasa ya kuweka utu na utaifa wake sokoni.

The post Maradhi ya kisiasa huuweka utu, utaifa sokoni appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *